Haya tu mambo matano Liverpool bila Salah, Mane na Keita

Friday January 14 2022
Liver PIC

LIVERPOOL. MAMBO si mazuri sana kwa klabu nyingi barani Ulaya kwa sababu wachezaji wao wengi tegemeo wameondoka kurejea Afrika kwa ajili ya kutumikia mataifa yao kwenye michuano ya Afcon.

Kwa upande wa Liverpool imekuwa moja kati ya timu zilizoathirika zaidi kwa sababu wachezaji watatu tegemeo hawapo ikiwa pamoja na Mohamed Salah, Sadio Mane na Naby Keita.

Mbali na wachezaji hao, Liverpool imekuwa na mastaa wengine ambao wamekumbwa na majeraha na miongoni mwao wanaugua corona.

Mwanaspoti linakuletea mambo matano ambayo yanaweza kuiokoa timu hiyo katika kipindi hiki ambacho wachezaji hao hawapo.


Firmino asogee mbele

Advertisement

Licha ya wachezaji wengine kucheza vizuri kwenye mchezo wa FA dhidi ya Shrewsbury, Firmino alikuwa mmoja kati ya wachezaji ambao walikuwa injini ya Liverpool

Hata hivyo, hakuonekana kwenye mechi dhidi ya Chelsea kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Firmino anaonekana kurejea kwenye kiwango chake na ndiye anayeweza kutumika kama mchezaji tegemeo kwenye ufumaniaji wa nyavu.

Hapa unaweza kutumika mfumo wa 4-3-3 ambapo kwenye wachezaji watatu wa safu ya ushambuliaji ambapo atakuwa mshambuliaji wa mwisho akiwa na kazi ya kuifanya timu ipate mabao kama ilivyokuwa kwa Salah na Mane.


Minamino asikae nje

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp kuna wakati hutumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao hubadilika kuwa 4-5-1 au 4-2-4 pale timu inapokuwa na mpira au la.

Kutokana na kasi yake Firmino anaweza kucheza katika eneo la winga wa pembeni na akasaidia sana Liverpool katika kutoa pasi za mwisho kwa straika ambaye atakuwa kwenye eneo la mwisho ama Diogo Jota au Divock Origi.

Kwenye mchezo uliopita dhidi ya Shrewsbury, Klopp alijaribu kumpa majukumu ya aina hiyo staa huyu kutoka Japan na akaonyesha kumudu vyema licha ya kuwa ametoka kwenye majeraha.

Hivyo ikiwa atampa nafasi supastaa huyu atakuwa amepunguza kwa asilimia fulani pengo la mastaa wanaokosekana kwenye kikosi.


Trent kuwa kiungo

Licha ya Klopp kuonekana kulipinga suala hili awali, lakini wataalamu wa mambo wanadai kwamba staa huyo ana uwezo mkubwa wa kucheza kwenye safu ya kiungo kwa sababu ameshawahi kucheza katika eneo hilo akiwa na timu za vijana za Liverpool.

Katika eneo la kulia wanaweza kucheza Neco Williams ambaye anakuwa beki, wakati Oxlade-Chamberlain akiwa winga ili kumpa nafasi Trent kusogea mbele zaidi na kuungana na viungo wengine wawili.

Hapa itasaidia timu kutokuwa inapokea mashambulizi mengi kwa sababu Trent ana uwezo mkubwa wa kuzuia mashambulizi, hivyo kutakuwa na ‘pressing’ ya kutosha kwenye eneo la kiungo la Liverpool kwenda timu pinzani, jambo ambalo litawafanya wapinzani wao kutokuwa kwenye nafasi nzuri ya kutuma mashambulizi ya mara kwa mara kwa wababe hao kutokana na presha watakayokuwa wanapewa.


Kazi kwake Origi

Ni kweli kwamba Divock Orogi amekuwa hapati nafasi ya kutosha kucheza katika kikosi cha kwanza cha Liverpool mbele ya Mane na Salah.

Lakini, kukosekana kwao inaweza kuwa nafasi ya staa huyu kuonyesha makali kwenye mechi zijazo ambapo Klopp anaweza kumchezesha sambamba na Jota na Firmino kwenye sehemu ya ushambuliaji.

Origi ameonyesha kiwango bora kwenye mechi kadhaa zilizopita, hivyo anaweza kuwa msaada kwa timu katika kipindi hiki cha mpito. Kutokana na hilo moja ya mifumo ambayo inaweza kutumika ili kupata kile kilicho bora zaidi kwa Origi ni ule wa 4-3-3.


Kumuamini Gordon

Kaide Gordon anaweza kuwa mbadala kwenye safu ya ushambuliaji ya Liverpool ikiwa ataaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha wababe wa Anfield.

Staa huyu mwenye umri wa miaka 17 alifunga bao kwenye mchezo wa FA Jumapili iliyopita dhidi ya Shrewsbury Town.

Kiwango chake kwenye mechi kilionyesha kuwa ni mmoja wa wachezaji wanaoweza kuja kuonyesha mambo makubwa ikiwa watapewa nafasi kama ilivyo kwa Trent na kuna matumaini makubwa Klopp anaweza akampa nafasi kubwa zaidi ya kucheza kwa sababu anaamini zaidi kwa vijana.

Advertisement