Hawazuiliki.. Wamehusika na mabao Ligi Kuu

Thursday July 15 2021
nyota pic
By Ramadhan Elias

NYOTA wa Barcelona na timu ya Taifa la Argentina Lionel Messi (34) ni mchezaji mwenye uwezo wa kutengeneza nafasi za mabao (asisti) na kufunga kwa kiwango cha hali ya juu muda wowote.

Messi alianza soka na timu za vijana za Barcelona na 2014 akiwa na miaka 17 alipandishwa timu ya wakubwa.

Kuanzia hapo ubora wake wa kupachika mabao na kutengeneza nafasi ulijionyesha kuwa mkubwa kwani hadi sasa ameifungia zaidi ya mabao 470 kwenye mashindano yote huku akitengeneza nafasi kibao. Sahau kuhusu Messi wa Barcelona, safiri zaidi ya maili 4075 hadi Tanzania nchi ambayo lugha pendwa ni Kiswahili na Simba na Yanga ndizo timu zenye wafuasi wengi zaidi.

Huku wapo jamaa kibao wenye uwezo kama wa Messi na wanakiwasha kinoma kwenye Ligi Kuu Bara, na kupitia makala haya tunakuletea wachezaji 10 ambao kila timu ikiwa imebakiza mechi mbili kumaliza ligi, wamehusikana mabao mengi ya timu zao kwa kutengeneza nafasi na kufunga.


CLATOUS CHAMA (23)

Advertisement

Anacheza Simba na ndiye anaongoza kutengeneza mabao mengi kwenye ligi akihusika nayo 23 hadi sasa.

Pia hadi sasa ameifungia Simba mabao nane na kutoa asisti 15 ambazo zinamfanya kuwa kinara katika chati ya kuhusika na mabao mengi.


PRINCE DUBE (19)

Mzimbabwe huyu anayekiwasha Azam FC amekuwa wamoto kinoma.

dube pic

Licha ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, Dube ameonyesha kuwa sio mnyonge kwani amehusika na mabao 19 ya Azam hadi sasa.

Dube ana mabao 14 nyuma ya John Bocco wa Simba aliyefunga 15 huku akiwa ametoa pasi za mabao tano.


LUIS MIQUISSONE (19)

Winga huyu kutoka Msumbiji ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vyema zaidi msimu huu akiwatumikia Simba.

Hadi sasa amehusika na mabao 19 sawa na Dube tofauti ikiwa kwenye mabao ya kufunga na asisti.

Luis ameifungia Simba mabao tisa huku akitoa asisti 10 kwa wenzake hadi sasa Simba ikitangazwa kuwa bingwa wa ligi msimu huu kwa mara ya nne mfululizo.


IDDI SELEMAN ‘NADO’ (18)

Winga huyu machachari wa Azam ni mchezaji mzawa aliyehusika na mabao mengi msimu huu hadi sasa, akihusika nayo 18, akiwa amefunga tisa na kutoa asisti tisa hadi sasa jambo linalomfanya kuwa kinara wa mafundi wa kutengeneza mabao msimu huu.


BOCCO (17)

Nahodha huyu wa Simba naye ameingia kwenye chati ya wachezaji waliohusika na mabao mengi msimu huu - 16 hadi sasa.

Bocco amefunga mabao 15 na kutoa pasi mbili kuisaidia Simba kuwa bingwa.


CHRISS MUGALU (15)

Mkongomani huyu naye hashikiki. Huu ni msimu wake wa kwanza kwenye ligi hiyo na ameonyesha ubora kwa kuhusika na mabao 15 Simba.

Mugalu amefunga mabao 13 na kutoa asisti mbili.


DANNY LYANGA (14)

Straika huyu wa JKT Tanzania ni miongoni mwa wazawa waliohusika na mabao mengi (14) ya timu yake.

Lyanga ameifungia timu hiyo mabao tisa na kutoa assisti tano zilizozaa mabao.


YACOUBA SONGNE (12)

Nyota huyu kutoka Burkina Faso hadi sasa Yanga ameingia kwenye chati akihusika kwenye mabao 12 sawa na Deus Kaseke tofauti ikiwa mabao ya kufunga na asisti.

yacoub pic

Yacouba ikiwa ni mara yake ya kwanza kucheza Tanzania amefunga mabao nane na kutoa asisti nne Ligi Kuu.

KASEKE (12)

Winga huyu mzawa msimu huu umekuwa bora kwake kwani amechangia moja kwa moja kwenye mabao 12 ya Yanga.

Kaseke ameifungia Yanga mabao sita hadi sasa na kutoa asisti sita na kuifanya timu hiyo ikae nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.


MESHACK ABRAHAM (12)

Mshambuliaji huyu wa Gwambina ni miongoni mwa waliohusika na mabao mengi ya ligi msimu huu akiwa ameshiriki kwenye mabao 12 ya chama lake ambalo linashiriki ligi kwa mara ya kwanza msimu huu.

Abraham ameifungia timu yake mabao tisa hadi sasa na kutoa asisti tatu zilizozaa mabao.

Advertisement