Hawa jamaa hata Wenger anaenjoi

Muktasari:
- Akizungumza kwenye video ya TikTok ya @goalglobal, bosi huyo wa FIFA wa masuala ya maendeleo ya soka duniani, alitakiwa kuwataja kwa namba wachezaji watano ambao anafurahia kuwatazama wakicheza kwa sasa.
PARIS, UFARANSA: GWIJI wa Arsenal, Arsene Wenger ametaja wachezaji watano ambao anafurahia kuwatazama wakiwa wanacheza mwaka huu 2025 – huku orodha hiyo ikiwahusu masupastaa wa Real Madrid, Barcelona na Liverpool.
Akizungumza kwenye video ya TikTok ya @goalglobal, bosi huyo wa FIFA wa masuala ya maendeleo ya soka duniani, alitakiwa kuwataja kwa namba wachezaji watano ambao anafurahia kuwatazama wakicheza kwa sasa.
Katika tukio la kumfanya asionekane mwenye upendeleo, Wenger alisema hatakwenda kumtaja mchezaji yeyote wa Arsenal, lakini hakuna ubishi kwenye kikosi hicho cha Emirates, mmoja wa wachezaji ambao wanamkosha kocha huyo wa zamani wa Washika Bunduki ni Bukayo Saka.
Hii hapa orodha ya mastaa watano wanaomkosha Wenger ndani ya mwaka huu wa 2025.
5. Lamine Yamal
Fikiria kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2006, wakati Barcelona ilipoichapa Arsenal ya Wenger, Yamal alikuwa hajazaliwa. Kwa kifupi tu, kinda huyo matata zao la La Masia alikuwa na umri wa miaka 10 wakati Wenger anaachana na Arsenal mwaka 2018.

Hadi sasa tayari amekuwa mmoja wa washambuliaji hatari duniani, akiisaidia timu yake kuvuka kwenye hatua ya mtoano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufunga na kuasisti kwenye mechi ya hatua ya 16 bora dhidi ya Benfica.
4. Cole Palmer
Staa huyo wa Chelsea kwa sasa yupo kwenye kipindi kigumu cha kufunga mabao na kuasisti, lakini ni mmoja wa wachezaji wenye vipaji vikubwa sana kwa kile alichokionyesha kwa miezi 18 iliyopita tangu alipojiunga na Stamford Bridge.

Palmer, 22, amejipambanua kama mmoja wa wachezaji bora kabisa kwenye kizazi hiki tangu alipoondoka Manchester City kwenda Chelsea kupata nafasi ya kucheza. Palmer amefunga mabao 39 na kuasisti 21 katika mechi 78 alizochezea The Blues.
3. Vinicius Junior
Wenger alimtaja staa wa Kibrazili, Vinicius Junior, ambaye ni mmoja wa wachezaji ambao pengine wanaweza kushinda tuzo ya Ballon d’Or.

Vinicius hakuwa kwenye kiwango bora tangu aliposhindwa kushinda kubeba tuzo hiyo ya ubora wa duniani, Oktoba mwaka jana, lakini amekuwa akifanya mambo ya maana katika kuisaidia timu yake ya Real Madrid kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Amekuwa mchezaji wa kufanya vizuri kwenye mechi kubwa na ameshafunga mabao kwenye fainali mbili tofauti za Ligi ya Mabingwa Ulaya jambo linalomfanya Wenger kuvutiwa na kumfuatilia.
2. Kylian Mbappe
Mfaransa pekee kutokea kwenye orodha hii ya Wenger, ambaye ni Mfaransa pia. Huwezi kushangaa kusikia jina la Mbappe, kwa sababu ni mchezaji ambaye Wenger mwenyewe alijaribu kutaka kumsajili kipindi hicho alipokuwa bado kinda.
Kipindi hicho Mbappe alipokuwa Monaco, Kocha Wenger alipokuwa akiinoa Arsenal alijaribu kunasa saini ya mchezaji huyo, lakini kwa bahati mbaya alishindwa kumsajili.

Baadaye, Mbappe alitimkia zake Paris Saint-Germain na kucheza hapo kwa mafanikio makubwa kabla ya kubamba dili la kwenda kujiunga na Real Madrid, ambako amekuwa moto kwa sasa.
1. Mohamed Salah
Wenger ameondoka kwenye Ligi Kuu England, lakini amekuwa akifuatilia ligi hiyo kutokana na kuwapo wachezaji wanaomkosha na anapenda kuwatazama.

Mmoja wa wachezaji hao ni supastaa wa Liverpool, Mohamed Salah. Mo Salah mwenyewe amekuwa na heshima kubwa kwa kocha huyo na hata kukubali ushauri wa masuala mbalimbali ya kisoka anayoambiwa na nguli huyo.
Mo Salah mara nyingi amekuwa akielekezwa baadhi ya mambo ya Wenger jambo ambalo limemfanya kuwa hodari sana ndani ya uwanja.