Hassan Dalali, Field Marshal wa Simba anayechapika

HATA kama hapewi heshima yake, lakini ukweli ndivyo ulivyo, Hassan Dalali ‘Field Marshal’ ana alama nyingi alizoacha ndani ya Simba, tangu akiwa mwenyekiti wa matawi ya Simba mkoa wa Dar es Salaam mpaka kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo kongwe nchini.

Kwa sasa wanamsimbazi wote akili yao ipo kwenye maandalizi ya tamasha lao la kibingwa la Simba Day litakalofanyika Septemba 19, jijini Dar es Salaam, lakini huwezi kuchekelea tamasha hilo kama humtaji Dalali, kwani yeye ndiye muasisi wake aliyelianzisha mwaka 2009.

Licha ya kubezwa kuwa ni kati ya wenyeviti waliowahi kuiongoza Simba bila ya kuwa na elimu kubwa, lakini kazi kubwa aliyoyafanya enzi za uongozi wake, imeifanya Simba ya leo kutembea kifua mbele na kutamba mbele ya wapinzani wao, kwa sababu ya hekima, busara na uamuzi mgumu wa mzee huyu.

Mzee huyo aliyejaa busara, mcha Mungu, mnyenyekevu na mkarimu kwa ugeni, alitembelewa na timu ya Mwanaspoti anakoishi kwa sasa kwa binti yake eneo la Mbagala Maji Matitu, jijini Dar es Salaam.

Ilishtua kidogo kuona Dalali ameenda kuishi kwa bintiye aliyeoelewa, ilhali ana maskani yake eneo la Magomeni Makanya, ndipo tulipopata mkasa ambao unaonyesha namna gani Field Marshal huyo anavyochapika kimaisha na akafunguka mambo mengi ambayo kwa mtu mwenye roho nyepesi lazima utokwe na machozi, hii ni kutokana na tofauti na ukubwa wa jina lake kwa wanamichezo hususani wana Msimbazi.

Pia amefichua kiu yake ya kuona uwanja alioupigania na kuupata kule Bunju ukikamilika kama alivyokuwa akitamani ili siku moja Simba iwe inacheza kwenye uwanja wake kama ilivyo Azam ama timu nyingine kubwa barani Afrika. Ebu tiririka naye katika katika mahojiano haya maalum...!


NDOTO ZAKE

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Simba anasema anapenda kuona mambo mengi aliyoyapigania kama kiongozi ndani ya Simba yanatimia na kuyashuhudia angali hai.

“Umri wangu umekwenda kwa sasa, nimezeekea Simba na ninatamani kuona ile ndoto waliyonayo wanachama takribani Tanzania nzima ya uwanja kukamilika inatimia,” anasema.

Anasema alinunua uwanja huo chini ya uongozi wake, ukaja ukaendelezwa na aliyefuata uongozini, yaani Ismail Aden Rage.

Anasema anatamani kuja kuinoa Simba inayojitegemea kwa kila kitu na kujiendesha kama klabu nyingine kubwa barani Afrika, ingawa tayari dalili zimeanza kuonekana chini ya Mohammed ‘Mo’ Dewji.


CHIMBUKO LA SIMBA DAY

Tamasha hili kubwa la utambulisho wa jezi na kikosi kipya cha msimu litakaloofanyika Septemba 19 mwaka huu, ni wazo la Dalali na wenzake walipokuwa madarakani, ambao waliingia uongozini mwaka 2007 hadi 2010 alipompisha Rage.

Anasema wazo hilo alilipata baada ya kuzunguka katika matawi mbalimbali ambapo wanachama walikuwa na kiu ya kuwa na uwanja wao.

“Ni wazo ambalo lilikuja likiwa na lengo la kutaka kuwakutanisha wanachama na mashabiki pamoja ili kubadilishana mawazo na kujipanga kwa msimu mpya, sikuwahi kuota kama lingekuja kuwa kubwa kama ilivyo leo.

“Nilipopata wazo hilo nikawashirikisha viongozi wenzangu ambao awali walinipinga, lakini sikukata tamaa hadi lilipofanyika na walipoona faida yake walianza kuniunga mkono,” anasema Dalali na kuongeza;

“Katika tamasha hilo la kwanza tulipata Sh70 milioni ambapo Sh20 milioni nikazipeleka kwenye Uwanja wa Bunju, katika hilo namshukuru sana Mwina Kaduguda (aliyekuwa Katibu Mkuu wakati huo) maana aliandika barua ya kuomba uwanja huo serikalini, nakumbuka barua hiyo tulilipa elfu tano (Sh5,000).”

Anasema waliialika timu ya SC Villa ya Uganda baada ya kushindwana dau la Sh300 milioni na Zamalek ya Misri.

“Kipindi hicho Zamalek ilikuwa kubwa sana, lakini pia sitamsahau marehemu Ruge Mutahaba ambaye alitumia kituo chake cha redio kulitangaza tamasha,” anasema Dalali.

Anasema anachofurahia ni kwamba baada ya misimu kadhaa hatimaye tamasha lao likaanza kuigwa na timu ya kwanza ikiwa ni Ndanda mwaka 2014, ambapo waliialika Simba kwenda kucheza nao mechi ya kirafiki na anakiri ilipata pesa ya kutisha.


ALIISHAURI YANGA

Licha ya Simba na Yanga kuwa wapinzani wakubwa wa jadi, lakini alisema kufana kwa tamasha lao na kuonekana faida zake, aliwashauri watani wao hao nao kuwa na tamasha lao ambapo ilipita miaka tisa kabla ya kukubaliana na wazo hilo na leo nao wana Wiki ya Mwananchi.

“Kuiga sio jambo baya, niliwaambia sana Yanga wawe na Yanga Day ambayo sasa hivi inawaingizia mamilioni ya pesa, iliwachukua miaka tisa kukubaliana na hilo, hivyo kwa upande mwingine najivunia kwamba nimesaidia hata Yanga nao kuwa na tamasha lao, huku Azam nao wakilifanya mwaka jana.”


ALAMA ALIZOACHA SIMBA

Dalali kama viongozi wengine wanaopita ndani ya klabu za soka na hata kwenye siasa, ameacha alama anazojivunia ikiwamo kuipambania Simba kupata wadhamini kipindi hicho ikiwa choka mbaya, lakini kuanzisha timu ya vijana ya Simba B, Simba Queens, kadi za kisasa na kuboresha ana za uanachama sambamba na uwanja unaofahamika kama Mo Simba Arena.

Anasema wakati anaondoka Msimbazi kumpisha Rage alikabidhi magari matatu, mikataba ya udhamini ya TBL, Push Mobile, Nsejere Sports & Casual Wear ya USA na hati ya kiwanja cha Bunju ambacho leo kuna Mo Simba Arena.

Anakumbuka Simba kupata udhamini kipindi hicho ikitegemea zaidi misaada na huruma ya Kundi la Friend’s of Simba ambao hata hivyo hawakukubalika mbele ya baadhi ya wanachama hususani, Simba Taleban. Anasema; “Kuna kiongozi mkubwa wa serikali (jina kapuni) aliniona nimepanda daladala, akawatuma watu ili niende kukutana naye Dodoma, nikasafiri hadi huko, baada ya kufika ofisini kwake, akaniambia mimi ni mtu mkubwa sana kwa nini napanda daladala,” anasimulia Dalali na kuongeza;

“Kisha akasema nitaje gari ninalopenda kutembelea, nikamjibu sitaki hilo, akasema nitoke nje nikatafakari, nilifanya hivyo kama mara tatu, ikabidi aniulize nataka nini, nikamjibu nataka udhamini kwenye timu yangu.”

Anasema kiongozi huyo alishangazwa kuona hajataka kujitanguliza, hivyo alikubaliana na ombi lake, ambapo alimuandikia barua na kumgongea mhuri wa serikali kwenda kwa uongozi wa kiwanda cha bia cha TBL.

“Niliona kama nachelewa, nilipanda lori usiku huo huo kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, mkono wangu haukubanduka mfukoni nilikuwa nahofia barua isije ikadondoka, saa 12:00 asubuhi nilikuwa nimefika katika ofisi zao, nikakutana na mlinzi aliyeniambia hawafungui muda huo, nisubiri hadi saa 2:00 asubuhi,” anasema Dalali na kuongeza;

“Mabosi walifika nikawapa ile barua, baada ya kuona mhuri wa serikali, hawakutaka kuniuliza mengi, waliniambia wamekubali kunipa udhamini ila nikaongee na viongozi wa Yanga ili watupe kwa pamoja, nikampigia simu Imani Madega wakati huo akiwa ndiye mwenyekiti wa Yanga naye akaafiki na akaja tukasaini mikataba, moja ya vitu walivyotoa ni yale mabasi ya timu.”

Ukiachana na hilo, analitaja tawi la Friends of Simba namna lilivyowajibika kuhudumia timu kwa kutoa pesa zao mfukoni.

“Tawi hilo limefanya makubwa mno Simba, lilisajili wachezaji, lililipa mishahara, yaani walijitoa kwa hali na mali, wanastahili kukumbukwa na kupongezawa,” anasema.

Anasema yeye alikuwa kwenye tawi la Ngurumo za Simba, ambapo baadaye gazeti la timu lilipoanzishwa liliitwa jina hilo. Tawi hilo kwa sasa linaitwa Mpira Pesa.

Pia anasema baadhi ya viongozi ambao walifanya kazi kubwa ni Zakaria Hans Pope, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Evans Aveva aliowaelezea walikuwa hodari kwa skauti ya kupata wachezaji wazuri.

“Simba B ndio iliyowatoa hawa kina Jonas Mkude, Christopher Edward, Ibrahim Ajibu, Abdallah Seseme, Said Ndemla, Haruna Chanongo na wengine hao viongozi walifanya kazi kubwa sana, chini ya Patrick Rweyemamu na makocha mbalimbali waliowahi kuinoa timu hiyo ya vijana kama Amri Said, Seleman Matola na wengineo.”

Anasema Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alihusika kwa asilimia kubwa kuwalea vijana hao, akitoa pesa na muda, jambo analoshauri uongozi kumtazama kwa jicho la pekee.

“Simba B yenye nguvu Rweyemamu amehusika asilimia kubwa sana, waulize hao kina Mkude, Ajibu watasema namna alivyowalea kama watoto wake,” anasema.

Anaongeza skauti walizokuwa wanafanya ziliwasaidia kuwa na timu iliyokuwa inadumu kwa pamoja muda mrefu na tishio katika ligi ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.


UBINGWA BILA KUFUNGWA

Dalali anasema hakuna kitu anachojivunia kama kuisaidia timu yao kunyakua ubingwa bila kupoteza mchezo wowote, rekodi ambayo mpaka sasa haijawahi kufikiwa na uongozi wowote wa Msimbazi, ingawa rekodi hiyo katika Ligi Kuu Bara iliwahi kuvunjwa na Azam walipotwaa ubingwa wao wa kwanza na wa pekee.

Simba ilitwaa ubingwa huo msimu wa 2009-2010 kwa kucheza mechi 22, ikishinda michezo 20 na kutoka sare mbili, huku ikifunga mabao 50 na kuruhusu 12 na kukusanya pointi 62, Azam wao wakaja kulipa 2013-2014, walipocheza mechi 26 kushinda 18 na kutoka sare nane, ikifunga mabao 51 na kufungwa 18 na kuvuna pia alama 62 kama ilivyofanya Simba.

“Tangu hapo hakuna kikosi ambacho kimewahi kuvunja rekodi hiyo ndani ya Simba na najivunia hilo, kwani kwa mazingiara ya sasa ya soka la ushindani ni mtihani mkubwa,” anasema.


YANGA KUWAKIMBIA

Anasema katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), kutafuta mshindi wa tatu Yanga iliwakimbia Simba 2009 kwa madai wamepotea njia ya kwenda Uwanja wa Uhuru na badala yake wakajikuta Kimbiji.

“Nilimpigia simu Madega kwamba kwanini hamjafika hadi sasa uwanjani, akaniambia tumepotea tupo Kimbiji, Simba ilikuwa ya moto wangepigwa nyingi, basi tukapewa ushindi, ndio maana sikushangaa msimu uliopita kuondoa timu uwanjani,” anasema.


KOMANDOO HADI MWENYEKITI

Haikuwa safari rahisi ya Dalali kuwa mwenyekiti wa Simba mwaka 2007-2010. Alianzia kwenye ukomandoo miaka ya 80, ambapo alifanya mambo mengi ya kuisaidia timu.

“Nimewahi kufanya umafia nikiwa komandoo, Simba ilifungwa na Mecco ya Mbeya mabao 2-0 ilikuwa ya moto ambapo kina Abeid Kasabalala ndio walikuwa mastaa, viongozi walikuwa hawataki kuachia ngazi wakati timu ilikuwa imepata matokeo mabaya kwa mfululizo,”a nasema Dalali na kuongeza;

“Tulitoka Dar es Salaam hadi Tukuyu kwenda kuiteka timu, tulienda na dereva Hassan Mbashiri tukiwa na fimbo za kuwatandikia viongozi, tukachukua timu na kurudi nayo jijini, ambapo tuliweka kambi Temeke katika hoteli ya aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba, Yusuf Hazal, yote hayo nilijitoa kuhakikisha timu inafanya makubwa,” anasema.

Inaendelea kesho