Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hapa pesa tu

Muktasari:

Tanzania ilikuwa mwenyeji na ilimaliza nafasi ya tatu, huku Uganda ikiibuka kidedea kwa kunyakua taji na kukata tiketi ya kuiwakilisha kanda hiyo katika fainali zijazo za Afcon U17 2019 zitakazofanyika hapa nchini.

KAMA kuna kipindi mashabiki wa soka walipata burudani, basi ni kwenye michuano ya Afcon U17-Kanda ya Cecafa.

Unajua kwa nini? Timu ya vijana U17, Serenget Boys ilikuwepo na zaidi ni kazi waliyokuwa wakiipiga kwenye michuano hiyo. Ilikuwa ni burudani tosha.

Tanzania ilikuwa mwenyeji na ilimaliza nafasi ya tatu, huku Uganda ikiibuka kidedea kwa kunyakua taji na kukata tiketi ya kuiwakilisha kanda hiyo katika fainali zijazo za Afcon U17 2019 zitakazofanyika hapa nchini.

Serengeti Boys chini ya Kocha Oscar Milambo, ilionekana kukamilika kila idara, licha ya dosari chache zilizowanyima nafasi ya kutinga fainali kwa kukubali kipigio cha mabao 3-1 kutoka kwa mabingwa Uganda.

Hata hivyo, ndani ya kikosi hicho kuna nyota ambao kama wataendelea na kasi yao katika kusukuma gozi, wanaweza kuuzika kokote ndani na nje ya nchi kwa soka wanalolipiga.

Mwanaspoti linakutajia baadhi ya nyota hao ambao ni hazina kwa taifa na wana kila dalili za kufuata vyayo za kina Mbwana Samatta, Simon Msuva ama Abdi Banda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, iwapo vipaji vyao vitaendelezwa zaidi.

Hassan Kimwaga-Kipa

Huyu ndiye aliyekuwa mhimili wa Serengeti kwa kulilinda vyema lango la timu hiyo.

Katika michuano hiyo ya Cecafa alifanya kazi kubwa ya kuokoa hatari nyingi ambazo zilielekezwa langoni kwake na wakati mwingine kwa makosa ya mabeki wake yaliyowapa nafasi wapinzani kulisogelea lango.

Kiwango chake kiliwafanya baadhi ya wadau wa soka nchini, wawe wanamtazama kwa jicho la tatu na baada ya miaka kadhaa anaweza akaingia katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kama ilivyokuwa kwa Ramadhan Kabwili.

Salum Lupepo- beki

Alikuwa imara sana eneo la ulinzi kuhakikisha anaokoa hatari zilizokuwa zinaelekezwa kwao na kati ya sifa alizonazo ni utulivu na umakini wa kutochelewesha mpira eneo la kipa wao.

Utulivu wake unaweza ukamsaidia kupata timu Ligi Kuu na hata kwenda kucheza nafasi ya kwanza moja kwa moja, hata hivyo kujengwa kwa fikra kunaweza kumsaidia akazidi kuwa bora kwa miaka ijayo na hata kuuzwa nje ya nchi.

Jefferson Olivertwist-Kiungo

Anajua kupiga pasi zenye macho, ngumu kumnyang’anya mpira anapokuwa nao mguuni, hilo liliwafanya mashabiki waelekeze mapenzi kwake na kuburudika na kazi yake wakati wa michuano hiyo.

Pasi zake zilikuwa zikiwasaidia washambuliaji Kelvin John na Agiri Ngoda kufanya kazi yao kwa wepesi kwasababu walikuwa wakipigiwa pasi rula kwani kiungo cha Serengeti kilikuwa kimekamilika kupitia Jefferson na Morice Abraham.

Morice Abraham -kiungo

Anastahili kupewa beji ya unahodha kutokana na kazi nzuri aliyoifanya kwenye michuano hiyo alipokuwa uwanjani, kwanza kucheza kwa ustadi wa hali ya juu, pia kuwa kiongozi mzuri kwa wenzake.

Aliwahi kuidokezea Mwanaspoti ipo siku kikosi hicho kitaleta mapinduzi ya soka kwa madai wana kiu ya kuona wanafika mbali hasa kucheza AFCON ya Dunia.

“Watanzania watuamini na kutupa nafasi na kutuunga mkono kama wanavyofanya kwenye kikosi cha Taifa Stars, tutafanya kitu cha tofauti, tuna nia na hamu ya kuona tunapeperusha vyema bendera ya Taifa,” alikaririwa.

Kelvin John-Straika

Kutokana na kiwango alichokionyesha alipachikwa jina la kinda aliyekuwa mdogo zaidi kwenye Kombe la Dunia, Kylian Mbappe kutokana na namna alivyokuwa analijua goli.

Hata makocha mbalimbali wa timu pinzani walikikubali kiwango chake akiwemo Kocha wa Rwanda, Rwasamanzi Yves, aliyempigia saluti Kelvin na kumtabiria atacheza Ulaya.

Kutokana na kiwango chake alipewa kiatu cha uchezaji bora wa mashindano hayo akiwa ametupia kambani mabao sita.

Agiri Ngoda-Straika

Huyo naye alikuwa habari nyingine ni fundi wa kutoa pasi za kufunga, anafunga na mpambanaji, kiwango chake kilikuwa na mvuto machoni kwa wadau wengi wa soka ambao walikuwa wanafika uwanjani kuiunga mkono Serengeti.

Kombinesheni yake na Kelvin John ilikuwa na msaada mkubwa katika timu hiyo, lakini kama ikipatikana pacha nyingine inaweza kunogesha zaidi timu hii na kuwa bora hata pale wachezaji fulani wanapokosekana katika kikosi hicho.

Kama kipaji chake kitalindwa na kuendelezwa, sio ajabu kumuona akiwafuata kina Shaaban Idd Chilunda na Farid Mussa kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya.