Gwambina, maji kupwa maji kujaa!

ULE usemi wa kutesa kwa zamu unaweza kutumika kwa Kocha wa Gwambina, Mohammed Badru ambaye siku chache zilizopita alishinda tuzo ya Kocha Bora wa Mwezi Marchi Ligi Kuu Bara. Badru alinyakua tuzo hiyo ya Machi akiwapiga bao, Juma Mwambusi aliyekuwa Yanga, Didier Gomes wa Simba na hata George Lwandamina wa Azam FC.

Licha ya ugeni wake kwenye Ligi ndani ya muda mfupi, Machi mambo yalimwendea vizuri kocha huyo, Mzanzibar kwani aliongoza Gwambiana kuvuna pointi saba, ilikuwa ni baada ya kuzifunga ugenini, Ihefu (2-1) na Mtibwa Sugar (2-0) huku wakitoa suluhu (0-0) nyumbani dhidi ya Maafande wa Polisi Tanzania.

Gwambina ilijikuta ikipanda kwa kasi kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara huku ikiziacha nafasi za chini Mwadui, JKT Tanzania, Mbeya City na Kagera Sugar.

Baada ya kutoka kwenye siku 21 za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli wakaonyesha kuwa bado wapo ngangari kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Ule usemi wa kutesa kwa zamu ukaanza kuchukua nafasi yake, Aprili 16 ambapo alijikuta akipoteza kwa mabao 3-0, akiwa na matumaini ya walau kupata sare dhidi ya Yanga, Aprili 20 mambo yaliendelea kumwendea kombo kwa kutandikwa tena mabao 3-1 kisha kuchapwa tena na Simba 1-0 kabla ya kwenda kupasuka tena nyumbani dhidi ya vibonde Mwadui waliowanyoa 2-1.

Nini kimeiangusha Gwambina? Mwanaspoti inakuletea mambo matatu ambayo yamemuangusha Badru na vijana wake, ikiwemo ukubwa wa michezo wamekumbana nayo mfululizo na makosa binafsi ya mchezaji mmoja mmoja kwenye kikosi hicho.


VIGOGO

Ratiba ya Gwambina kuanzia Aprili 16 hadi 24 kuna vigogo watatu ambao inahitaji nguvu ya ziada ili kupata pointi dhidi yao, wakiwemo Simba na Yanga.

Gwambina walianza kukaribishwa Dar na KMC, licha ya kwanza walianza vizuri dakika 45 za kipindi cha kwanza cha mchezo huo, walijikuta wakichemka kipindi cha pili na kukumbana na mvua ya mabao 3-0, Uwanja wa Uhuru.

Baada ya kukaribishwa kwa mabao hayo matatu na KMC ambao mchezo wa nyuma yao walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga, Gwambina wakawa na mlima mwingine mbele yao dhidi ya Wananchi mambo yakawa kama ambavyo mlishuhudia.

Bado shughuli haikumalizika, kwani walirejea nyumbani kwao, jijini Mwanza kukumbana na kipigo kingine cha bao 1-0 na Simba ambapo bao pekee liliwekwa kimiani na beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.


MAKOSA

Ndani ya michezo miwili iliyopita, Gwambina wameruhusu mabao sita huku wakifunga bao moja dhidi ya Yanga, aina ya mabao ambayo wamefungwa yametoka na makosa ya wachezaji mmoja mmoja kwenye kikosi chao.

Tukianza na mabao matatu ambayo walifungwa kwenye mchezo dhidi ya KMC, unaweza kubaini kwamba kulikuwa na makosa ya ukabaji, yapo ambayo yalifanywa na beki wao wa kushoto, Amosi Kadikilo ambaye hakukaa kwenye nafasi wakati wakishambuliwa.

Upande wa mchezo dhidi ya Yanga, Gwambina waliangushwa na makosa ya kipa wao, Ibrahim Isihaka bao ambalo alifungwa na Ditram Nchimbi hakuwa na hesabu nzuri wakati akiwa na golini na hata lile la Bakari Mwamnyeto ambalo alifunga kwa kichwa.

Kwenye mchezo wa Simba uzembe mdogo uliofanywa na mabeki wake katika kutoa pasi iliwapa nafasi wageni wao kuondoka na pointi tatu ugenini na kukamilisha mechi zao tatu za Kanda ya Ziwa ikivuna jumla ya alama 9 zilizowarejesha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu wakiing’oa Yanga.


UZOEFU

Huu ni msimu wa kwanza kwa Gwambina kushiriki Ligi Kuu Bara, wanahitaji muda ili kumudu presha ya michezo mikubwa licha ya kwamba walionyesha kiwango kizuri kama timu kwa kujaribu kumiliki mpira na kutengeneza nafasi.

Ni ngumu kwa timu ngeni moja kwa moja kuwa shindani hasa wanapokutana na vigogo wa soka la Tanzania, lakini Gwambina wamenyesha uthubutu, uzoefu wa timu kwenye ngazi ya ushindani ni kitu ambacho kimeiangusha timu hiyo licha ya kikosi chao kuwa na wachezaji wakongwe kama vile, Paul Nonga bado haikutosha.


MSIKIE

Baada ya kushindwa kuambulia pointi hata moja kwenye michezo miwili iliyopita dhidi ya KMC na Yanga , kocha wa Gwambina FC, Mohammed Badru aliyepanga kuvuna alama kwa Simba, lakini licha ya kuwabana watetezi hao, wakashtushwa na bao la shuti la mbali.

“Tumekuwa na michezo migumu mfululizo, ni kweli timu yetu ni changa lakini kuna kitu tumejaribu kukionyesha hasa kwenye mchezo uliopita, nadhani tunatakiwa kuendelea kuonyesha, siku zote unapocheza na timu kubwa unapofanya makosa huwa ni hatari,”

“Kosa moja linaweza kukuadhibu ndivyo ilivyokuwa dhidi ya Yanga na Simba. Hayo yamepita na michezo zetu ijayo tunajipanga kupambana ili kuhakikisha tunasahihisha makosa,” anasema.

Kupoteza kwa Gwambina michezo yao minne mfululizo kwenye Ligi kumewafanya kushuka kwenye msimamo wa Ligi na Coastal Union ya Tanga pamoja na Namungo kutoka nafasi ya 10 hadi ya 12 wakiendelea kusalia na pointi 30.