Prime
Gusa Achia, twende robo fainali CAF
Muktasari:
- Mechi za kesho kwa kila timu wawakilishi hao wa Tanzania ni muhimu kwani ndio itakayotoa dira ya kwenda robo na kama litatokea la kutokea, basi watasubiri hadi wikiendi ijayo kumalizia kazi zote zikiwa nyumbani, lakini uzito mkubwa ni michezo ya kesho kwani itafanya mechi za mwisho zisiwe na presha.
WIKIENDI ya Gusa Achia Twende Robo Fainali imefika. Simba na Yanga zina dakika 180 sawa na mechi mbili za kuamua hatma ya kufuzu robo fainali kwa mara nyingine tena katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, moja ikiusisha mechi za ugenini zinazopigwa kesho Jumapili.
Mechi za kesho kwa kila timu wawakilishi hao wa Tanzania ni muhimu kwani ndio itakayotoa dira ya kwenda robo na kama litatokea la kutokea, basi watasubiri hadi wikiendi ijayo kumalizia kazi zote zikiwa nyumbani, lakini uzito mkubwa ni michezo ya kesho kwani itafanya mechi za mwisho zisiwe na presha.
Simba inayoshiriki Kombe la Shirikisho ikiwa Kundi A, ipo jijini Luanda Angola kuikabili Bravos do Maquis ikihitaji angalau sare tu kufuzu robo fainali, wakati Yanga iliyopo pia Kundi A lakini katika Ligi ya Mabingwa, yenyewe ipo Mauritania kukabiliana na Al Hilal ya Sudan.
Mechi hizo zote zitachezwa kesho zikitofautiana muda tu, Simba ikianza mapema saa 1:00 usiku kisha baada ya mchezo huo wa Angola, itafuata zamu ya Yanga kumalizana na Al Hilal kuanzia saa 4:00 usiku, huku mashabiki wa klabu hizo wakiomba dua zinazofanana kuhakikisha kila timu inafanya kweli ugenini.
BRAVOS v SIMBA
Ni mechi ya mapema. Itapigwa pale nchini Angola kwenye Uwanja wa 11 de Novembro, Luanda. Wote wawili hapa wana nafasi ya kufuzu. Wanatofautiana pointi tatu tu, Simba iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa kundi hilo ina tisa, wakati wenyeji Bravos yenye alama sita ikiwa ya tatu na kila moja imecheze mechi nne.
Ushindi au sare tu, kwa Simba utaifanya ifuzu moja kwa moja robo fainali kutoka kundi hilo, kwani itafikisha kati ya pointi 10 ana 12, lakini kama itapata ugumu kwa Bravos, maana yake kila moja itafikisha pointi tisa na sasa kusubiri mechi za mwisho wiki ijayo kuamua nani aende robo.
Wakati huohuo, CS Costantine itakayocheza dhidi ya CS Sfaxien inazo pointi tisa huku wapinzani wao hawana kitu.
BRAVOS INAFUNGA, INAFUNGIKA
Wenyeji wa Simba licha ya kuwa na rekodi ya kutofungika kirahisi wakiwa nyumbani, lakini wanaruhusu mabao mengi kama wanavyofunga katika mechi zao za michuano hiyo ya CAF.
Hadi sasa imefunga mabao sita na kuruhusu tisa huku mechi zote nne hakuna iliyotoka uwanjani bila ya nyavu zao kutikiswa.
Mfumo wao wa kucheza kwa kupishana ndio unatoa nafasi kwa Simba endapo ikijipanga vizuri basi inaweza kufunga bao ambalo litawaweka sehemu nzuri ya kuondoka na pointi.
Mchezo wa kwanza waliokutana jijini Dar es Salaam, Bravos ilionekana kuwa ngumu eneo la kiungo ikiibana zaidi Simba ambayo ilishindwa kutegua mtego huo hadi ilipokuja kupata penalti na kufunga bao pekee kupitia Jean Charles Ahoua.
Licha ya kwamba Bravos inaonekana inafungika, lakini Simba inapaswa kuwa makini kwani Waangola hao mechi mbili za nyumbani imegawa dozi mfanano ya mabao 3-2 dhidi ya CS Constantine na CS Sfaxien hivyo inapokwenda kushambulia isisahau kujilinda.
Ni mechi mbili za nyumbani zote zikiwa za raundi ya awali ya michuano hiyo ndizo ilipocheza bila kuruhusu bao, ikiifunga Coastal Union kwa mabao 3-0 kisha FC Lupopo ya DR Congo kwa bao 1-0.
MBINU ZA FADLU
Kocha wa Simba, Fadlu Davids amemuacha Steven Mukwala ambaye ni mshambuliaji, kisha kuondoka na viungo 11 wakiwa ni nusu ya kikosi kizima kilichosafiri.
Uamuzi huo umetajwa ni sehemu ya mbinu zake za kwenda kushambulia zaidi kwa kuwatumia viungo kwani inaonekana timu hiyo inabebwa na eneo hilo kulinganisha na ushambuliaji.
Uimara wa Simba unaanzia kwenye ulinzi hadi kiungo ambapo wamekuwa wakifanya vizuri zaidi.
“Nimesafiri na viungo wengi sio kwa sababu ninakwenda kujilinda, lakini ni kutokana na utayari wao kuelekea mchezo husika dhidi ya Bravos,” alisema Fadlu.
Simba iliyofunga mabao matano na kuruhusu matatu, asilimia kubwa yametokea kwa viungo ambapo Jean Charles Ahoua amefunga mawili kama ilivyo kwa Kibu Denis wakati beki na nahodha wa kikosi hicho, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ akifunga moja.
Wakati Ahoua na Kibu wakifunga mabao, kipa Moussa Camara anafanya kazi kubwa kuzuia mipira isiingie langoni akiwa na clean sheet mbili katika mechi nne akiruhusu mabao matatu.
Simba inaisaka robo fainali ya sita katika misimu saba iliyopita kunako michuano ya CAF kuanzia 2018-2019 huku rekodi zikionyesha mara zote ilipocheza makundi, haijawahi kukwama njiani, imetoboa hadi robo fainali. Msimu huu itakuwaje?
WABURKINABE KULIAMUA
Jean Ouattara anayetekuwa kati akisaidiwa na Seydou Tiama atakayekuwa laini namba moja na Levy Sawadogo atakayekuwa mwamuzi msaidizi namba mbili, wakati mwamuzi wa akibna atakuwa ni Hamidou Diero.
Rekodi zinaonyesha mwamuzi Jean Ouattara ni mzoefu wa mechi za CAF akitumika zaidi kucheza mechi za timu za taifa zikiwamo za mtoano za Afcon, huku akitajwa sio mtu anayependa sana kutoa kadi uwanjani, lakini huwa ni mkali wachezaji wanapozingua.
AL HILAL VS YANGA
Jana Ijumaa MC Alger ilikuwa nyumbani kukabiliana na TP Mazembe katika mchezo wa lazima wenyeji kushinda, lakini hata wapinzani wao walihitaji ushindi.
Hiyo inatokana na timu hizo sambamba na Yanga kuwania nafasi moja ya kufuzu robo fainali kutoka Kundi A la michuano hiyo, baada ya Al Hilal kujimilikisha nafasi moja mapema ikiwa na pointi 10.
KIMAHESABU
Kabla ya mchezo huo, timu zote tatu hizo mojawapo inaweza kufuzu kutokana na pointi zilivyo. MC Alger (5), Yanga (4) na TP Mazembe (2). Matokeo ya ushindi kwa MC Alger ni faida kwao, lakini kichapo inakuwa faida kwa Yanga na TP Mazembe.
Wakati macho jana yakielekezwa kwa wawili hao waliokuwa wakisaka pointi za kibabe, kesho yatahamishiwa pale Mauritania Al Hilal ikiikaribisha Yanga.
HESABU ZA RAMOVIC
Yanga chini ya Kocha, Sead Ramovic, hesabu zao ni kuona inarudi Dar na pointi ikipendeza zaidi ziwe tatu ili kuweka hesabu zao sawa.
Kwa sasa timu hiyo inayoisaka rekodi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa pili, ina pointi nne huku Al Hilal iliyotangulia kufuzu inazo 10.
Utamu wa kundi hili utanoga zaidi baada ya kuchezwa mechi za wikiendi hii kwani endapo MC Alger imeshinda na Yanga ikashinda, zitauana zenyewe Januari 18 zitakapokutana Dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ramovic anafahamu ugumu uliopo katika mechi mbili zilizobaki ambapo anabainisha kuwa anachokifanya ni kutoangalia wapinzani wake wanafanya nini zaidi ya kuiandaa timu yake ya ushindi.
“Simuangalii mpinzani ili kuwa bora, napambana kuhakikisha najenga timu yenye ushindani, ninachokifurahia zaidi ni namna timu yangu inavyoimarika na ipo kwenye morali nzuri, hivyo naamini kila kitu kinawezekana kwa kushindana sisi wenyewe kwa kuboresha timu yetu.
“Tunakutana na mabingwa wa ligi kutoka mataifa tofauti na kuna timu ambazo zina uzoefu mkubwa, tumecheza na TP Mazembe ambayo imeshatwaa mataji ya michuano hii, sasa tunajiandaa kukutana na timu nyingine bora na kongwe kwenye michuano hii, hatutakiwi kuangalia nini wanafanya zaidi kujipanga ili tuwe washindani,” alisema Ramovic
MZIZE ABADILI UPEPO
Yanga katika kuisaka robo fainali, mshambuliaji wa timu hiyo, Clement Mzize ameonekana kubadili upepo pindi alipofunga mabao mawili waliposhinda 3-1 dhidi ya TP Mazembe tena wakitokea nyuma.
Ushindi huo ulikuwa muhimu sana kwa Yanga ukiwa ni wa kwanza kwao katika hatua hiyo msimu huu baada ya mechi mbili za kwanza kupokea vichapo kisha kuambulia sare ya 1-1 ugenini kwa Mazembe.
Wakati Yanga ikipoteza mechi mbili za kwanza, ilionekana bado inajitafuta chini ya Kocha Ramovic, lakini baadaye mambo yakaanza kukaa sawa na falsafa yao ya ‘Gusa Achia Twende Kwao’ ambayo imezitesa timu nyingi kuanzia michuano ya ndani sambamba na Mazembe.
Kufanya vizuri kwa Yanga katika mechi tano zilizopita za michuano tofauti ambazo imeshinda zote ikifunga mabao 19 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu, ni dhahiri imeimarika eneo la ushambuliaji na ulinzi.
Mbali na hilo, pia kurejea kwa Clatous Chama aliyekosekana katika mechi tano zilizopita sambamba na uwepo wa kipa Djigui Diarra ambaye alirejea dhidi ya TP Mazembe, inazidi kuimarisha kikosi cha Yanga ambacho kwa sasa kinashambulia sana bila ya kumpa mpinzani nafasi ya kujiuliza.
IBENGE HANA CHA KUPOTEZA
Kufuzu kwa Al Hilal mapema zikisalia mechi mbili, inamaanisha kwamba timu hiyo inayonolewa na Kocha Florent Ibenge haina cha kupoteza zaidi ya kulinda heshima na kusaka kumaliza kileleni mwa kundi lao.
Katika kundi hilo, Al Hilal ndio timu pekee isiyofungika kirahisi na ambayo haijapoteza mechi yoyote kama ilivyo MC Alger, kwani licha ya pointi 10 mkononi, lakini imefunga pia mabao sita na kuruhusu mawili kutinga nyavuni mwao.
Moto iliouwasha Al Hilal mechi tatu za kwanza ikishinda ugenini dhidi ya Yanga (0-2), kisha nyumbani mbele ya TP Mazembe (2-1) na ugenini kwa MC Alger (0-1), ilionyesha wazi kwamba ni timu ambayo ikipania kufanya jambo lake haishindwi.
Hata hivyo, baada ya kufuzu, Ibenge amechukua uamuzi wa kubadili kikosi kazi chake kilichomfikisha hapo na kusema atawapa nafasi wengine wakiwemo wale watokea benchi ili kutunza nguvu za robo fainali.
Licha ya uamuzi huo wa Ibenge, lakini isionekane ni kama nafuu kwa Yanga kwani katika mabao sita iliyofunga timu hiyo, nusu yametokana na watokea benchi. Yasir Mozamil aliyewafunga Yanga ana moja wakati Jean Girumugisha akifunga mawili dhidi ya TP Mazembe na MC Alger.
“Kwa sasa tunayo nafasi ya kupumzika kidogo na kujiandaa kwa hatua inayofuata. Hatuwezi kupuuza umakini, lakini ni muhimu pia kuhakikisha wachezaji wangu wanakuwa na nguvu za kutosha kwa changamoto kubwa zilizo mbele yetu,” alisema Ibenge na kuongeza:
“Mchezo dhidi ya Yanga utakuwa na umuhimu mkubwa kwao, lakini kwa upande wetu, tunahitaji kujiandaa kwa hali yoyote. Siwezi kujivunia mapema. Wachezaji wangu watahitaji kupumzika kidogo kabla ya michezo inayofuata.”
Katika hatua nyingine, Ibenge anaiona Yanga ikifuzu robo fainali baada ya kubainisha kwamba timu hiyo ina kikosi kizuri kinachoweza kufikia malengo hayo.
ANGALIZO
Yanga inapiga hesabu zake kwa kuifunga Al Hilal, kisha kuja kuimaliza MC Alger hapa nyumbani, lakini ikumbuke kwamba soka lina matokeo ya kushangaza. Katika kusaka ushindi, lazima ikumbuke kuna kulinda lango lao lisiruhusu bao.
Tatizo la Yanga katika mechi nne ilizocheza ni kuwa ya kwanza kuruhusu bao ingawa mechi mbili za mwisho zote dhidi ya TP Mazembe imefanikiwa kujibu mapigo.
Katika mechi za maamuzi, kukubali kuruhusu mpinzani akufunge kwanza inakupa presha ya kusawazisha na kusaka la ushindi kitu ambacho ukikutana na mpinzani mgumu imekula kwako.
WANYARWANDA WABEBA MSALA
Mechi hii itaamuliwa na waamuzi kutoka Rwanda ambapo mwamuzi wa kati ni Samuel Uwikunda, huku wasaidizi wakitarajiwa kuwa, Dieudonne Mutiyimana na Didier Ishimwe na mezani atakuwepo Rurisa Fidele.
Rekodi zinaonyesha Uwikunda katika mechi saba za kimataifa alizochezesha alitoa kadi za njano 23, ikiwa ni wastani wa kutoka kadi tatu kwa kila mchezo mmoja, lakini akiwa na bahati kwa timu mweyeji kupata matokeo mazuri, kwani katika mechi hizo ni mara moja tu mgeni ametokla na ushindi na ilikuwa ni Petro de Luanda iliyoitandika Etoile du Sahel kwa mabao 2-0 Desemba mwaka jana.
Mwamuzi huyo inakuwa mara ya pili kuzihukumu Yanga na Al Hilal kwani ndiye aliyeuamua mchezo wa raundi ya pili baina ya timu hizo Oktoba 08, 2022 na kumalizika kwa sare ya 1-1, kisha Yanga kwenda kupasuka ugenini 1-0 na kung’olewa Ligi ya Mabingwa na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika ilipofika fainali.