GEGO: Khalid Aucho? Mtu sana!
Muktasari:
- Ukitaja viungo bora wazawa katika Ligi Kuu Bara, hautawaacha wakali watatu kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mudathir Yahya na Khalid Habib Idd ‘Gego’.
ZANZIBAR imekuwa ni zao la wachezaji wengi wenye vipaji wakiwamo wa eneo la kiungo wanaonufaisha klabu za Tanzania Bara na visiwani.
Ukitaja viungo bora wazawa katika Ligi Kuu Bara, hautawaacha wakali watatu kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mudathir Yahya na Khalid Habib Idd ‘Gego’.
Gego ni kiungo fundi wa boli anayekipiga katika kikosi cha Singida Black Stars, ambaye licha ya kutotajwa sana midomoni mwa wadau wa soka, kazi ‘chafu’ anayoifanya, imeutingisha ufalme wa Kelvin Nashon kikosini SBS.
Kiungo bora huyo wa Ligi Kuu Zanzibar msimu uliopita akitwaa pia tuzo ya Mchezaji Bora wa ZPL, amefanya mahojiano na Mwanaspoti na kufunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumtaja Khalid Aucho kuwa ni kiungo wake bora kwa nyota wa kigeni.
AUCHO MTU SANA
Kanuni za Ligi Kuu Bara zinaruhusu kila timu kusajili hadi wachezaji 12 kutoka mataifa ya kigeni, jambo ambalo limechangia kuifanya ligi hiyo kuwa shindani na kushika nafasi ya 6 katika chati ya ligi bora za Afrika.
“Kabla sijatua Bara nimekutana na wachezaji wengi wa kigeni bora kwenye michuano ya Mapinduzi Cup, sasa nakipiga soka Ligi Kuu na naendelea kukutana na viungo wazuri. Kwangu hadi sasa Khalid Aucho ndiye mchezaji bora,” anasema na kuongeza;
“Aucho ni kiungo mzuri ana vitu vingi bora ambavyo kwa namna moja ama nyingine nimekuwa nikijifunza kutoka kwake. Ni mchezaji ambaye amekamilika, ana nguvu na anatumia akili awapo kiwanjani.”
Gego anasema licha ya wadau wengi kumtaja Aucho kwa kucheza rafu uwanjani, “mimi nafikiri sio sawa, kwani kutokana na utimamu wa mwili alionao mchezaji akimuingia kwa nguvu anaumia yeye, hiyo ndio imekuwa ikisababisha shida.”
Tangu Gego ametua ndani ya Singida Black Stars kwa upande wa Nashon ambaye alikuwa panga pangua kikosi cha kwanza umekuwa mtihani kwake kupata nafasi ya kucheza hadi kufikia wakati kutaka kutolewa kwa mkopo kabla ya dili lake kufeli.
FEI TOTO NI NEMBO
Ubora wa kiungo wa Azam FC, Fei Toto umekuwa kivutio kwa mastaa wa ndani na hata wale wanaokuja Tanzania kucheza soka la kulipwa. Haijaishia hapo tu bali hadi wachezaji kutoka Zanzibar alikozaliwa nyota huyo wamekuwa wakifunguka kuhusu ubora wake kama anavyothibitisha Gego.
“Kuna wachezaji wengi wazawa wanacheza nafasi ninayocheza mimi, lakini kwangu kioo changu ni Fei Toto. Ni mchezaji ambaye hakubali kushindwa, lakini pia haridhiki kutokana na kile anachokifanya siku hadi siku,” anasema Gego na kuongeza;
“Ubora wake na mafanikio anayoyapata Bara yamekuwa kivutio na kichocheo kwa wachezaji wanaoibuka na waliopo kuendelea kupambana ili kuweza kufikia alipo yeye sasa.”
KIUNGO TU UTAMPENDA
Mastaa wengi wamekuwa maarufu kutokana na nafasi ambazo wamekuwa wakicheza mara kwa mara huku wengine wakiwa maarufu kutokana na kutumika kwenye nafasi nyingi kiwanjani (kiraka). Kwa upande wa Gego amethibitisha kuwa yeye ni bora zaidi akipangwa eneo la kiungo.
“Sio kiraka lakini kutokana na kuchagua kazi ya soka kuwa ajira yangu kama kocha ataamua kunipanga nafasi tofauti na kiungo naweza kucheza kwa kufuata maelekezo lakini mimi ni bora zaidi na nafurahia kucheza nikiwa eneo la kiungo,” anasema na kuongeza;
“Kiungo naweza kucheza chini na juu na sasa nimekuwa nikitumika zaidi chini ndani ya Black Stars lakini nilipokuwa KMKM nilikuwa nikicheza juu namba nane na nilipata nafasi ya kufunga na nilikuwa natumia sana nafasi.”
Gego anasema anafurahi zaidi kucheza eneo la kiungo bila hata ya kupewa maelekezo hivyo ili kocha aweze kumuelewa na kumpa nafasi kila wakati ampange eneo hilo.
SIMU MOJA YAMLETA BARA
Mastaa wengi wa Kizanzibar wanaocheza Ligi Kuu Bara wameibuliwa kupitia michuano ya Mapinduzi Cup kama ambavyo anathibitisha Gego ambaye amejiunga na Singida Black Stars katika dirisha kubwa la kuingia msimu huu.
“Baada ya michuano ya Mapinduzi kutamatika nilipokea simu moja kutoka kwa kiongozi ambaye sitaweka wazi jina lake akaniambia kuhusiana na kunihitaji ili nije kucheza katika timu yake nikamwambia mimi bado nina mkataba anatakiwa azungumze na viongozi wa KMKM,” anasema na kuongeza;
“Nilikuwa na mkataba wa mwaka mmoja nilipomwambia hivyo alirudi kwa viongozi wangu na kumalizana nao na mimi ndipo nilipokaa nao mezani kwa lengo la kumalizana nao na sasa naitumikia Singida Black Stars.”
Gego anasema matamanio makubwa kwake yalikuwa ni kuja kucheza Ligi Kuu Bara ambapo pia ni njia yake ya kutoka kwenda kusaka mafanikio zaidi nje ya Tanzania.
AITAJA YANGA, JKT TANZANIA
Ligi Kuu Bara imesimama kwa miezi miwili kupisha michuano ya Mapinduzi sambamba na michuano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024 inayoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda. Kiungo wa Singida Black Stars anataja mechi mbili bora mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
“Katika mechi 16 tulizocheza hadi sasa kwenye ligi mechi dhidi ya Yanga ambayo tulicheza kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar nikitumika kwa dakika 80 ndio ilikuwa bora kwangu,” anasema Gego na kuongeza;
“Ukiondoa kupoteza kwa bao 1-0 mchezo huo ulikuwa bora sana upande wetu lakini matokeo hayakuwa upande wetu lakini pia ukiondoa mchezo huo pia JKT Tanzania imeingia kwenye historia yangu.”
Gego anasema mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania ambao uliisha kwa sare ya bao 1-1 ulikuwa bora pia kwani timu zote zilicheza kwa kukamiana na kila mmoja alikuwa anahitaji pointi tatu, lakini dakika 90 ziliamua sare.
BARA UBORA, ZENJI VIPAJI
Wakati Ligi Kuu Bara ikitajwa kuwa namba sita kwa ubora Gego amekiri hilo huku akiweka wazi sababu kuwa ni kutokana na kuwakutanisha wachezaji kutoka mataifa mbalimbali tofauti na Zanzibar.
“Kuna utofauti mkubwa wa Ligi Kuu Bara na ligi ya Zanzibar kuanzia uwekezaji na namna timu zilivyo na mchanganyiko wa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali tofauti na Zanzibar,” anasema na kuongeza;
“Lakini pia Bara ligi yao ni ngumu sana ina ushindani mkubwa tofauti na Zanzibar ambayo uwekezaji wao ni mdogo.”
NNE, TISA FRESHI TU
“Navaa jezi namba 4 kwasababu ndio namba niliyopewa baada ya kukuta haina mtu ndani ya Singida Black Stars pia kwenye maisha yangu ya mpira siamini katika kuvaa jezi namba ndio ubora, mimi navaa namba yoyote,” anasema na kuongeza;
“Hata namba moja ingekuwa inavaliwa na wachezaji wa ndani ningevaa pia nyingine zote naweza kuvaa hadi tisa ambayo inatajwa kuwa ina mkosi mimi naweza kuivaa kikubwa nipate nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.”