Fursa ya kihistoria Serengeti Boys Afcon 2025

Muktasari:
- Kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye kundi lake A lenye timu za Morocco, Uganda na Zambia kutaihakikishia moja kwa moja Serengeti Boys kufuzu fainali za Kombe la Dunia chini ya miaka 17 zitakazofanyika Qatar.
BAADA ya makundi ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (Afcon U17) na zile za chini ya umri wa miaka 20 (Afcon U20) 2025 kupangwa juzi, timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ina nafasi nzuri ya kufuzu Kombe la Dunia, baadaye mwaka huu.
Kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye kundi lake A lenye timu za Morocco, Uganda na Zambia kutaihakikishia moja kwa moja Serengeti Boys kufuzu fainali za Kombe la Dunia chini ya miaka 17 zitakazofanyika Qatar.
Na hilo likishindikana, bado Serengeti Boys itafuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia ikiwa itamaliza katika nafasi ya tatu ikiwa na matokeo mazuri zaidi kulinganisha na timu zitakazoshika nafasi ya tatu kwenye makundi mengine.
Hiyo ni kufuatia uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) wa kuongeza idadi ya timu shiriki kwenye mashindano hayo jambo lililofanya Afrika kuongezewa idadi ya wawakilishi ambapo sasa itakuwa na timu 10.
Kati ya timu hizo 10, nane ni zile ambazo zitatinga robo fainali na mbili ni zitakazomaliza katika nafasi ya tatu zikiwa na matokeo mazuri (best losers).
Fainali hizo za Afcon U17 zitafanyika Morocco kuanzia Machi 30 hadi Aprili 19 mwaka huu zikishirikisha nchi 16.

UGUMU UKO HAPA
Kazi kubwa inapaswa kufanywa na Serengeti Boys katika kundi hilo kutokana na wasifu wa wapinzani ambao itakabiliana nao kwa maana ya Morocco, Uganda na Zambia.
Morocco U17 inayonolewa na kocha Nabil Baha inabebwa na uenyeji wa mashindano hayo lakini ina historia na mafanikio makubwa kulinganisha na Serengeti Boys.
Katika fainali zilizopita ilifika hatua ya fainali na mwaka 2013 ilishika nafasi ya nne.
Imewahi kucheza hatua ya robo fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo mwaka 2023.
Uganda U17 imekuwa na historia nzuri ya ubabe dhidi ya Serengeti Boys katika mechi za mashindano tofauti ambayo timu hizo zimewahi kukutana.

Mfano ni mechi tano zilizopita baina yao ambazo Uganda U17 imepata ushindi mara tatu, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.
Hii ni mara ya pili kwa Uganda kushiriki Afcon U17 ambapo ya kwanza ilikuwa 2019 ilipoishia hatua ya makundi.
Zambia sio timu tishio sana kwenye fainali za Afcon na imeshiriki mara mbili zote imeishia hatua ya makundi.

KAKA ZAO KAZI IPO
Timu nne zitakazotinga hatua ya nusu fainali ya Afcon U20 ambazo mwaka 2025 zitafuzu fainali za Kombe la Dunia ambazo zitafanyika huko Chile baadaye mwaka huu.
Katika Afcon U20 ambazo zitafanyika Ivory Coast kuanzia Aprili 26 hadi Mei 18 mwaka huu, timu ya Taifa ya Tanzania ‘Ngorongoro Heroes’ imepangwa katika kundi A na wenyeji, DR Congo. Ghana na timu moja kutoka kanda ya soka ya Afrika ya Kati (Unifac)
Wenyeji Ivory Coast sio wanyonge kwani wameshiriki fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo mara nne tofauti na moja wakiishia hatua ya 16 bora. Ghana ni tishio zaidi katika mashindano hayo kwani imekuwa ikitamba ndani na nje ya Afrika.
Kombe la Dunia la vijana wa umri huo, Ghana imetwaa mara moja, imemaliza katika nafasi ya tatu mara moja na nafasi ya nne mara moja.

KOMBE LA DUNIA MTIHANI
Ili itinge Kombe la Dunia, Ngorongoro Heroes inatakiwa kuhakikisha inafuzu robo fainali ya Afcon U20 ili iwe miongoni mwa timu nne zitakazoenda Chile.
Hapana shaka kibarua kikubwa kwa Ngorongoro Heroes kitakuwa ni kusogea hadi nafasi za juu badala ya kuishia makundi kama ilivyofanya katika fainali za Afcon U20 2021.

KARIA NA AHADI YA KIBABE
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ametamba kuwa anaamini timu zote hizo zitatinga Kombe la Dunia mwaka huu.
“Tumejidhatiti vizuri na timu zetu zinaonyesha muelekeo mzuri hivyo zinatupa matumaini kwamba zitafanya vizuri katika hayo mashindano hayo.
“Sisi kama TFF tunaishukuru serikali chini ya Rais Dk. Samiah Suluhu Hassan kwa sapoti kubwa ambayo imesaidia kuongeza hamasa kwa wachezaji na kuchangia timu zetu kufanya vizuri,” alisema Karia.