Funika mdomo, siri ya wachezaji wakiteta uwanjani
Muktasari:
- Hata hivyo, je umewahi kujiuliza; Kwa nini wachezaji au makocha hufunika midomo wanapoongea uwanjani?
HUENDA umekuwa ukiona jambo hili, lakini hukuwahi kufikia linafanyika kwa sababu zipi. Ndiyo, ni mara nyingi imekuwa ikionekana wachezaji au makocha pale wanapokuwa wakizungumza uwanjani hupenda kufika midomo.
Hata hivyo, je umewahi kujiuliza; Kwa nini wachezaji au makocha hufunika midomo wanapoongea uwanjani?
Mwanaspoti linakudadavulia sababu zinazochangia jambo hilo, kwani ni mbinu zinazofanywa kwa makusudi kulingana na soka la kisasa na kuna baadhi ya mastaa wanaopenda kufanya jambo hilo.
SABABU MAALUMU
Wachezaji hufunika midomo yai wanapozungumza uwanjani kwa sababu kadhaa muhimu ikiwamo;
Kuepuka kusomwa midomo (lip-reading)
Kamera za TV, wapinzani au wachambuzi wanaweza kusoma midomo na kugundua mbinu au ujumbe wa siri.
Kamera za kisasa zina ubora mkubwa. Maagizo yanaweza kusomwa na wapinzani au wachambuzi wa TV. Hivyo kujiweka salama wachezaji na makocha wanalifanya hivyo kimbinu na wengine hufundishana kabisa kambini sio bahati mbaya.
KUFICHA MIKAKATI NA MBINU
Wachezaji na makocha hujadili mbinu, nafasi au mabadiliko ya mchezo, hayo yakisikika au kuonekana yanaweza kumpa mpinzani faida.
Mazungumzo mengi yanahusu mipango ya kona, friikikii au mabadiliko ya mfumo wa uchezajina hivyo kuepuka kuvujisha siri, wenyewe huamua kuziba midomo kuwa salama.
Wakati mwingine wanazungumza mambo binafsi au wanakosoana na hawataki dunia nzima ijue. Pia hata kusema neno la ovyo na kunaswa ni rahisi na kuwa kituko duniani.
Maneno makali, matusi au malalamiko kwa refa yakionekana wazi yanaweza kuleta kadi au adhabu.
Ni dhahiri matusi au maneno makali yakisomwa midomo yanaweza kuleta faini au kusimamishwa.
Kwa wachezaji wa ngazi ya juu, hili limekuwa tabia ya kawaida, hufundishwa mapema kuwa waangalifu na mawasiliano yao.
HUTUMIKA ZAIDI WAPI?
Wachezaji wengi hutumia mbinu hii ya kuziba mdomo wakiwasiliana katika maeneo yafuatayo;
Mpira wa adhabu au kona; kabla ya kona au friikikii, wachezaji husema: Wewe kata ya kwanza, mimi nitaenda nyuma na kadhalika. Wakisema wazi, wapinzani watajipanga mapema na kukwama kutimiza malengo yao uwanjani.
Kiongozi wa timu (nahodha) mara nyingi humwambia mwenzake au refa kitu nyeti (kama onyo au mkakati wa muda mfupi). Hivyo huchukua tahadhari mapema kwa kuziba mdomo, ili kujiweka salama na timu kwa ujumla uwanjani.
UJANJA KWA WAJANJA
Kufunika mdomo husaidia kuepuka maneno yao kuwa gumzo mitandaoni, hasa kwa dunia ya sasa ambayo kila mtu ni mwanahabari. Enzi za kamera kila kona. Siku hizi kuna kamera karibu kila sehemu ya uwanja. Wachezaji wanajua lolote wakisema linaweza kuwa klipu TikTok dakika chache baadaye.
Maneno ya ‘kisaikolojia’ kwa mpinzani; wakati mwingine wanamwambia mpinzani kitu cha kumvuruga kisaikolojia, hawataki kisikike au kionekane wazi.
Mawasiliano ya haraka katikati ya kelele; uwanja una kelele nyingi; kufunika mdomo na kuongea karibu husaidia ujumbe ufike kwa usahihi. Kwa hiyo si ujanja wa kuigiza ni sehemu ya mchezo wa kisasa kabisa.
Kwa nini imekuwa muhimu zaidi?
Teknolojia ya HD & slow-motion; midomo inasomeka kirahisi. Mitandao ya kijamii; clip ndogo huenea kwa kasi ajabu.
Timu zina wachambuzi wa lip-reading (hasa kwenye mechi kubwa).
Pia kuna ukweli unaochekesha kwani katika baadhi ya klabu kubwa, wachezaji hufundishwa ‘usizungumze chochote nyeti bila kufunika mdomo wako’.
Kwa hiyo ukiona wachezaji wanaonekana kama wanafanya siri nzito, mara nyingi ni mpango na mikakati ya timu.
MASTAA WANAOJULIKANA
Kuna mastaa wanaojulikana kwa kufunika midomo na hawa ni pamoja na Lionel Messi. Mara nyingi mwamba huyo huzungumza na wachezaji wenzake au refa, huku akifunika mdomo; ni mtulivu lakini makini sana na maneno yake.
Cristiano Ronaldo; mkali huyo hufunika sana mdogo, hasa anapotoa maelekezo au kumkemea mwenzake, hufunika mdomo kuzuia kamera ‘kumsoma’.
Sergio Ramos; mtaalamu wa mbinu za ulinzi; huongea sana uwanjani na karibu kila mara hulinda midomo. Kumbuka huyo jamaa alikuwa msela sana.
Kevin De Bruyne; kiungo huyo mahiri naye ni kati ya wanaopenda kufunika mdogo, hasa akipanga mashambulizi au mipira ya adhabu, anahakikisha wapinzani hawajui mpango.
WANAOKIUKA SASA
Yapo matukio yaliyowahi ‘kuvuja’ baada ya mchezaji alisahau kufunika mdomo, kamera zikamsoma, na maneno yake yakawa gumzo (hasa ligi za Ulaya).
Wakati mwingine mashabiki hugundua malalamiko kwa refa au matusi kwa mpinzani, jambo linalozua mijadala mitandaoni.
CHUKUA HII
Wachezaji wakifunika midomo sio wanaficha siri ya maisha, ni wanaogopa kamera zisimnase na kusikika kwa mbinu zao kabla mpira haujapigwa. Pia uwanjani hakuna siri, kuna kamera ndiyo maana midomo inafunikwa kama Wi-Fi ya mpinzani.
WASIKIE WACHEZAJI
Mshambuliaji wa Namungo, Mkongomani Fabrice Ngoy, alisema kuziba mdomo wakati wa mazungumzo ndani ya uwanja maana yake ni kutaka kulinda faragha kati ya watu wawili tu, kutokana na maelekezo yanayotolewa.
“Kwangu ishawahi kunitokea mwamuzi alizungumza na mimi, katika mazungumzo hayo nilishuhudia akitumia lugha nzuri tu ya kunionya kwa kuziba mdomo, ila nilichogundua hakutaka mchezaji mwingine uwanjani asikie alichokuwa ananiambia kwa wakati ule,” alisema Ngoy.
Ngoy alisema uamuzi wa waamuzi kutumia aina hiyo ya mawasiliano ni nzuri kwa sababu inalinda haki ya mchezaji mmoja na mwingine uwanjani, kwani maadili ni tofauti, hivyo anaposikia ulichoambiwa kama ni kibaya kinaweza kuleta taswira mbaya.
Nahodha wa Coastal Union, Aidan Bakari, naye ametolea mfano huo wa kuzungumza na mwamuzi akisema: “Kwanza unajua unapoenda kuongea na mwamuzi lazima kamera ikufuate, kwa hiyo huwa tunaficha maongezi tunayoongea na refa ndiyo maana tunaweka mkono mdomoni.”
Mbali na nyota hao, baadhi yao wamesema hata wanapokuwa wanajadili mbinu zao pindi mwamuzi amesimamisha mchezo, anayezungumza huwa analazimika kuziba mdomo kwani huenda kuna mpinzani mtaalamu wa kufahamu nini unazungumza kwa kuangalia mdomo tu hata bila ya kusikia sauti.