Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Folz, Fadlu wana kazi kubwa kimataifa

NONDO Pict


LIGI Kuu Bara msimu wa 2025-2026 imefunguliwa rasmi kwa kuanza kupigwa mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya bingwa mtetezi, Yanga SC dhidi ya mshindi wa pili, Simba SC. Hiyo ilikuwa ni Dabi ya Kariakoo.


Baada ya matamasha ya kutambulisha vikosi kwa timu zote mbili, zimepata mchezo wa ushindani ambao pia umetumika kama mchezo wa kujiandaa na mechi za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa lkesho Ijumaa na keshokutwa Jumamosi.


Tukirudi katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, kimbinu na ufundi ilikuwa nzuri na mwishowe watazamaji walipata burudani ya kutosha, lakini makocha wa timu hizo, Romain Folz wa Yanga na Fadlu Davids wa Simba, wana kazi kubwa ya kufanya katika michezo yao ya kimataifa, hiyo ni kutokana na kile nilichokiona kwenye mchezo wao wa Ngao ya Jamii.

Ukiangalia katika mchezo huo, Simba iliingia na muundo wa 1-4-4-2, uliokuwa unabadilika kulingana na mnyumbuliko wa timu na kadiri mpira unapohama eneo moja kwenda lingine. Wanapokuwa na mpira, mfano wakianza kwa Moussa Camara, umbo linakuwa 1-2-4-2-2.

NOND 01

Camara mbele yake kukiwa na Abdulrazack Hamza na Rushine De Reuck, baadae aliingia Chamou Karaboue nafasi ya Hamza, hawa ndio wachezaji wa Simba waliogusa mara nyingi mpira kwa sababu ndio waliokuwa na jukumu la kuanza ujenzi wa shambulizi lakini pia Yanga ilikuwa ikikabia kwenye eneo la katikati mwa uwanja, hivyo kuwaacha huru.

Faida ya muundo wao iliwapa idadi kubwa eneo la kiungo na kuwafanya viungo wao wa kushambulia kuwa karibu na washambuliaji, pia uliwalazimisha walinzi wa pembeni wa Yanga kupambana na washambuliaji wawili, Kibu Denis na Steven Mukwala, hata alipoingia Seleman Mwalimu ambao wakati timu ina mpira, Simba ilikuwa ikifungua pembeni kitu kilichosumbua safu ya ulinzi ya Yanga na walinzi wa kati wakajikuta wana machaguo mawili, kuwafuata pembeni au kubaki kati kuzuia eneo.

NOND 02

Pia ikawaondolea ushirikiano kwa sababu Dickson Job na Ibrahim Bacca walilazimishwa kukaa mbalimbali, hivyo kufanya mapambano mengi ni ya kujitegemea kitu kilichoifanya Simba kutengeneza hatari nyingi kwani mabeki hao walipoondoka katikati, viungo washambuliaji wa Simba waliingia kwenye maeneo yaliyoachwa, hili utaliona hata wakati Neo Maema anakosa nafasi alikuwa peke yake, hakuna aliyemkaba.

Kwenye kuzuia, umbo la Simba liliwasaidia kunyumbulika katika muundo wa 1-4-5-1 kuanzia katikati ya uwanja uliowapa Yanga ugumu. Eneo pekee waliloshindwa kuwazuia Yanga ni kwenye kubadilika kutoka kuwa na mpira na wanapopoteza ndipo walikuwa na nafasi ya kuadhibiwa kama sio ubinafsi wa baadhi ya wachezaji wa Yanga au kukosa umakini, hapo wanapaswa kupafanyia kazi katika michuano ya kimataifa na eneo la kutumia nafasi wanazotengeneza.

NOND 03

Kwa Yanga, kama timu ya kwanza kwenye mchezo huo ilitumia muundo wake uliozoeleka wa 1-4-2-3-1. Kutokana na ugeni wa Kocha Romain Folz, aliwaheshimu wapinzani ambao nao walimheshimu, hivyo kukawa hakuna timu inayomlazimisha mwenzake kufanya makosa, muundo wao uliwasaidia walipokuwa na umiliki wa mpira, lakini ni muundo unaotegemea zaidi watu wa pembeni kushambulia kitu ambacho walikikosa, hakukuwa na ufanisi na ubunifu eneo hilo hasa wakiwa na umiliki wa mpira.

Unaweza kusifia namna nzuri ya Simba kujilinda, lakini huwezi kuacha kuzungumzia ubunifu eneo hilo ambalo ndilo hatari zaidi kwa wapinzani wanaokabiliana na Yanga ukiachilia mbali jitihada zilizofanywa na viungo.

Yanga iliwakosa kiwanjani washambuliaji wake wa pembeni, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua wakiwa kwenye ubora wao kwani wawili hao huwa ni kazi sana kukabiliana nao. Licha ya kwamba ndio wamehusika na bao hilo moja kwa moja, lakini hakuna matukio mengine yaliyowakilisha kile wanachoweza kufanya hata alipotangazwa Pacome kama mchezaji bora wa mechi, nilipata mshtuko kuona kazi yote iliyofanywa na Djigui Diara kuibakisha timu mchezoni imefutwa na tukio moja tu la bao?

Yanga kiuchezaji inaonekana ni timu inayowaheshimu wapinzani kuanzia dhidi ya Bandari, unaweza kumuona kocha ana tahadhari nyingi.

NOND 04

Katika michuano ya kimataifa, wanatakiwa kufanyia kazi wanaowajibika timu inapokuwa inajilinda kwani mbali na kuzuia kuanzia katikati, bado walikuwa wanafunguliwa kirahisi hasa mstari wao wa kwanza wa ulinzi na kuboresha utengenezaji wa nafasi kwa mashambulizi wanayofanya hasa kwenye mashambulizi ya kujibu yanayoonekana kocha ndiko anapotengeza hatari nyingi kwenye mchezo.

Leo Ijumaa, Yanga itashuka dimbani kule Angola kucheza dhidi ya Wiliete. Wanayanga wanataka kuiona timu yao ikicheza tena hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyokuwa msimu uliopita, lakini kubwa zaidi ni kuvuka hatua hiyo, kazi inabaki kwa benchi la ufundi kufanikisha hilo na mchezo wa Dabi ya Kariakoo utakuwa umewapa kipimo sahihi cha kimataifa.

Simba yenyewe itacheza kesho Jumamosi ikiwa ugenini dhidi ya Gaborone United ya Botswana. Msimu uliopita, timu hiyo ikiwa chini ya Kocha Fadlu ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, safari hii katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kuna matarajio makubwa waliyonayo Wanasimba juu ya timu yao.

Kila la kheri kwenu Simba na Yanga, pia bila ya kusahau Azam na Singida Black Stars zitakazoshuka pia dimbani wikiendi hii katika michezo ya ugenini ya Kombe la Shirikisho Afrika.