Prime
Feisal, Simba kuna nini?

Muktasari:
- Nyota huyo wa zamani wa JKU ya Zanzibar na kupita kwa muda mfupi Singida United kabla ya kutua Yanga msimu wa 2018-2019 akiwa na kiungo mkabaji kabla ya kusogezwa eneo la mbele na kucheza kama kiungo mshambuliaji na kuwafunika washambuliaji tishio.
ACHANA na stori zinazoendelea juu ya kuhusishwa na klabu za Simba na Yanga, kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amethibitisha kuwa yeye sio mchezaji wa mchezo mchezo kutokana na namba alizoziandika ndani ya misimu mitano mfululizo.
Nyota huyo wa zamani wa JKU ya Zanzibar na kupita kwa muda mfupi Singida United kabla ya kutua Yanga msimu wa 2018-2019 akiwa na kiungo mkabaji kabla ya kusogezwa eneo la mbele na kucheza kama kiungo mshambuliaji na kuwafunika washambuliaji tishio.
Ndio, namba huwa hazidanganyi na kwa Fei Toto tangu acheze katika eneo ushambuliaji ametupia sana mabao kiasi cha kuwakimbiza hadi washambuliaji asilia hasa wachezaji wazawa, kwani katika misimu hiyo mitano yeye ndiye kinara wa kufunga mabao mengi.
Fei Toto aliitumikia Yanga kwa misimu mitano kuanzia 2018-2019 hadi 2022-2023 kabla ya kuhamia Azam msimu uliopita na kumaliza kama mfungaji namba mbili za Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 19 nyuma ya Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyemaliza na 21.
Kiungo mshambuliaji huyo kutoka visiwani Zanzibar anayeongoza kwa sasa kwa kuasisti mara nyingi (13) namba zimembeba kwa kucheka na nyavu katika Ligi Kuu kwa misimu mitano kuanzia 2020-2021 hadi huu wa 2024-2025 uliopo ukingoni kwa sasa.
Katika misimu hiyo mitano, Fei Toto amekuwa kinara kwa wachezaji wazawa kwa kufunga mabao mengi (40), akiwazidi hadi John Bocco aliyepo JKT Tanzania, Clement Mzize aliyepo Yanga na Reliants Lusajo aliyepo Dodoma Jiji.
Hapa chini ni orodha wachezaji wazawa wanaotengeneza 10 Bora ya kufunga mabao mengi katika misimu hiyo mitano, huku Fei Toto akiwa ndiye kinara, lakini kitu cha ajabu, Simba haipo katika orodha ya timu zilizotunguliwa na kiungo huyo anayetajwa kunyemelewa na timu pamoja na Yanga..

1) FEISAL SALUM-40
Kiungo mshambuliaji huyo anayemudu kucheza nafasi zote za kiungo kuanzia ile ya ukabaji, ushambuliaji na mshambuliaji wa pili hadi unaposoma makala haya, ndiye anaongoza orodha ya wachezaji wazawa waliofunga mabao mengi katika Ligi Kuu.
Katika misimu mitano mfululizo mitatu akiwa na Yanga na miwili akiwa na Azam amefunga jumla ya mabao 40 ikiwa ni saba zaidi na aliyofunga John Bocco anayeshika nafasi ya pili katika orodha hiyo akiwa na 33 aliyofunga akiwa na Simba na JKT Tanzania.
Katika misimu mitatu akiwa na Yanga, kuanzia 2020-2021, 2021-2022 na 2022-2023, Fei Toto aliifungia timu hiyo ya mabao 17, huku mengine 23 akiifunga akiwa na Azam yakiwamo manne ya msimu huu na 19 ya msimu uliopita alipochuana na Aziz KI.
Kitu cha ajabu ni kwamba katika timu zote zilizotunguliwa na Fei Toto, Simba haipo kabisa katika orodha hiyo kama ilivyo kwa Mashujaa, Fountain Gate, Pamba Jiji, kwa timu zilizopo ndani ya Ligi ya msimu huu.
Kingine ni kwamba kinachovutia zaidi ni kwamba katika mabao yote 40 aliyofunga Fei Toto yalipatikana au kuisaidia timu alizozitumikia kuibuka na ushindi kwa misimu hiyo mitano, huku klabu aliyoionea sana ikiwa ni Ihefu (sasa Singida Black Stars) akiitungua mabao sita hadi sasa.
Ameitungua mara tatu ikiwa kama Ihefu, enzi akiitumikia Yanga, kisha akafanya hivyo msimu ujao kwa kuifunga mabao mawili akiichezea Azam na msimu huu timu hiyo ilipobadilishwa jina na kuwa Singida BS ameifunga mara moja katika ushindi wa 2-1.
Kagera Sugar inafuata katika orodha ya zilizoonewa na Fei Toto kwa kufungwa mabao matano, ikiwamo moja alipokuwa na Yanga na manne akiitumia Azam, likiwamo la msimu huu walipoicharaza bao 1-0 kwa mkwaju wa penalti wa nyota huyo.
Ruvu Shooting ni timu ya tatu kufungwa mabao mengi na Fei Toto, ikipigwa manne, yote akifunga wakati akiitumikia Yanga, kwani ilishuka daraja kabla hajatua Azam FC.
Tabora United ni kati ya timu tano zilizofungwa mabao matatu kila na Fei Toto, ikiwamo KMC, Tanzania Prisons, Coastal Union na Dodoma Jiji, huku Azam na Mtibwa Sugar zenyewe kila moja zikiruhusu mawili. Aliiitungua Azam katika sare ya mabao 2-2 wakati akiitumikia Yanga msimu wa 2022-2023 kabla ya kusajiliwa na matajiri hao.
Timu nyingine zilizoonjwa na kiungo huyo ambaye katika mabao hayo 40, zipo penalti nne tu kati ya sita alizopiga, akipoteza mbili zote akiitumikia Azam ni pamoja na Yanga aliyoifunga msimu uliopita katika ushindi wa mabao 2-1.
Pia zimo Geita Gold iliyoshuka daraja msimu uliopita, Namungo, JKT Tanzania, KenGold na Polisi Tanzania iliyoshuka daraja sambamba na Ruvu Shooting msimu miwili iliyopita.

2) JOHN BOCCO-33
Nahodha huu wa zamani wa Azam FC na Simba ndiye anayefuata nyuma ya Fei Toto akiwa na mabao 33 aliyoyafunga akiwa na uzi wa Wekundu wa Msimbazi (31) na mawili akikitumikia kikosi cha maafande wa JKT Tanzania msimu huu.
Bocco anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji wa muda wote wa Ligi Kuu Bara kwa sasa akiwa na mabao 156 kupitia misimu 17 mfululizo akiipiku rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyekuwa na mabao 153 kupitia misimu 13 mfululizo.
Nyota huyo mkongwe anayemiliki mabao mawili kwa msimu huu hadi sasa, ni mmoja ya wazawa wawili waliowahi kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora katika misimu hiyo mitano akiwamo na George Mpole ambaye naye yumo katika orodha hii ya 10 Bora ya wazawa.
Bocco alitwaa tuzo ya Mfungaji Bora msimu wa 2020-2021 akifunga mabao 16 kabla ya Mpole kuja kumpokea msimu uliofuata wa 2021-2022 akikwamisha wavuni mabao 17 akimpiku Fiston Mayele aliyekuwa Yanga kabla ya kutimkia Pyramids ya Misri.
Baada ya msimu huo alitwaa kiatu cha dhahabu akimpiku mshambuliaji wenzie waliokuwa wakicheza pamoja Simba, Bocco alifunga msimu uliofuata mabao matatu, kisha kuongeza mengine 1o na msimu uliopita akimalizana na Simba alitupia mawili kbla ya msimu huu akiwa na JKT Tanzania akifunga pia mawili na kufikisha mabao 33.

3) RELIANTS LUSAJO-32
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Toto Africans, Yanga, Namungo na Mashujaa kwa sasa anakipiga Dodoma Jiji, ndiye anayeshika nafasi ya tatu ya wachezaji wa kizawa wenye mabao mengi ndani ya misimu mitano akiwa na mabao 32.
Mabao hayo ameyafunga kupitia timu za KMC, Namungo na Mashujaa, huku kwa sasa akiwa na Dodoma Jiji bado hajatupia bao lolote, japo bado ana michezo mitano ili kuhitimisha msimu na kikosi hicho kinachonolewa na kocha Mecky Maxime.
Lusajo alianza kufunga mabao sita akiwa na KMC/Namungo msimu wa 2020-2021, huku misimu miwili mfululizo akiwa na Namungo alifunga mabao 18, akianza na 10 kisha kuongeza manane na msimu uliopita alifunga manane akiwa na Namungo/Mashujaa kabla ya msimu huu kutua Dodoma Jiji ambako ameasisti mabao mawili hadi sasa.

4) IDD SELEMAN ‘NADO’-28
Winga huyu wa zamani wa Mbeya City anayekipiga Azam FC kwa sasa, Idd Seleman ‘Nado’ ndiye anayeshika nafasi ya nne katika misimu mitano kwa kufunga mabao mengi akiwa na 28.
Tofauti na wachezaji waliomtangulia, Idd Nado amefunga mabao hayo yote akiwa na timu moja tu, yaani Azam, huku akiwa mmoja ya wachezaji waliyehusika na mabao mengi ya timu hiyo katika misimu hiyo mitano. Pia ni mmoja ya nyota walioisaidi Azam kumaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita na kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili baada ya ile ya 2015 ilipotwaa ubingwa wa Bara 2013-2014.

5) SEIF RASHID KARIHE-25
Mshambuliaji huyo kutoka visiwani Zanzibar ndiye anayeshika nafasi ya tano akilingana na Jeremiah Juma wa Tanzania Prisons kila mmoja akifunga mabao 25.
Karihe amefunga mabao hayo ndani ya misimu mitano akiwa na timu tatu tofauti, 15 akifunga katika misimu mitatu akiwa na Dodoma Jiji kabla ya msimu uliopita akiitumikia Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja akitupia mabao saba.
Msimu huu nyota huyo wa zamani wa Polisi Tanzania na Azam, anakipiga Mashujaa na hadi sasa wakati Ligi Kuu ikisaliwa na mechi za raundi tano amefunga mabao matatu.

5) JEREMIAH JUMA-25
Mshambuliaji huyo anayefahamika kwa jina la JJ akitumia zaidi jezi namba 10 akiwa na yupo katika orodha hii ya wazawa wenye mabao mengi akiwa na 25 sawa na aliyonayo Karihe, japo Jeremiah mabao yote ameyafunga akiwa na Tanzania Prisons.
Jeremiah ambaye aliondolewa katika kikosi cha timu hiyo kwa msimu huu kabla ya kurejesha baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu akiwa hajafunga bao lolote hadi sasa, kwa misimu minne ta nyuma, Mwamba alikuwa anajua kucheka na nyavu.
Msimu wa 2020-2021 alitupia mabao sita, uliofuata alifunga saba na msimu wa 2022-2023 alikwamisha mipira tisa nyavuni ikiwamo hat trick moja na msimu uliopita alifunga matatu na kwa sasa baada ya kurejeshwa kikosini ana mechi nne za kuongeza idadi hiyo.

7) DANNY LYANGA-22
Mshambuliaji huyo mwenye mwili jumba aliyewahi kuzitumikia klabu za Coastal Union, Azam, Geita Gold na JKT Tanzania kwa sasa anakipiga Mashujaa iliyomsajili katika dirisha dogo, ndiye anayeshika nafasi ya saba kwenye orodha hii ya wazawa wakali.
Lyanga ambaye ni kaka wa winga machachari aliyepo Singida BS aliyewahi pia kupita Coastal Union na Azam, Ayoub Lyanga analingana mabao na Clement Mzize wa Yanga na Adam Adam wa Tanzania Prisons, kila mmoja akifunga 22, huku Mzize akitumia misimu mitatu tu kufikisha idadi hiyo kulinganisha na wenzake.
Mshambuliaji huyo ambaye kwa msimu huu akiwa na Mashujaa, bado hajatupia bao lolote, amefunga mabao yake 22 katika misimu hiyo mitano, akianza kwa kufunga mabao 10 akiwa na JKT Tanzania msimu wa 2020-2021 kabla ya kutupia manane misimu miwili mfululizo alipokuwa akikipiga Geita Gold, msimu mmoja akifunga sita na mwingine mwili kisha akarudi JKT TZ msimu uliopita alifunga mabao manne kabla ya kutua Mashujaa ambako hajaonyesha makeke licha ya kuasisti mabao mawili.

7) CLEMENT MZIZE-22
Mshambuliaji huyo chipukizi wa Yanga akiwa anaitumikia timu hiyo kwa msimu wa tatu sasa anaonekana ndiye mkali zaidi kwa sasa kwani ametupia mabao 22 akilingana na Lyanga na Adam Adam akitumia misimu hiyo michache kati ya mitano.
Mzize aliyepandishwa kutoka timu ya vijana ya Yanga, kwa sasa amefunga mabao 11 akilingana na Prince Dube pia wa Yanga katika orodha ya wafungaji wa msimu huu wakiwa nyuma ya kinara, Jean Charles Ahoua wa Simba mwenye mabao 12.
Katika msimu wake wa kwanza na kikosi cha Yanga, Mzize alifunga mabao matano na msimu uliopita alitupia sita, huku akimaliza kama Mfungaji Bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) akifunga mabao matano. Mzize ana nafasi ya kuongeza idadi ya mabao kwa mechi tano zilizosalia kwa watetezi hao kabla ya kufunga msimu huu.

7) ADAM ADAM-22
Mshambuliaji huyo wa zamani wa JKT Tanzania, Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar, Ihefu, Azam na Mashujaa kwa sasa anakipiga Tanzania Prisons akiwa ameifungia bao moja pekee, lakini anaingia katika orodha hii ya 10 Bora ya wazawa wenye mabao mengi kwa misimu mitano akiwa na 22 kama ya Mzize na Lyanga.
Adam aliyewahi kuitumikia Prisons kabla ya kupita klabu hizo nyingine aliyafunga mabao hayo 22 kupitia JKT Tanzania (saba), Polisi Tanzania (2), Mtibwa Sugar na Ihefu (matano) na msimu uliopita akiwa na Mashujaa alitupia mabao saba pia. Na juzi kati alifunga bao moja akiwa na Prisons wakati timu hiyo ikiizamisha KenGold mabao 3-1.
Nyota huyo aliyekuzwa na Azam ana nafasi ya kuongeza hazina yake kwa idadi ya mechi nne ilizosaliwa nazo Prisons kabla ya kufunga msimu huu, akiwa na asisti mbili hadi sasa na kikosi hicho kinachopigana kuepuka kushuka daraja.

10) GEORGE MPOLE-21
Mfungaji Bora huyo wa msimu wa 2021-2022 enzi akiwa na Geita Gold akifunga mabao 17, moja zaidi na aliyofunga straika wa Yanga, Fiston Mayele aliyekuwa akichuana naye aliyemaliza na 16, anashika nafasi ya kumi ya wazawa wenye mabao mengi kwa misimu hiyo mitano akimiliki jumla ya mabao 21.
Mpole aliyewahi kukupiga Polisi Tanzania na FC Lupopo ya DR Congo kwa sasa yupo Pamba Jiji akiifungia mabao mawili, kama aliyofunga alipoichezea mara ya mwisho Geita Gold kabla ya kwenda DR Congo.
Mabao mengine mawili aliyoweka katika orodha hiyo aliyafunga na Geita kabla ya kutimkia FC Lupopo, naye ana nafasi ya kuongeza idadi ya mabao kupitia mechi nne zilizosaliwa kwa kikosi hicho cha Pamba Jiji kilichorejea Ligi Kuu tangu iliposhuka 2001.
WENGINE
Ukiacha nyota hao 10 waliokwamisha mabao mengi katika misimu mitano kwa wazawa, pia kuna orodha ya wakali wengine wanaofuta nyuma ya wakali hao akiwamo, staa wa zamani wa Toto Africans, Yanga, KMC na Dodoma Jiji kwa sasa yupo Iraq akicheza soka la kulipwa nchini humo, Wazir Junior akiwa na mabao 20.
Huku Abdul Suleiman ‘Sopu’ aliyepo Azam FC akiwa na mabao 19 aliyoyafunga kupitia timu za Coastal Union na Azam kwa misimu hiyo mitano, ilihali Samson Mbangula akiwa na mabao 18 yote akiyafunga akiitumikia Tanzania Prisons tu.