Faida za mazoezi ya viungo hizi hapa

IWE ni mwanamichezo au mtu yeyote yule anayefanya mazoezi kwa afya anahitaji kufanya mazoezi ya viungo kila mara katika maisha ya kila siku.
Bila mazoezi ya viungo kungelikuwa na idadi kubwa ya majeruhi katika michezo. Vile vile kwa wale wanaofanya kazi maofisini wangeliweza kupata hisia pengine ni wagonjwa.
Ingawa si lazima uwe ni mfanya mazoezi pekee ili ufanye mazoezi ya viungo, hata wale wanaofanya shughuli zinazoushughulisha mwili kama makuli, wakulima, mafundi ujenzi na wafanya kazi wa ndani na wao wanahitaji mazoezi hayo.
Mazoezi haya ndio yanayoufanya mwili ujione ni mpya usio na uchovu wala maumivu ya viungo.
Kwa kawaida kuna aina kuu mbili za mazoezi ambayo ni mazoezi mepesi kitaalam Aerobics exercise na mazoezi magumu yanayojulikana kitaalam kama Anaerobics exercise.
Kabla ya kuingia katika mazoezi hayo na baada ya mazoezi haya ni kawaida walimu wa mazoezi ya viungo kutumia muda wa angalau dakika 5 kufanya mazoezi haya.
Hawafanyi hivi kwa kubahatisha bali ni sahihi hii ni kutokana na ukweli kuwa mazoezi haya ndiyo nyenzo kuu ya kuandaa mwili kufanya majukumu ikiwamo mazoezi mepesi na magumu kwa ufanisi pasipo kujeruhi viungo vya mwili.
Kuamka ni mwanzo wa siku mpya hivyo inahitajika kuwa na mwili na akili mpya na afya njema ili kuweza kufanya majukumu ya kimwili kwa wepesi na ufanisi.
Hata wanyama wafugwao nyumbani huwa na tabia ya kujinyoosha viungo mara tu wanapokuwa wameamka vivyo hivyo kwa mwanadamu hitajika kufanya hivyo ili kuvuna faida mbalimbali za kiafya.
Kwa upande wa wanamichezo au watu wa vyombo vya ulinzi na usalama wanaoshiriki kozi mbalimbali za kijeshi kabla ya kuanza mazoezi yoyote ni kawaida kutumia muda kidogo kufanya mazoezi ya viungo.
Lakini si tu kabla ya mazoezi au mafunzo ya kimwili bali hata wanapomaliza mazoezi au mafunzo ya kimwili ni kawaida kuwaona wakufunzi wa utimamu wa mwili kutoa mazoezi ya viungo.
Kabla ya kuianza siku, wataalam wa sayansi ya mazoezi ya mwili wanashauri unapoamka tu kitandani kufanya mazoezi ya viungo angalau hata kwa dakika 3-5.
Hapa tunapata picha kuwa mazoezi ya viungo yana faida kubwa kuandaa mwili kufanya mazoezi na baada ya mazoezi makali mazoezi ya viungo yanauponya mwili na uchovu hasa baada ya viungo kufanya kazi sana.
Kunyoosha viungo vya mwili huwa ni kwenye maeneo ya misuli, maungio, ngozi, nyuzi ngumu za tendoni na ligamenti na vifupa blastiki ambavyo ndiyo huwa na kazi ya kuujongesha mwili kutoka pointi moja kwenda nyingine.
Unyooshaji huanzia miguuni na mikononi, kiwiliwili, kichwani na shingoni na huitajika kufanyika taratibu kwa muda wa dakika 5-10 mara ili kupata faida zifuatazo.
Faida kubwa ya kwanza ni kuondokana na uchovu hivyo kukufanya kupata utulivu wa kimwili na kiakili.
Kurundikana kwa shinikizo katika misuli huifanya ijikunyate hivyo kuleta hali ya hisia za kukakamaa na kutohisi wepesi. Hali hii huleta madhara hasi kiakili pamoja na kimwili.
Unyooshaji viungo vya mwili husaidia kuondoa shinikizo lililopo katika misuli hatimaye kuuwezesha mwili kuianza siku vizuri kwa ufanisi.
Ndiyo maana wanamichezo au wanajeshi hupasha mwili moto kwa mazoezi kabla ya kuingia kufanya mazoezi au kucheza mechi lengo ni kuvifanya viungo kupata wepesi na kuweza kunyumbulika.
Ikumbukwe pale unapoamka kitandani au katika benchi au popote alipokuwa imetulia unaweza kuhisi uchovu au kuumwa viungo hatimaye kukupa hofu pengine unaumwa.
Kufanya mazoezi haya ndiyo kunaondoa hali hiyo, hatimaye kukufanya unapoingia uwanjani au mazoezini kujiona umepona kwani tayari viungo vimenyooka na kuwa na utayari wa kufanya kazi.
Mazoezi haya yanaifanya misuli ya mwili isibane na kuipa utulivu hivyo kutoa nafasi kwa damu kutiririka kirahisi.
Kemikali zijulikanazo kama Endorphins zinazoufanya mwili kupata hisia za furaha huku pia ikukupa usingizi mzuri hapo baadaye hutiririshwa wakati wa zoezi hili.
Pili kusaidia kuweka ulalo sahihi wa mwili kwa kunyoosha misuli ya mwili iliyokakamaa kwa kuivuta na kuirudisha mahali pake kiasili.
Kunyoosha misuli kama ya eneo la chini mgongoni, kifuani na mabega husaidia kuuweka uti wa mgongo katika mpangilio sahihi hivyo kuepusha uchovu na maumivu.
Tatu kukupa wepesi wa mwili (flexibility) hivyo kuufanya mwili kuwa na utayari wa mabadiliko wakati wowote ikiwamo kwenye mijongeo kama kutembea, kuruka au kukimbia.
Nne kuongeza uwezo (stamina) hivyo huifanya misuli na tendoni kuwa wepesi na laini hatimaye kuondokana na kukakamaa na uchovu.
Kadiri misuli inavyofanya kazi ndivyo pia huchoma kiasi kikubwa cha sukari (glucose). Kunyoosha viungo husaidia kuchelewesha kujijenga kwa uchovu wa mwili kwa kusaidia damu kuingia kwa wingi misulini.
Tano kupunguza majeraha yatokanayo na shughuli za siku ikiwamo kutembea au kunyanyua mizigo.
Hii ni kwa sababu huifanya misuli kupokea damu na virutubisho kwa wingi hatimaye husaidia hupunguza vijidonda vya misuli na huku pia kuiponesha haraka vijeraha vya misuli.
Sita kukupa hisia nzuri na kujiamini kwani mazoezi haya yanakupa burudani hatimaye kuiboresha siku yako katika mazingira ya kazi au masomoni.
Saba kukujenga kinidhamu kwani kunyoosha viungo mara kwa mara kila unapoamka huzoeleka na kuwa sehemu ya maisha yako hivyo kuzipata faida zote kirahisi.
Hizi ni zile faida za kiafya ambazo zimeonekana kirahisi ingawa zipo nyingi zaidi, ni muhimu kushikamana na mazoezi haya ili kudumisha Afya ya mwili na akili hatimaye kuianza vyema siku au mazoezi tunayofanya.
Usiache kujiongezea maarifa kuhusu mazoezi haya kila mara kwani inasaidia kupata taatifa mpya zenye faida kubwa kiafya.