EVODY: Beki aliyewazima mastaa Simba akiichezea Mtibwa Sugar
Muktasari:
- Evody ni nahodha msaidizi wa Mtibwa Sugar, ni beki ambaye amevaa kitambaa cha unahodha tangu akiwa timu ya vijana ya timu hiyo na amepata bahati ya kupanda anaaminiwa kupewa usinga mkononi.
HAROUB Evody ndiye aliyekuwa shujaa kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 kati ya wenyeji Simba na Mtibwa Sugar kwa kukabidhiwa tuzo ya mchezaji bora baada ya dakika 90 kutamatika.
Evody ni nahodha msaidizi wa Mtibwa Sugar, ni beki ambaye amevaa kitambaa cha unahodha tangu akiwa timu ya vijana ya timu hiyo na amepata bahati ya kupanda anaaminiwa kupewa usinga mkononi.
Mwanaspoti limepata bahati ya kuzungumza na mchezaji huyo chipukizi kutoka timu ya vijana ya Mtibwa Sugar ambapo amefunguka mambo mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuona nafasi ya mabeki kwa wazawa kuaminika kwani wana vipaji na wanaweza kuzibeba timu zao kama ilivyo kwa Yanga ambayo inaongozwa na Dickson Job, Abdallah Hamad ‘Bacca’ na Bakari Mwamnyeto.
Soko la nyota wa kigeni limehamia eneo la kiungo na washambuliaji hivyo ndio unaweza kusema kwa miaka ya karibuni licha ya eneo la beki pia kuguswa, lakini sio kwa ukubwa kama ilivyo kwa washambuliaji na viungo.
Wakati dirisha la usajili likifungwa tayari usajili mwingi umefanyika ukilenga eneo la viungo hasa timu za Simba, Yanga, Azam na Singida Black Stars ambazo ndizo zina msuli mkubwa wa kusajili nyota wengi wa kigeni.
WAZAWA WAAMINIWE
Inaelezwa kuwa Ujio wa nyota wa kigeni katika soka la Tanzania umekuwa chachu ya kukua kwa Ligi Kuu Bara lakini nahodha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Evody amesema licha ya nyota wa kigeni kuongeza chachu ya ushindani lakini viongozi waangalie namna kwa kuthamini ubora wa wazawa.
“Kwa nafasi ya mabeki wa kati wazawa wapo wengi wazuri shida iliyopo ni kutokuaminiwa na timu kubwa ambazo zinatazama zaidi nyota kutoka mataifa mbalimbali huku zikiacha vipaji vikubwa,” anasema.
“Mfano mchezaji kama Oscar Masai kwa mabeki wa Tanzania yupo vizuri na ana mchango mkubwa katika kikosi cha Mtibwa hadi kufikia nafasi tuliyopo, akiaminiwa na kupewa nafasi ana uwezo wa kufanya mambo makubwa.”
Anasema Yanga imefanikiwa kuwa bora eneo la ulinzi ikiongozwa na wazawa ambao pia wamekuwa wakifanya vizuri kwenye kikosi cha timu ya taif na ili kuwe na mwendelezo wa kutengeneza nyota wengine bora ni klabu kuamini wazawa.
CHACHU YA UBORA
Licha ya kutaja ubora wa wazawa katika nafasi anayocheza beki wa kati kuwa wanastahili kuaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza kwenye klabu kubwa za Simba, Yanga, Azam na Singida Black Stars ambazo zina utamaduni wa kusajili nyota wa kigeni, Evody anautaja umuhimu wa nyota wa kigeni kwenye ligi.
“Kuna faida tunayopata kupitia wachezaji wa kigeni hususan mabeki wa kati. Changamoto inaongezeka kwa kuwa ligi yetu kila siku inakuwa bora zaidi. Ila hata mabeki wazawa wanafanya vizuri katika nafasi ya beki, hivyo waaminiwe.
“Sina maana kwamba nafasi nyingine wazawa hawafanyi vizuri, lakini nina mfano mzuri kwa mabeki kwa kuitazama Yanga imetengeneza uaminifu mkubwa ambao umekuwa na faida, si kwa timu hadi taifa kwani mabeki wao ndio wanaotumika timu ya taifa,” anasema mchezaji huyo.
Anasema uwepo wa nyota wa kigeni kwenye ligi umekuwa chachu ya kukuza na kuendeleza vipaji vingi kutokana na ushindani akiomba usajili wa nyota hao uzingatie ubora na sio kuletwa wakiwa na viwango vya kawaida.
SIRI YA UBORA
Licha ya kupanda kutoka timu ya vijana, Evody ameaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza huku akiwa na kitambaa cha unahodha mkononi, na mwenyewe anaweka wazi siri ya nafasi hiyo.
Mchezaji huyo anawashukuru makocha kuanzia timu ya vijana hadi wakubwa kumuamini na kwamba ataendelea kupambana bila kuchoka.
“Mimi napenda kujifunza ni mwanafunzi siku zote. Napenda kuwa bora, hivyo siku zote nidhamu yangu nikiwa uwanjani na nje ya uwanja vimekuwa sehemu ya mafanikio yangu na waalimu wanapenda mtu ambaye hakuzwi na mafanikio, siku zote anajifunza hiki ndio kitu kinanibeba,” anasema.
“Ukiondoa hivyo pia nimekuwa mwanafunzi wa kuangalia watangulizi wangu. Napenda kuwaangalia mabeki wote wanaocheza Ligi Kuu na hata wanaocheza madaraja ya chini. Huko nachota ujuzi na kuwa bora kila siku zinavyokwenda.”
Evody anasema pia amekuwa bora kwa kuwatazama zaidi mabeki anaofanya nao kazi pamoja ili aweze kuendana nao wanapokuwa uwanjani, na asifanye makosa kwa kuwa yupo nao muda mwingi mazoezini.
Pia anakuwa nao kwenye mechi muda mwingi na akikosea wanamuelekeza bila shida, na anapokea maelekezo kuyafanyia kazi.
GEITA GOLD
Bado Evody anajitafuta kwenye Ligi Kuu Bara kutokana na umri na nafasi aliyoipata akipandishwa kutoka timu ya vijana, ambapo anasema kwenye mechi za ushindani alizocheza hatasahau fainali timu ya vijana chini ya miaka 20 dhidi ya Geita Gold.
“Mechi ambayo siwezi kuisahau maishani mwangu ni mechi ya fainali ya under 20 na Geita. Ile mechi yaani kuna muda nakaa natazama marudio, ilikuwa bora sana kwangu, kwani imeacha historia kutokana na kufanikiwa kutwaa taji kwa jasho sana,” anasema na kuongeza:
“Fainali hiyo ilichezwa kwa dakika 120, tulitwaa taji baada ya kupata bao dakika ya 117. Ilikuwa fainali bora sana kuwahi kutokea timu zote zilikuwa bora na ubora wa Mtibwa ulithibitika dakika hizo tulizopata bao.”
KUVAA GWANDA
Licha ya kuwekeza juhudi kwenye soka akili yake inatamani kutimiza ndoto ya siku moja kuvaa gwanda la jeshi kwani ndicho anapenda nje ya mchezo huo, na kama asingepata nafasi ya kuonyesha kipaji chake angekuwa mwanajeshi.
“Kama sio mpira nilipenda sana nije kuwa mwanajeshi na bado nina ndoto hizo. Ni kazi nayoipenda sana. Nilijaribu kufuatilia kipindi cha nyuma nafasi za jeshi, lakini ikashindikana ikanibidi niendelee kupambana na mpira,” anasema.
“Bado sijakata tamaa, nafasi ikitokea nitafanya hivyo kwani umri unaniruhusu. Pia elimu yangu ya kidato cha nne na matokeo niliyoyapata yananipa nafasi ya kwenda kutimiza ndoto yangu kama ilivyo kwenye mpira.”
COLLINS, JOB HIZI BEKI KWELI
Ligi Kuu ina mabeki wengi bora kulingana na uchezaji na namna ambavyo wanazibeba timu zao, lakini Evody anamtaja Victor Collins ambaye anacheza Mtibwa Sugar na nahodha wa Yanga, Job, kuwa mabeki anaowakubali.
“Kwa beki wa kigeni ni Victor Collins, ni beki ambaye anatumia sana akili, anajua sana na ni mzuri kuelekeza uwanjani, hivyo mbali na ubora wa kucheza ni kiongozi. Napenda aina ya uchezaji wake, nimekuwa nikijifunza mengi kutoka kwake kwani ni kaka yangu kiumri na kiuchezaji,” anasema.
“Kwa upande wa wachezaji wazawa Masai ni beki bora kwangu kwa muda wote, na navutiwa kumuona akicheza. Ni beki mgumu na ni mhamasishaji anapokuwa uwanjani. Pia kuna Jamal Masenge anacheza Tanzania Prisons.”
YONDANI, NDITI WALIMVUTA
Miaka ya nyuma wachezaji wengi ambao sasa wanafanya vizuri walikuwa wanaingia kwenye mchezo wa soka kutokana na kuvutiwa na watangulizi wao, lakini pia mapenzi ya mchezo huo tofauti na sasa ambapo soka imekuwa biashara na ajira kwa vijana kama anavyodai Evody.
“Napenda mpira tangu nikiwa na umri mdogo na kulikuwa na wachezaji nawatazama na kuamini kuwa ipo siku nitakuwa kama wao. Walikuwa wananipa nguvu na imani ya kupambana zaidi ili niweze kufikia walipo wao,” anasema.
“Sio wengine ni aliyekuwa beki wa Simba, Yanga na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Kelvin Yondani. Ni mchezaji aliyenivutia hadi kuingia kwenye soka. Shabani Nditi, Agrey Morris, Salim Mbonde hawa ni sehemu ya mafanikio yangu hadi hapa kwani nilikuwa nawatazama kama mfano wa kuigwa na kupendezwa na namna walivyokuwa wanacheza.”