Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Elimu ya michezo mashuleni ipewe kipaumbele

Muktasari:

Wanamichezo, wanasiasa na hata watetezi wa haki za watoto hawakuliona hili kama tatizo kwa watoto kukosa haki yao ya msingi ya kucheza ambayo kila mtoto anatakiwa kuwa nayo kwa mujibu wa azimio la saba la Umoja wa Mataifa la haki za watoto la mwaka 1959.

WAHENGA wanasema ‘kufanya kosa si kosa ila kurudia kosa ndio kosa’ sote tunakumbuka mwishoni mwa miaka ya 1990 vipindi vya michezo mashuleni vilionekana kuwa vinapoteza muda wa wanafunzi kusoma masoma mengine muhimu darasani, hivyo serikali kupitia Wizara ya Elimu ikafikia uamuzi wa kuondoa michezo katika shule za msingi na za sekondari zinazosimamiwa na serikali ingawa hata shule nyingine zilifanya hivyo.

Wanamichezo, wanasiasa na hata watetezi wa haki za watoto hawakuliona hili kama tatizo kwa watoto kukosa haki yao ya msingi ya kucheza ambayo kila mtoto anatakiwa kuwa nayo kwa mujibu wa azimio la saba la Umoja wa Mataifa la haki za watoto la mwaka 1959.

Haki hiyo inatoa nafasi kwa watato kuonesha vipaji vyao katika michezo mbalimbali ukiachilia mbali uwezo wao kuelewa masomo ya darasini kwani inapofika muda wa michezo, kila mtoto hukimbilia kwenye mchezo anaoupenda hivyo kuwarahisishia kazi waalimu na wagunduzi wa vipaji vya michezo katika kuviibua na kuvikuza.

Ni kwenye umri huo huo baada ya watoto kuonekana kuwa na kipaji cha mchezo fulani ndipo waalimu huendeleza vipaji hivyo kwa kuwaongezea maarifa na nidhamu ya mchezo husika huku wakielekezwa pia umuhimu wa elimu kama wengine tulipopita.

Na kwa kuwa mtoto umleavyo ndivyo akuavyo ndio maana wazazi wengi hupoteza muda mwingi kuwaelekeza watoto wao ili wakue katika misingi sahihi ya uadilifu na wengine kutaka watoto wao wapitie katika njia walizopitia wao ili na wao wawe kama wazazi hao walivyo. Jitihada zote hizi hufanyika wakati ambapo watoto huwa wanaanza kujiunga shule za chekechea hadi shule za msingi kwani wazazi wote wanajua kuwa umri huo ndio umri sahihi kwa watoto kuwa wa uelewa wa kutofautisha mabaya na mazuri na kuanza kuonesha hisia za mchezo anaoupenda kutoka moyoni.

Hivyo watoto ambao hawapati maelekezo sahihi katika umri huo wengi wao hujikuta wakipotea na kushindwa kufikia hata malengo ambayo pengine familia zao zilitarajia ikiwa ni pamoja na kushindwa kuvitumia vipaji vyao ambavyo hapo awali vilionekana lakini vikashindwa kuendelezwa. Na vijana wa aina hii wenye vipaji ndio wamejaa kwenye michezo mbalimbali hapa kwetu Bongo kitu ambacho kimekuwa kikiwafanya Watanzania wengi waendelee kuimba ule wimbo wa kila siku wa kuwa na vipaji vingi ila kushindwa kuviendeleza.

Nimesema hayo kwa kuwa sote tunafahamu umuhimu wa elimu ya msingi katika maendelo ya mwanafunzi wa kada zote kwani elimu hiyo ya msingi ambayo wakati wetu kigezo cha kuingia ilikuwa lazima mtoto aweze kugusa sikio la upande wa kulia kwa mkono wa kushoto au la kushoto kwa mkono wa kulia huku mkono huo ukipitia juu yaani utosini.

Hivyo watoto wenye umri kuanzia miaka saba ilikuwa ndio wengi wanoanza elimu ya msingi ingawa maeneo ya vijijni haikuwa taabu kwa watoto wengine wenye umri hata wa miaka 10 hadi 12 kujikuta wakianza shule za msingi wakiwa na umri huo. Siku hizi mambo mengi yamebadilika kutokana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ndio maana wapo watoto wanaoanza shule ya msingi wakiwa na umri wa miaka hadi mitano, sita na wengine miaka saba.

Umri huu wa kuanzia shule ya msingi ndio umri wanaouita Waingereza ‘Golden age of learning’ yaani umri sahihi kwa mtoto kuanza kujifunza na kushika vitu vya msingi kichwani. Ndio umri ambao watoto wanafundishwa misingi ya elimu watakayoendelea nayo hadi vyuo vikuu, ndio umri ambao vijana wenye vipaji wanafundishwa mambo ya msingi katika kuendeleza vipaji vyao ambavyo watavitumia miaka 10 au 20 ijayo.

Leo nimeandika makala hii kuhusu elimu ya msingi kwa kuwa watoto wengi wanaojiunga katika shule nyingi za msingi nchini wanakosa moja kati ya haki zao za msingi ya kushiriki katika michezo tu kwa sababu michezo iliondolewa katika mitaala ya kufundishia katika shule za msingi na sekondari na hivi karibuni kuonekana kurudishwa kwenye shule hizo lakini bado upokelewaji na utekelezwaji wake ni wa kiwango cha chini kutokana shule nyingi kukosa walimu wa michezo na miundombinu ya michezo kwa maana ya viwanja.

Hivyo watoto kukosa haki yao na taifa pia kukosa wanamichezo wa baadae ambao wangeweza kulifikisha taifa katika kilele cha mafanikio katika tasnia ya michezo.

Yote haya yanatokea kwa kuwa tumesahau na hatutaki kujikumbusha kuwa wanamichezo wote waliodumu kwenye michezo kwa muda mrefu kuanzia miaka ya 1990 mwishoni kurudi nyuma walipitia katika michezo ya shule za msingi na za sekondari hivyo kuimarika kimchezo na kitaaluma.

Mbaya zaidi ni sababu iliyotumika ya kuondoa michezo mashuleni kuwa eti michezo inawapotezea watoto muda wa kijifunza huku wakisahau kuwa michezo yenyewe inahitaji muda sahihi wa kujifunza pia. Nakumbuka hiyo ndiyo iliyokuwa sababu ya kuiondoa michezo mashuleni.

Serikali walisahau kuwa watoto hao hao wanatakiwa pia kujifunza michezo katika umri huo huo kwani baadaye michezo hiyo hiyo inaweza kuwa ndio njia ya kuwaendeshea maisha yao kama tunavyoona sasa namna vipaji vya akina Usain Bolt, Floyd Maywether, Serena Williams, Kobe Bryant, Nwankwo Kanu na wengineo wengi ambao wanaendesha vema maisha yao kupitia vipaji vyao walivyojaaliwa na muumba.

Kutokana na sababu hiyo kutolewa, wapo baadhi ya wazazi walioamini kweli kuwa michezo ilikuwa inawapotezea muda watoto wao huku wakishindwa kujua kuwa kila kitu kinatakiwa kuwa na muda wake, yaani wakati wa michezo ni michezo na wakati wa masomo ya darasani ni masomo.

Hapa kwetu uamuzi mwingi hufanyika bila ya kufanyika utafiti wa kina hivyo ni bahati mbaya sana tafiti zilizofanyika kwa miaka ile ilielezwa kuwa hazikuzingatia mambo mengine ya msingi katika kufikia uamuzi ule kwani tafiti yoyote ya kutaka kujua tija ya michezo mashuleni lazima iwe ‘multi disclipline’ yaani itakayochanganya wataalamu wenye taaluma mbalimbali kuanzia waalimu, wanasosholojia, wanasaikolojia, wataalamu wa masomo ya maendeleo na wengineo.

Itaendelea Jumamosi ijayo...

wengi hivyo kuwa ngumu na yenye kuchukua muda mrefu.

Lakini katika tamasha kubwa la mpira wa miguu la Soccerrex la mwaka 2013 lililofanyika Durban nchini Afrika ya Kusini viongozi wa soka kutoka Nigeria waliwasilisha mada kutokana na tafiti iliyofanywa na wizara ya michezo ya nchi hiyo a ambayo iliyotoka na majibu kuwa shule zinazofundisha michezo nchini Nigeria ndizo zilizokuwa zikifanya vema katika matokeo ya wanafunzi wa sekondari kuliko shule zisizokuwa na michezo hivyo kuzishawishi shule hizo kuiga mfano huo ili ziweze kupata matokeo mazuri kwa wanafunzi wao.

Sina uhakika ni watanzania wangapi walihudhuria katika kongamano hilo lakini Shaffi Dauda wa Clouds FM alikuwepo na alishuhudia uwasilishwaji huo. Nakumbuka wakati Kanali wa jeshi mtaafu Iddi Kipingu pamoja na Kanali Mstaafu Fabian Massawe wakati wanafanya jitihada za kuendeleza michezo kupitia shule walizokuwa wakizisimamia wakati huo, Makongo na Jitegemee kwa kukusanya wanafunzi wenye vipaji katika michezo mbalimbali na kuwasomesha.

Siku zote walikuwa wakituambia wanafunzi wao wa wakati huo kuwa hawajawahi kuwa na hawatarajii kuwa na wanafunzi wanamichezo ambao ni wazito wa kuelewa kwani michezo ya utotoni huongeza uharaka wa kufikiri kwa mtoto ili kumshinda yule anayeshindana nae hivyo wanafunzi wanamichezo siku zote huwa ni fast learners yaani waelewa wa haraka isipokuwa usimamiaji wa ratiba za wanafunzi wanamichezo ndio kitu cha muhimu kwa wanafunzi hao pamoja na waalimu wao.

Naandika huku nikifarijika kuona katika matokeo ya kidato cha nne ambayo yametoka hivi karibuni yanaonesha shule ya Alliance ya jijini Mwanza ikiwa katika nafasi ya pili kwa kufaulisha wanafunzi wa kidato cha nne kwa Taifa kitu ambacho kinaweza kuthibitisha kuwa michezo haiwezi kuwa sababu ya kutofanya vizuri ila usimamizi wa ratiba za michezo ndicho kitu muhimu.

Kumbuka shule hii pia inachukua wachezaji wanafunzi wengi wenye vipaji kwa ajili ya kuendelezwa vipaji vyao huku wakipewa elimu, shule hii hii pia ndio itakayokuwa mwenyeji wa michuano iliyoahirishwa ya kitaifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 13 ili watakaoonekana kuwa na vipaji na kuchaguliwa watapata nafasi ya kusomeshwa kwenye shule hiyo. Hivyo ni faraja kwa wanamichezo na hasa vijana ambao wana vipaji halisi vya mchezo wa soka ambao wanaweza kupata nafasi kwenye shule hiyo kisha kupata vitu viwili katika viwango stahiki, yaani elimu sahihi pamoja na elimu ya mchezo wa soka.

Wataalamu wa maswala ya mitaala ya kufundishia watakuwa wanafahamu kuwa elimu sahihi hutakiwa kutolewa katika muda na wakati sahihi pia kwani katika mzunguko wa maisha ya mwanadamu anapofikisha umri fulani basi hata aina ya elimu anayohitaji huzingatia umri huo ndio maana wenzetu wa mikoa ya pwani husikia mtoto wa kike anapofikisha umri fulani husikia akienda kuchezwa ngoma ambapo pamoja na mambo mengine lakini pia hufundishwa namna ya kuishi kwenye nyumba kama mama mwenye nyumba.

Ndio maana wataalam hao husisitiza mambo ya msingi yafundishwe katika elimu ya msingi kwani huwa ndio msingi wa kupata elimu nyingine kubwa mbeleni. Hivyo wanamichezo nao hutakiwa kupata elimu ya misingi ya michezo katika wakati sahihi kulingana na vipaji vyao ambavyo mwenyezi mungu kawajaalia ili elimu hiyo ije iwasaidie katika kupata elimu nyingine iwapo wataamua kuendeleza vipaji vyao na kufikia katika ngazi za kimataifa.

Mwisho niseme tu yoye haya yanaendelea kutokea kwa kuwa siku hizi imejengeka tabia kila mtu kuchambua mapungufu ya kiuongozi hata wale waliopewa majukumu ya kuendeleza sekta hii na wanaotakiwa kuyafanyia kazi nao pia hujikuta wakutumia muda mwingi kuyachambua mapungufu hayo hayo bila ya kutekeleza wajibu wao kwanza.

Kwani kila mmoja kwenye nafasi yake akiweza kufanya kile kinachotakiwa katika michezo sidhani kama inaweza kufika miaka kumi mbele bila ya kuanza kuona matunda yake. Kwani wapo baadhi ya wadau ambao ambao hawajatekeleza majukumu yao ipasavyo katika michezo mashuleni lakini tumekuwa tukiwasikia wakitoa maoni kuhusu kuanzishwa kwa vituo vya kukuza na kuendeleza vipaji huku wakisahau kuwa shule za msingi na sekondari ni zaidi ya vituo hivyo.

Katika hili pengine tukumbushane tu kuwa tumekuwa tukiona vituo hivi vya michezo kwenye nchi zilizoendela kama vile Hispania, Ujeruamni, Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya na Marekani lakini kabla ya kuiga chochote kwanza tunatakiwa kuangalia tofati zilizopo kati ya nchi hizo na nchi yetu ili kuweza kuanzisha na kuviendesha vituo hivyo na kutuletea matokeo.

Kuna tofauti ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiteknolojia na kijiografia pia kati ya nchi hizo na nchi yetu hivyo kile kinachiweza kufanyika kule na kuzalisha si rahisi kitu hicho kuleta majibu kama yale yale wanayoyapata wao kwani kuna maswala mengi mtambuka ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi ikiwemo tija kati ya vituo na shule za msingi na sekondari ambazo ni ‘natural academies’ yaani vituo vya asili.

Kwa msingi huo utaona kabisa kuwa dawa ya yote haya ni kutoa fursa kwa watoto kucheza mashuleni na kuonesha vipaji vyao kwenye shule za msingi na za sekondari kisha kuwa na ratiba sahihi zitakazosimami utakelezaji wa sera ya michezo mashuleni na hatimaye watoto kufanya vizui darasani kama walivyofanya Alliance ya Jijini Mwanza.