EDITH KLINGER: Mwamuzi wa kwanza wa kike aliyeleta mageuzi katika soka

Muktasari:
- Wanaume wengi waliwaona hao ni wanawake wa ajabu kwa vile kandanda ilitambulika kama ni mchezo wa wanaume, japo walikuwapo wanawake walioucheza kuanzia mwishoni mwa karne ya 16.
HADI ilipoanza nusu ya mwisho ya karne ya 20, yaani mwaka 1951 idadi ya mashabiki wanawake waliofika uwanjani kuangalia mchezo wa kandanda ilikuwa ndogo sana.
Wanaume wengi waliwaona hao ni wanawake wa ajabu kwa vile kandanda ilitambulika kama ni mchezo wa wanaume, japo walikuwapo wanawake walioucheza kuanzia mwishoni mwa karne ya 16.
Ni kuanzia mwaka 1970 ndipo mchezo huu kwa wanawake ulipoanza kupata maarufu na hasa baada ya Italia kuwa nchi ya kwanza kuunda timu ya taifa ya kandanda ya wanawake.
Lakini mageuzi yanayotokea katika kila sekta pia yameukumba mchezo wa kandanda.
Hii leo wastani wa wanawake wanaofika viwanjani kuangalia mpira ni asilimia 10 katika nchi za Kiarabu na Asia, asilimia 30 Amerika ya Kusini na asilimia 42 katika nchi za Ulaya.
Haya ni mabadiliko makubwa kwani hali viwanjani sasa ni tofauti kwa vile wapo wachezaji , watazamaji, waamuzi na walimu wengi wanawake, hata kwa timu za wanaume.

Katika mwaka 1935 zaidi ya nusu ya watazamaji 600 waliomiminika uwanjani kuangalia pambano la Austria walitoka nje kwa hasira mara timu zilipojngia uwanjani.
Kilichowakasirisha ni kuona mwanamama ambaye ni mzaliwa wa nchi hiyo, Edith Klinger, akiingia na filimbi akifuatana na washika vibendera wawili wanaume.
Uamuzi wa mwanamke kuwa msimamizi mkuu wa mchezo ulitafsiriwa na wanaume kama kitendo cha dharau.
Uamuzi wa wale wanaume ulikuwa ni uthibitisho wa wanaume wengine wa wakati ule kuonyesha dharau kwa kina mama na kuwaona wao ni viumbe wasiostahiki kuwaongoza wala kuwasimamia wanaume, hata katika michezo.
Ninakumbuka nilizoeleka siku za nyuma Zanzibar ilipotokea mwanamke kuonekana akiendesha baiskeli au kucheza kandanda na wanaume aliitwa kidumedume.
Hata namna watazamaji na waandishi wa michezo wengi bado wanazo tafsiri za zama za kale wanapouchambua mchezo wa kandanda.

Kwa mfano, timu za kandanda za wanawake zinapocheza na moja kufungwa kwa tabu utasikia timu hiyo ilipambana na kiume. Sijui kupambana kike kumekaa vipi.
Hapo zamani hata ilipotokea mwanamke kuuliza matokeo ya mchezo wapo watu walioshangaa, kama vile ni jambo la ajabu.
Katika nusu ya mwisho ya miaka ya 1960 nilipoandika habari za michezo ilikuwa si kawaida kuona zaidi ya wanawake 10 kufika uwanja wa Ilala (siku hizi Uwanja wa Karume), Dar es Salaam kuangalia mchezo.
Hao wanawake wawili au watatu waliofika waliangaliwa zaidi na baadhi ya watazamaji kuliko kuelekeza macho yao kwenye mchezo.
Katika miaka ya mwisho ya 1950 na mwanzo wa miaka ya 1960 Zanzibar alikuwapo mwalimu, msanii maarufu na mchezaji wa klabu ya Vikokotoni na timu ya Zanzibar na baadaye muamuzi, Musa Bakari, aliyefika uwanjani na mke wake.

Hii ilikuwa awe uwanjani anacheza, akiwa mwamuzi au akiwa amekwenda kuangalia mchezo.
Wote wawili sasa ni marehemu, lakini wameacha kumbukumbu ya aina yake katika historia ya soka ya Zanzibar.
Hadi mwanzoni mwa miaka ya 1930 wanawake waliocheza kandanda au kuwa waamuzi katika nchi nyingi walikuwa wachache.
Katika mwaka 1935 alijitokeza mwanamke wa kwanza Austria, Edith Klinger, kuwa mwamuzi wa kwanza wa kandanda na kuchezesha timu za wanaume na wanawake kati ya 1935 hadi 1938.
Haikuwa rahisi hapo mwanzo kwani baadhi ya wachezaji wanaume walionekana hawakufurahishwa na mwanamke kuwa ndio mwamuzi.
Lakini baada ya kumudu mikikimikiki ya kukataliwa na kuzomewa, mwanamama huyu aliwahamasisha wanawake kucheza na kuchezesha kandanda licha ya kupata pingamizi kutoka kwa wanaume.
Hapo kwanza alishitakiwa alipounda timu ya mpira ya wanawake mwishoni mwa miaka ya 1920.

Kelele za kina baba na wanawake zilipokuwa nyingi wanawake walipigwa marufuku kucheza kandanda Austria na baadhi ya nchi za Ulaya.
Hata hivyo, walikuwapo wanawake waliocheza kandanda kwa siri kama ilivyojitokeza katika miaka ya hivi karibuni katika baadhi ya nchi za Kiarabu.
Dada huyu wa Austria aliyezaliwa Desemba 20, 1911 alikuwa mwanamke aliyejihusisha na mengi yaliyoonekana hayastahili wanawake kujihusiha nayo wakati ule.
Ukakamvu wake ulichangia baadaye kutambulika kuwa sio mchezaji mzuri wa kandanda na mwamuzi tu, bali pia mcheza sinema na mchambuzi wa masuala mbalimbali katika runinga, ikiwa pamoja na kandanda.
Michezo yake ya sinema iliyompatia umaarufu ni pamoja na Kiss Me Casanova (1949), Good Fortune in Ohio (1950) Aprili (1952) na Herr Puntila and His Servant Matti (1955).
Katika mwaka 1935 yeye na rafiki zake waliunda timu ya wanawake iliyoitwa Erste Wiener Damenfussball Club na baadaye Tempo.
Willy Schmieger, aliyekuwa mwandishi wa habari maarufu wa michezo Austria, aliwaunga mkono na kueleza ni haki yao kucheza kandanda kama wanaume.
Aliwaambia watu waliopinga kama walivyokuwa wanakataa wanawake wasicheze soka basi pia wawakatae mama na wake zao.
Hapo ndipo watu wa Austria, wakiwamo wanasiasa na wafanyabiashara wa nchi hiyo na za jirani walipojitokeza kuwaunga mkono wanawake kucheza kandanda.
Kilichofuatia ni kuwekwa utaratibu wa wanawake kuruhusiwa kucheza kwa kati ya dakika 20 na 25 eti kwa sababu hawawezi sulubu kucheza muda mrefu.
Katika mwaka 1935 ndio yalipotayarishwa mashindano ya kwanza ya klabu bingwa ya soka Austria na mwaka uliofuata likaundwa Shirikisho la Soka la Wanawake la Austria.
Edith alikwenda hatua moja zaidi alipochukua mafunzo ya uamuzi na kufuzu kuwa mwanamke wa kwanza kupuliza filimbi katika mchezo huu kwa kuwa mwamuzi wa timu ndogo ndogo huku akiwashawishi wanawake kushiriki michezo.
Utawala wa kidikteta wa manazi wa Italia ulipoiteka Austria mwaka 1938 ulipiga marufuku mchezo wa kandanda kwa wanawake.

Wakati huo Edith alishakuwa mwamuzi wa michezo miwili ya kimataifa ya wanaume.
Baada ya Vita Kuu vya Pili vya Dunia kumalizika 1945 aliwashawishi wanawake kupenda kandanda na kufanya kampeni ya kuwapo mashindano ya Kombe la Ulaya na Dunia kwa wanawake.
Katika miaka ya mwisho kabla ya kuiaga dunia mwaka 2013 alifika kwenye viwanja na kusisitiza umuhimu wa mchezo wa soka kwa kina mama na kudai haki zote wanazopata wanaume katika michezo nazo wapate kinamama.