Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Drama zilivyokuja kutuliza ndoa ya  Enzo, Valentina

Muktasari:

  • Baada ya kuishi pamoja London kwa miezi 18 tangu ajiunge na Chelsea, Enzo alimvunja moyo mkewe baada ya kumwambia kwamba hataki tena kuwa naye, hivyo kila mmoja ashike njia yake.

KIUNGO wa Chelsea, Muargentina Enzo Fernandez, 25, na mwandani wake wa muda mrefu, Valentina Cervantes, 24, wanaishi maisha mazuri nje na ndani ya nyumba mpya ya kifahari iliyopo jijini London, Uingereza.

Hata hivyo, nyuma ya maisha yao wamepitia kipindi kigumu ambapo uhusiano wao uligonga vichwa vya habari kwa mambo yasiyo mazuri ikiwemo migogoro na drama nyingi. 

Baada ya kuishi pamoja London kwa miezi 18 tangu ajiunge na Chelsea, Enzo alimvunja moyo mkewe baada ya kumwambia kwamba hataki tena kuwa naye, hivyo kila mmoja ashike njia yake.

Valentina alithibitisha habari hiyo kupitia mitandao ya kijamii, Oktoba 2024, kupitia Insta story yake alitangaza kwamba yeye na Enzo wametengana. “Mimi na Enzo tumeamua kuweka umbali kati yetu kuanzia leo. Lakini tutabaki kuwa familia daima, na tutaendelea kusaidiana katika kila jambo, kwa sababu tuna watoto wawili wanaohitaji upendo mkubwa kutoka kwetu.

“Najua Enzo ni mtu wa aina gani, ni baba bora kiasi gani, na ana moyo mzuri. Hilo linanitosha. Tafadhali msijaribu kuanzisha migogoro pasipo na sababu,” alisema Valentina.

Baadaye aliongeza kuwa bado anampenda Enzo na alimtakia kila la heri. Inaelezwa kwamba Valentina alirejea kwao Argentina pamoja na watoto wao wawili, Olivia (2020) na Benjamin (2023).

Mwandishi wa habari kutoka Argentina, Julieta Argenta, alitoa maelezo zaidi kuhusu kutengana kwao akidai kuwa mchezaji huyo alipanga kuishi maisha yake mwenyewe. “Alimwambia kuwa anataka kuishi maisha yake mwenyewe. Bado wao ni familia, lakini anahisi anahitaji kupitia hatua ya maisha ambayo aliikosa kwa sababu alichagua kuwa na familia mapema,” alieleza Julieta.

Wakiwa wametengana, Enzo alihusishwa kutoka kimapenzi na rapa wa Argentina, Nicki Nicole, pamoja na mwanamitindo Pampita Ardohain, ingawa wote walikanusha madai hayo. Hata hivyo, ripoti za mwanzoni mwa 2025 zilionyesha kwamba Enzo alirudiana na mama wa watoto wake, yaani Valentina, ambapo walionekana wakisafiri pamoja kwenda London kusherehekea mwaka mpya.

Baadaye walionekana wakibusiana na kushikana mikono jijini humo, jambo lililochochea uvumi kuwa wamerudiana.

Valentina alithibitisha rasmi kurudiana huko mnamo Aprili 2025 kwa kuposti picha kwenye Instagram akimuonyesha Enzo akiwa amepumzika kitandani katika hoteli moja jijini Madrid. Mwezi uliofuata, Valentina alionekana akiwa naye uwanjani baada ya ushindi wa Chelsea katika fainali ya UEFA Conference League wakiichapa Real Betis mabao 4-1, ambapo moja ya mabao hayo alifunga Enzo.

Hata hivyo, drama nyingine ilizuka tena ndani ya uhusiano wao, awamu hii akitajwa mke wa zamani wa mchezaji wa Argentina Mauro Icardi, Wanda Nara aliyedaiwa kumtumia Enzo ujumbe wa kimahaba.

Inadaiwa Enzo alimuonyesha mpenzi wake ujumbe huo akisema ni mwaliko wa kushiriki kwenye kipindi cha MasterChef Celebrity Argentina kinachoendeshwa na Wanda, kitu kilichomchefua Valentina. Kulingana na Jarida la Caras, hali hiyo ilisababisha mazingira ya wasiwasi, lakini Valentina mwenyewe alijaribu kupunguza uvumi wa mgogoro huo kwenye kipindi cha SQP kinachoruka La Nacion.

“Sina tatizo lolote na Wanda Nara; hajawahi kunifanyia chochote kibaya. Watu wataendelea kutunga stori zao lakini mimi sina tatizo naye. Hakuwahi kunifanyia chochote,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema: “Ndio, niliona taarifa hizo ila ukweli ni huu, sijaona ujumbe wowote. Enzo hajawahi kuniambia chochote kuhusu hilo, na hata sikumuuliza.”

Valentina alipoulizwa kuhusu kutengana na kurudiana kwao, alisema: “Nafasi za pili zipo kwa kila mtu, kwa sababu sisi ni binadamu na tunakosea. Lakini hakuna nafasi ya tatu au ya nne. Kwa sasa tunaendelea vizuri sana; tumefahamiana kwa muda mrefu. Enzo akiniangalia sasa anajua kinachoendelea kwangu.”

Kwa upande mwingine alisema pia kutengana kwa muda kuliimarisha uhusiano wao, kwani kilimpa mtazamo mpya, kugundua mambo mengi na kuthamini vitu zaidi.

“Nikikumbuka tulianza tukiwa wadogo sana na hatukuwahi kutengana. Sasa mimi si yule Valentina wa zamani. Zamani Enzo aliposema twende kutalii sisi wawili tu, nilikataa kuwaacha watoto. Sasa nimebadilika kidogo. Siku hizi naweza kuwaacha hata kwa siku tatu, kisha nawakumbuka. Kitu kimoja muhimu ni kwamba hatugombani, hilo ni jambo la msingi kwetu. Tunajuana sana. Namkubali jinsi alivyo, sitaki kumbadilisha. Tunakamilishana vizuri. Nimemzoea sana Enzo,” alisema Valentina.

Inaelezwa kuwa Valentina alikutana na Enzo akiwa na miaka 16, huku Enzo akiwa na miaka 17, na mapenzi yao yalianza katika eneo la Mar del Tuy, licha ya wote kutoka San Martin, Argentina.

Kwa sasa Valentina ni mshawishi wa chapa kwenye mitandao ya kijamii ambapo ana umaarufu mkubwa akiwa na wafuasi milioni 3.3 Instagram.


Amekuwa akihudhuria mara kwa mara mechi za Enzo akiwa na uzi wa Chelsea na timu ya taifa ya Argentina, na mara nyingi huposti picha akiwa amevaa jezi yenye jina la mumewe.

Kwa miaka mingi, Valentina amekuwepo katika nyakati muhimu za mafanikio ya Enzo, mathalani alikuwepo uwanjani wakati Argentina inatwaa Kombe la Dunia 2022, michuano ambayo ilifanyika nchini Qatar.