Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dokta Pamba Jiji: Uoga wa kupoteza namba unavyoongeza majeruhi

Muktasari:

  • Hofu ya kupoteza nafasi kwa wachezaji wenzao au kuonekana dhaifu mbele ya makocha na mashabiki huwafanya baadhi yao kupuuza ushauri wa kitabibu na kuendelea na mazoezi au mechi wakiwa hawako fiti.

KATIKA ulimwengu wa soka ushindani wa namba na nafasi katika kikosi cha kwanza ni mkubwa kiasi kwamba wachezaji wengi huhisi wanalazimika kuendelea kucheza hata wanapokuwa na majeraha.

Hofu ya kupoteza nafasi kwa wachezaji wenzao au kuonekana dhaifu mbele ya makocha na mashabiki huwafanya baadhi yao kupuuza ushauri wa kitabibu na kuendelea na mazoezi au mechi wakiwa hawako fiti.

Tabia hii ya ‘kukomalia kucheza’ licha ya majeraha huweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya kwa mchezaji, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ukubwa wa jeraha, kuchelewa kupona, au hata kumaliza kabisa maisha ya mchezaji kitaaluma.

Mwanaspoti ilikutana na Dk Dishon Chacha ambaye anaihudumia Pamba Jiji kama Mkuu wa Kitengo cha Afya, ambaye amefichua janga kubwa linalosababisha wachezaji kutopona majeraha kwa wakati.


CHANGAMOTO YA WACHEZAJI

“Nakutana na changamoto nyingi za kiafya, kuna wakati mchezaji anakwambia anaumwa lakini hataki kocha ajue hilo kwa sababu akijua atamuacha na kumpa nafasi mwingine, kitu ambacho mchezaji hakitaki kimtokee, hivyo tuna siri nyingi za wachezaji.

“Kocha anakuuliza huyo vipi unamwambia hajaniambia kama anaumwa, kama ana shida ataniambia, lakini ukweli ni kwamba anajiumiza,” anasema.


CHANZO CHA MAJERAHA

Anasema kuwa chanzo cha majeraha ni wachezaji wenyewe kwa wenyewe, hata kabla ya viwanja na matendo yasiyozuilika.

“Mara zote ushindani unakuwa mkubwa ndani ya timu basi utegemee na majeraha pia yatakuwa mengi, huwezi kukwepa vitu fulani ambavyo wakati mwingine vinatokea.

“Hii inatokea pia kwa sababu ya ushindani wa namba, mtu anapoona katika nafasi yake kuna mchezaji kaongezwa hasa hawa wadogo na anafanya vizuri, basi watafanyiana makusudi ili mmoja akae benchi kwa majeraha.”


MAJERAHA YANAYOJIRUDIA

Anasema kuwa yapo majeraha ya aina nyingi ila kuna makubwa mawili ambayo yanajirudia kila msimu lazima wachezaji wawe nayo.

“Wachezaji ni watu ambao wanaishi na majeraha kwa sababu wengi hawatibiwi wakapona, sana ni enka na magoti haya yanawasumbua sana.

“Ukisema enka unazungumzia chini huku ya mguu, hayo yote yanasabishwa na mazoezi wanayoyafanya, unakuta wengine wanafanya mazoezi magumu wanatonesha majeraha.”


SABABU ZA MAJERAHA

“Viwanja ni sababu namba moja, lakini pia wao wenyewe kwa wenyewe wanavyocheza hivi kwa nguvu kugongana kunakuwa kwingi.

“Lakini hasa ni viwanja na mazoezi ya nguvu sana mpaka mtu anajiumiza katika majeraha yaliyopita. Pia kugongana ambako kunachangiwa na mtu kama amekuzidi nguvu basi lazima akuumize.


ALIFIKAJE PAMBA JIJI?

“Mimi ni mtumishi wa serikali, baada ya hii timu kuletwa katika Halmashauri yetu ya Jiji, ndipo sasa wakachukua watu wa kuwahudumia na miongoni mwao nilikuwa  mimi.

“Kwa hiyo huyu meneja wa timu alikuwa mwalimu kabisa anafundisha akatolewa kule aje kufanya kazi huku, mimi nilikuwa nahudumia wananchi katika Hospitali ya Wilaya ya Jiji la Mwanza, nikatolewa.

“Baada ya kuja huku kuna mafunzo ambayo ni lazima ukayasome kwa ajili ya hawa wachezaji kwa sababu wako tofauti na wagonjwa wa kawaida.

“Shida zao huwa ni maumivu, kugongana wenyewe kwa wenyewe, kwa hiyo ni lazima upewe mafunzo, nilipokuja huku nilipata changamoto kidogo.


BAADA YA MAFUNZO

“Baada ya mafunzo ya kuwatibu wachezaji ndio nilipogundua kuwa madaktari wanaoitwa kwenye hizi timu sio wote wenye huo ujuzi.

“Mimi ni daktari kabisa, sio muhudumu, kwenye michezo wengi sio madaktari na nilipoingia huku, ndio nikafahamu hilo.

“Yani mtu tu alikuwepo kwenye mpira, akawa na timu fulani anapeleka maji kwa wachezaji, hivyo wanamzoea na kumuita daktari na anaenda kupata mafunzo ya afya kidogo, ndio wengi waliopo kwenye timu zetu Tanzania.


TATIZO LIKO HAPA

“Nimefanya utafiti kwa muda mfupi sana nikagundua wachezaji wengi hawaponi kwa haraka majeraha kwa sababu hawatibiwi na madaktari bali wanapata huduma kutoka kwa wahudumu.

“Unaweza kukuta mtu yupo na timu kwa muda mrefu akisaidia kazi za hapa na pale, hivyo wanamuita mchua misuli na unamkuta anaifanya kazi hiyo msimu hadi msimu.

“Mtu kama huyo hawezi kujua mchezaji ana homa au amepata shida ya upumuaji au amepasuka misuli, ila kupaka mafuta tu na hao ndio waliojazana kwenye timu zetu.”


MAJUKUMU NDANI YA PAMBA JIJI

Anasema kuhusu afya za wachezaji huwa anapata taarifa kwa nahodha kwa kuzingatia mambo muhimu ikiwamo mfumo wa chakula na mazingira.

“Kila siku lazima nijue afya za wachezaji kupitia nahodha wao, kuangalia chakula watakachotumia kutokana na mazingira tuliyopo au siku ya mechi.

“Chakula chochote ambacho mmeng’enyo wake unachukua muda mrefu, hakimfai mchezaji anapotakiwa kwenda mazoezini au kwenye mechi, sana wanakula vyakula vya kuupa mwili nguvu.

“Kama siku tuna mechi saa 10 jioni, basi watakula mapema kuanzia saa 5 hadi 6, ili wapate muda wa kupumzika na chakula kijichakate kwa haraka ndani ya saa mbili halafu tunaenda uwanjani.”


MUDA GANI MZURI KUCHEZA

“Sisi tunapenda kuwachezesha kipindi cha jua kali ili waweze kuzoea kucheza wakati wote iwe ni mchana au jioni.

“Mwalimu wao alichagua hivyo na sisi tukaona kuwa haina madhara basi tukakubaliana na ratiba hiyo na inawasaidia, kiukweli wako imara.”


USHIRIKIANO KATI BENCHI LA UFUNDI

“Kwenye timu uko uongozi ambao tunauita benchi la ufundi na hapo kuna kocha na msaidizi wake na wa viungo pia.

“Kwa hiyo huwa nawasiliana sana na kocha wa viungo ambaye ndiye anayejua utimamu wa wachezaji na kama ataona changamoto basi haraka ananifikishia taarifa.

“Huwa naanza kumchunguza kujua kama shida yake ni ya muda mfupi basi haraka naanza kuifanyia kazi, lakini kama ni kubwa tunafuata mchakato wa kwenda hospitali kwa matibabu zaidi.

“Hawa wachezaji tunaosafiri nao ukiwaona hapa ujue wako timamu kabisa, hatuna shaka na tumeshawapanga ila ukisikia mmoja kaumia basi atakuwa kapata shida hapa.


TATHIMINI KWA MSIMU

“Huwa tunafanya tathimini za kiafya hasa kwa mchezaji ambaye anakuwa ni mgeni, tena huwa ni mwanzoni kabisa mwa msimu tunapowasajili tu.

“Lakini tunachofanya ni uchunguzi tu kwa mchezaji ambaye anaonekana kama hayuko sawa, shida moja ni kwamba kumfanyia tathimini mchezaji mmoja ni shilingi laki tatu, hivyo sio pesa ndogo.

“Timu nyingi haziwezi kulipa, ndio maana tunafanya tathimini kwa macho kwamba huyu tulikuwa naye msimu uliopita hivyo yuko sawa.”


LISHE NA PROGRAM MAALUM

“Huwa inabadilika kwa wiki kulingana na siku zinaweza kuwa za mapumziko ambazo zina aina yake ya vyakula na za mechi pia.

“Kila wikiendi wachezaji wanakuwa na mazoezi maalum (Gym) ambapo kila mtu huwa anapata muda wa kufanya kila zoezi analotaka.”


VIFAA VYA KITEKNOLOJIA

“Huwa tunatumia vifaa vya kisasa kuwatibia wachezaji na muda mwingi huwa vinapatikana hospitalini na sio huku katika timu kwani huko ndiko tunawatibia.

“Endapo tutakuwa na shaka na mchezaji huwa tunampeleka hospitali kwani ipo ya Jiji na nyingine ya Rufaa Bugando inayotuunga mkono.


IMANI POTOFU

“Wengi wanaumia unawaambia shida labda ni enka yeye anaamini amechezewa, hivyo kazi yetu ni kuwashauri na kuwashawishi ijapokuwa ni ngumu.

“Unajua suala la imani ni la mtu binafsi kwa hiyo hata ukizungumza naye basi hawezi kukuelewa, kwa sabababu hawana elimu ya afya.


USHAURI

“Timu nyingi hazina madaktari kwa hiyo ingewezekana kila timu iwe nao hata wawili kwa sababu wanachangia mchezaji kuchelewa kupona.

“Wengine wanacheza sana muda mrefu kwa hiyo kuumia ni rahisi hivyo wakiwapo itasaidia kuwafanya wawe sawa.

“Pia wachezaji pia hawajali afya zao wao wenyewe, unakuta wakipata muda wanaendekeza starehe na wanawake, jambo ambalo sio zuri kwao,” anasema.


MCHAKATO WA MATIBABU

“Hapo huwa inategemea na ukubwa wa jeraha, yale madogo muda huohuo mtu anakuwa sawa kabisa, yale makubwa ndio tunampeleka hospitalini.

“Kwa hiyo mengine yanachukua wiki tatu au mwezi kabisa, kutegemeana na maelekezo maalum ambayo Wataalamu watampa na mimi pia.”


MAJERAHA HAYAZUILIKI

“Ni ngumu kwa majeraha kuzuilika ni kitu ambacho hakiepukiki, yani unapozungumzia jeraha huwezi kujua litatokea wakati gani.

“Inaweza kutokea kwa namna nyingi na huwa tunatafuta njia ya kumsaidia tu ili awe sawa pale ambapo majeraha yamepatikana.”


USAIDIZI WA KISAIKOLOJIA

“Lazima tupate muda wa kukaa na wachezaji kwa mwanasaikolojia, ili aweze kuzungumza naye na kusaidia kuelewa kuwa hiki ni kipindi cha muda tu.

“Hii inasaidia sana kumuweka mchezaji sawa, ili atambue kuwa ni maisha ya muda mfupi na atarejea katika hali yake na kurudi kazini.


UKAGUZI WA KIAFYA

“Sisi huwa tunafanya vipimo vya afya mara tatu ndani ya msimu mmoja, pia katikati ya msimu kabla hatujaanza msimu wa pili tunafanya.

“Kama hapa tukibakiza mechi mbili tunaenda kufanya uchunguzi wa kiafya na hapo ndipo tunajua yupi yuko sawa au majeruhi.”