DIARRA: Wala msihofu, tunabeba!

Sunday October 24 2021
Diarra pic
By Mustafa Mtupa

UTAMU wa Ligi Kuu Bara unatokana na ushindani uliopo katika timu 16 zinazoshiriki, huku baadhi zikiwa na ushindani mkubwa ndani ya vikosi.

Ukienda Simba makipa wapo watano, ila ni lazima wawili waingie kikosi cha wachezaji 18 watakaocheza na kukaa benchi, huku wengine wakicheza na jukwaa na pale mitaa ya Jangwani, langoni wapo watatu, ila wawili wanapigania kukaa langoni au benchi.

Msimu uliopita Yanga iliwatema Farouk Shikhalo na Metacha Mnata na kuna makipa watatu - Erick Johora, Ramadhan Kabwili na Djigui Diarra.

Ushindani mkubwa upo kwa Diarra ambaye ni kipa namba moja akifuatiwa na Kabwili huku Johora ambaye ni ingizo jipya akiwa chaguo la tatu.

Miongoni mwa usajili bora Yanga ni wa Diarra, raia wa Mali aliyeonyesha kiwango bora na kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza, huku baadhi wakihitaji muda zaidi kuzoea mazingira.

Katika mechi tatu za Ligi Kuu alizokaa langoni, kipa huyo hajaruhusu bao na kuiwezesha timu yake kukaa kileleni ikiwa na alama tisa na mabao manne, huku kwenye Ngao ya Jamii aliwakatili Simba na kuiwezesha Yanga kuibuka mbabe wa bao 1-0 na kubeba ngao hiyo. Ubora wa Diarra akiwa langoni umewafanya hata mashabiki kumuita kipa anayedaka hadi mishale.

Advertisement

Katika mahojiano na Mwanaspoti, kipa huyo anaelezea mambo mbalimbali ikiwamo alivyotumia pesa zake za kwanza alizopata na kusisitiza kuwa baada ya Ngao ya Jamii, kwa jinsi Yanga ilivyo anaamini wanabeba ubingwa Ligi Kuu Bara msimu huu.


FEDHA ZA KWANZA

Diarra anakumbuka alipoanza kuonja utamu wa soka ni pale alipopata mkwanja mnene. Anasema: “Ilikuwa Kombe la Dunia la Vijana U-20 mwaka 2015 kule New Zealand timu ilimaliza nafasi ya tatu. Ilikuwa ni heshima kubwa kwa taifa na tuliporudi nyumbani tulipokewa kishujaa na serikali ilituzawadia kila mchezaji faranga 23 milioni (takriban Sh93 milioni), kamwe sitasahau. Niliitumia kugawia watu wangu wa karibu na nyingine nilinunua kiwanja na kujenga nyumba ya kukaa.”


KUBADILISHA NAFASI

Kama unadhani Diarra alianza soka akiwa kipa ndio maana amekuwa mtamu, umekosea. Jamaa alianza kucheza kiungo na baadaye kubadilisha na kuwa kipa na hapa anafafanua: “Ni kweli nilianza kiungo, lakini nimekuwa nikipenda nafasi ya kipa kwani ndiye mlinzi wa mwisho, hivyo kilichosababisha nitamani kucheza kiungo ni shauku ya kuwa tegemeo kwenye timu. Pia licha ya kuwa nilicheza nafasi ya kiungo lakini sikujisikia furaha na kutimiza ndoto za kurudi nyuma na kuwa kipa hadi leo. Hizi zilikuwa ndoto zangu za kuwa kipa bora.”


TATIZO LUGHA

Licha ya kufurahia maisha akiwa Tanzania, Diarra anakiri mazingira ya hapa ni furaha kubwa, lakini anakumbana na changamoto kidogo za lugha.

“Lakini nashukuru baadhi ya wachezaji na wafanyakazi wanaelewa ninachozungumza, hivyo nawasiliana nao lakini ni wachache, wengi hawajui,” anasema Diarra anayezungumza Kifaransa tu, lugha inayotumika zaidi nchini Mali.

Juu ya ishu za misosi, Diarra anasema tangu amewasili Tanzania hajawahi kusumbuliwa na suala la chakula kwa sababu anapenda kula ugali - chakula alichodai ni maarufu nchi nyingi za Afrika na bahati nzuri hata hapa unaliwa na anainjoi kwa sababu unapikwa vyema na mboga zinamfanya asijione mgeni na kufurahia maisha. “Napenda sana ugali na kwa bahati hapa upo na unalizwa sana, pia hata upishi wake ni mzuri na unanifanya niwe na amani kabisa,” anasema kipa huyo.


MSHIKAJI WA KANOUTE

Wakati Yanga ikimsajili Diarra, Simba ilimsajili kiungo mkabaji Sadio Kanoute ambaye ni raia mwenzake wa Mali na ukimuuliza kama wanafahamiana anasema: “Namfahamu vizuri, ni mshkaji wangu sana. Tulicheza pamoja Stade Malien. Anapokuwa uwanjani muda mwingi huwezi kuona tabasamu lake, hiyo inatokana na umakini alionao kuhakikisha timu inashinda.”


ANAIONAJE YANGA

Licha ya kucheza timu kubwa Mali, Diarra anasema Yanga pia ni miongoni mwazo kuwahi kuiona Afrika.

“Kuna umoja sana kwenye timu kuanzia viongozi, benchi la ufundi na wachezaji jambo ninaloona kuwa litawezesha kushinda mataji.

“Malengo yangu ni kuhakikisha inashinda kila mechi. Hilo nitafanya kwa kujitolea asilimia mia kwani ndio njia pekee ya kupata ubingwa. Hivyo nawaomba mashabiki wasihofu, tunabeba ubingwa, watuombee tu,” anasema.


KARIAKOO DERBY

Anasema ndoto ya mchezaji yeyote mkubwa ni kucheza mechi kubwa kama ile ya Simba na Yanga, hivyo hata yeye lilikuwa jambo la furaha kutimiza ndoto.

“Kulikuwa na presha kubwa kwa sababu ulikuwa mchezo unaoamua nani atachukua Ngao ya Jamii, lakini sikuwa na jinsi zaidi ya kutuliza akili na kufikiria zaidi kusimama vizuri langoni ili kuisaidia timu na nashukuru tulifanikiwa na sasa tunaiangalia Ligi Kuu.”


MSIKIE FATHER

Kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyeng’ara na timu kadhaa ikiwamo Simba, Plisner na Taifa Stars, Idd Pazi ‘Father’ anasema Diarra ni kipa mzuri na ubora wake upo kwenye kuanzisha mashambulizi na kuzuia vizuri anapobaki na mshambuliaji wa timu pinzani. “Lakini shida ipo kwenye mipira ya kona na krosi. Navyoona umbo lake pia linamuangusha. Timu pinzani ikipata kona mabeki wa Yanga wanatakiwa wawe makini kwani kuna asilimia nyingi za kufungwa. Lakini jamaa yupo vizuri na ataisaidia timu yao,” anasema

Advertisement