Dalali: Simba Day mwakani tunaitaka Barcelona

BAADA ya kuona jana namna mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali alivyovamiwa nyumbani kwake na kufanyiwa fujo, katika sehemu ya mwisho anasimulia jinsi utani wa jadi ulivyobadilika miaka ya karibuni.


UTANI WA JADI
Dalali anashangazwa na chuki zinazoenezwa na vijana wa sasa kugeuza utani wa jadi hadi kufikia hatua ya kutoshirikiana mambo ya msingi, badala yake wamejaa matusi na kejeli.
“Zamani kama kiongozi ama mwanachama wa Yanga kafariki dunia, Simba ndio tulikuwa tunaubeba msiba. Kama kushona sanda, kupika na mambo mbalimbali, vivyo hivyo Yanga walifanya hayo tukikutwa na matatizo. Tunatembeleana kwenye hitma. Tulikuwa tunakwenda klabuni kwao, wanakuja kwetu ila sio sasa,” anasema.
Kwa upande wake anadhani uhasama huo unasababishwa na uhuru wa watu kuposti kitu chochote kwenye mitandao ya kijamii.
“Mfano mzuri mechi ya mzunguko wa pili (msimu uliopita) tuliyofungwa bao 1-0 na Yanga, mzee mwenzangu akaniletea nyumbani mihogo ya kuchemsha miwili, chupa ya chai na vikombe viwili. Tulivyowachapa Kigoma nikampelekea na yeye. Huo ndio utani. Uwe ndani ya dakika 90 baada ya hapo ni ndugu,” anasema.

KATOKA PATUPU SIMBA
Ukimuuliza Dalali kuitumikia kwake Simba amepiga hatua gani ya maisha. Jibu lake ni nyepesi tu tena kwa hekima akisema hakufanya kazi ili anufaike badala yake alitaka kujenga umoja, uimara wa timu na kuwapa raha mashabiki na wanachama.
“Kusema ukweli niliambulia kupigwa mawe, kuuza baadhi ya vitu vyangu ili kuhakikisha wachezaji wanapata haki zinazostahiki. Sasa nimebakia mimi kama mimi,” anasema.
Kuhusu mahala anapoishi kwa sasa, Dalali anasema: “Hapa ni nyumbani kwa mtoto wangu wa kike na ameolewa, nimekimbia kwenye nyumba yangu Magomeni kwa sababu ya mafuriko, pia upande mmoja paa limeondoka.”
Anasema, ni ngumu kuishi kwake mpaka maji yatakapokauka, lakini hata mazingira si rafiki kibinadamu na anasema anapambana kuona anaimarisha mjengo wake, ingawa kiuchumi hali yake ni tete. Hata hivyo mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu anaonyeshwa kushtushwa na taarifa ya Dalali kuwa na hali mbaya na kudai watalifuatilia suala hilo kuona wanamsaidiaje kwani ni mtu muhimu kwao na kiongozi mwenye heshima Msimbazi na wadau wa michezo nchini.


MANARA ANAZUGA
Simba kwa sasa inataniwa katika mitandao ya kijamii ikiitwa Kolo FC - jina lililozalishwa na aliyekuwa msemaji wao, Haji Manara ambaye kwa sasa anaitumikia Yanga. Manara alikaririwa akisema kolo ni mtu mmoja, makolo wawili na wakiwa wengi ni makolokolo, lakini Dalali anasema kwa Kizaramo neno hilo linamaanisha upande wa mama, yaani wajomba.
Mama yake na hata babu yake alikuwa mwana Simba, hivyo kwenda kwake Yanga ni kwa-mba ameenda kwa wajomba.
“Kwa Kizaramo maana yake ni hiyo, ingawa sipendi kuzungumzia kabisa hayo maana sijaona kama yana sababu ya kufanya hayo,” anasema.


NJE YA SOKA
Dalali anasema baba yake alikuwa rafiki wa mwasisi wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na baada ya kumaliza darasa la saba alikwenda kumuombea kazi Tanu.
“Baada ya kufika huko nilijiunga na bendi ya Vijana ilikuwa inaitwa Tanu Youth, nilikuwa napiga (gitaa la) solo na mwalimu wangu alikuwa George Mkuchika, baadaye tukapelekwa mafunzo ya kijeshi miaka miwili mwaka 1969 hadi 1971, sikutaka kufanya kazi hiyo, niliendelea na muziki na mpira,” anasema Dalali.
“Baada ya kufanya vizuri kwenye muziki nakumbuka walikuja viongozi wa Bendi ya Msondo nilikataa kwa sababu akili yangu ilikuwa kwenye mpira.”
Anasema aliipenda sana Simba kiasi kwamba hakutaka kujikita katika muziki. Mwaka 1968 kadi yake ilikuwa namba moja timu ilikuwa ikiitwa Sunderland.
“Baada ya kadi kubadilishwa namba moja ni Mheshimiwa Kawawa (Rashidi sasa marehemu), namba mbili Fredrick Sumaye na ya tatu ni ya kwangu,” anasema.


AMPONGEZA MO DEWJI
Anasema uwekezaji alioufanya Mohamed Dewji ‘Mo’ umeipa Simba hatua kubwa ambayo imeleta matunda katika michuano ya kimataifa.
“Japo wanambeza sio kitu rahisi mtu kutoa pesa nje ya uwekezaji. Alianza kuipenda Simba tangu akiwa mdogo na alikuwa anajitolea sana. Kwa hakika anastahili pongezi kwa kuifanya Simba leo itambe Afrika na kutetemesha vigogo, kwani amewekeza vya kutosha. Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake lazima apewe,” anasema Dalali.


FARAJA LA MASTAA WA ZAMANI
Dalali anasema kuna mastaa wa zamani wa Simba ambao humtafuta mara kwa mara, kumjulia hali na kwenda kumtembelea nyumbani kwake.
“Baadhi yao ambao kila siku napokea simu zao ni Idd Pazi, Julio, Mohamed Mwameja, Juma Kaseja, Ulimboka Mwakingwe yaani ni wengi sana. Nawashukuru kwa kweli,” anasema.


FAMILIA
Dalali aliyekuwa mahiri kwa kucharaza gitaa la solo akiwa Vijana Jazz amebarikiwa kupata watoto watatu ambao ni Yahya, Mushi na Umi. Pia ana wajukuu 27. Familia nzima hakuna anayeipenda Yanga na anasema hapendi kuona linatokea hilo.


USHAURI WAKE
Dalali anawashauri viongozi waliopo Msimbazi akisema: “Viongozi wafungue akaunti ya kujenga uwanja, kisha wachague watu ambao watakuwa wanazunguka na watu wa benki kila mkoa, naamini watapata pesa kwa muda mfupi na wote tutafurahia matunda ya uwanja huo.”
Jambo lingine analowaomba viongozi ni wa kwamba Simba Day ya mwakani walete timu kubwa kutoka barani Ulaya kama Manchester City, Barcelona na nyinginezo kwani anaamini uwezo wanao.
“Mara ya kwanza nilitaka tucheza na Zamalek, lakini ilishindikana kipindi hicho walitaka Sh300 milioni ndio maana tukawaalika SC Villa ya Uganda. Kwa sasa uwekezaji uliopo timu za Ulaya zinaweza kualikwa kushiriki tamasha,” anasema.
Anasema wakati anaanzisha Simba Day alitaka liwe tamasha la kudumu na kwamba anamshukuru aliyekuja nyuma yake, Aden Rage kuliendeleza kwa nguvu ikiwemo kuendeleza mpango wa uwanja na meo wana Simba wanajiandaa kushuhudia tamasha la 13 la klabu yao.