Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dalali, Ahmed Ally hawakufanya uchochezi?

ZENGWE Pict

Muktasari:

  • Kesi hizi zimekuwa zikitupwa, kuishia njiani au washtaki, ambao ni waendesha mashtaka kuamua kuziondoa mahakamani kutokana na sababu za kiufundi.

TANGU nyakati za Uhuru ni nadra sana kwa kesi za tuhuma za uchochezi kumalizika mahakamani hadi hukumu au uamuzi utokee.

Kesi hizi zimekuwa zikitupwa, kuishia njiani au washtaki, ambao ni waendesha mashtaka kuamua kuziondoa mahakamani kutokana na sababu za kiufundi.

Tatizo kubwa la kesi hizi ni tafsiri yenyewe ya mashtaka. Wakati mahakama inataka tafsiri hiyo huomba pia ushahidi kuthibitisha uchochezi huo ulikuwa na ufanisi. Maana yake upande wa mashtaka uweze kuthibitisha bila ya shaka yoyote kuwa maneno yaliyosemwa yalichochea.

Yaani kuwepo na watu ambao watathibitisha kuwa walichochewa na wakashawishika, hivyo kuchukua hatua fulani, ama kuanza kupanga utekelezaji wa jambo hilo au kushiriki kulitekeleza. Kwa mujibu wa wanasheria, jambo hilo ndilo limekuwa likikwamisha kesi nyingi za uchochezi.

ZENG 01

Lakini hii imekuwa tofauti kwa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambayo ishawatia hatiani wanafamilia kadhaa kwa kosa hilo la uchochezi, wakati baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ni wanasheria na mawakili wanaoelewa fika kuwa marejeo ya kesi za uchochezi yanataka uwepo ushahidi wa waliochochewa kushawishika na kuchukua hatua.

Mtu wa mwisho kuhukumiwa kwa kosa hilo alikuwa ofisa habari wa klabu ya Yanga, Ali Kamwe. Kamati ilisema Kamwe alikutwa na hatia ya kosa la uchochezi baada ya kuandika katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram akizungumzia mjadala uliokuwa unaendelea redioni kuhusu uamuzi mbovu na kuitaka mamlaka kufanya uchunguzi.

Ni shida kuliona kosa la uchochezi katika mashtaka yake na iwapo kamati ingefuata mchakato wa kutaka ushahidi wa walioshawishika, ingekuwa ngumu zaidi kuthibitika kwa kuwa hakuna aliyehamasika na kuchukua uamuzi wa kuwashughulikia waamuzi eti kwa kushawishiwa na Kamwe.

ZENG 02

Lakini kuna kosa la dhahiri lililojitokeza wiki mbili zilizopita. Wakati Simba ikielekea kucheza mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco kulitolewa maneno ya uchochezi yaliyokuwa na ufanisi.

Katika kikao cha kuelekea mchezo huo ulioisha kwa sare ya bao 1-1, wazee wa Simba na hasa Mwenyekiti wa zamani, Hassan Dalali walitoa maneno makali kwa watu ambao walidhani wangeihujumu timu hiyo isitwae ubingwa.

Alizungumza maneno ambayo katika hali ya kawaida unaweza kutafsiri kwamba wana-Simba wawe tayari hata kutoa roho ya mtu atakayeonekana anajaribu kuihujumu Simba. Maneno yake yalidakwa na msemaji wa klabu hiyo, Ahmed Ally ambaye aliyarudia mara kadhaa.

Kosa la uchochezi huthibitishwa na hatua zinazochukuliwa na waliochochewa. Siku ya mechi hiyo, mashabiki wa Simba walishajenga chuki dhidi ya mashabiki wa Yanga na hivyo wakawa wakali.

ZENG 03

Wapo mashabiki wa Yanga waliopigwa, kuchaniwa nguo na hata kufukuzwa majukwaani kwa kile walichodhaniwa kuwa wameenda uwanjani kuipa nguvu RS Berkane na kuihujumu timu ya hapa nyumbani.

Huu ni mfano ambao mwanasheria yeyote atathibitisha kuwa kuna kosa la uchochezi lililothibitishwa na ushahidi mzito wa mashabiki kuwapiga, kuwazuia kuingia uwanjani, kuwaondoa jukwaani na hata kuwachania fulana zao za rangi ya njano.

Lakini hadi leo si Sekretarieti wala Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili aliyeagizwa wawili hao, yaani Mzee Dalali na Ahmed waitwe mbele ya kamati yake kujibu tuhuma za uchochezi.

Ilikuwaje yule ambaye maneno yake hayakuweza hata kumhamasisha shabiki mmoja achukue hatua dhidi ya waamuzi wanaochezesha vibaya na makossa yao kuonekana yanainufaisha timu moja, akaharakishwa kupelekwa maadili, tena kwa maagizo ya mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, lakini hao ambao maneno yao yamehamasisha watu kufanya vurugu, bado wameachwa huru?

ZENG 04

Mambo mengine ndio yanasababisha uongozi wa TFF uonekane kweli umepania kuwaadhibu watu fulani fulani tu na kuwaacha wengine wenye makossa kama hayo. Ukiona Yanga wanahesabu kuwa maofisa habari wao watano wamefikishwa mbele ya Kamati ya Maadili na kupatikana na makossa, lakini upande mwingine huwa hawaonekani na makosa, ujue wametunza kumbukumbu kama hizo.

Kwa kawaida kosa kama hilo, si tu linashughulikiwa na vyombo vya haki vya TFF, bali hata Jeshi la Polisi ambalo jukumu lake kubwa ni kulinda watu na mali zao.

Ni dhahiri kilichotokea Uwanja wa Amaan siku ya fainali ya Kombe la Shirikisho ni aibu kwa taifa na tulitegemea TFF ingekuwa imeshachukua hatua kuwawajibisha, lakini ukimya huu wa TFF unaendelea kutia shaka kuhusu uadilifu wa viongozi wa juu na kamati zake.

Hakujatokea hata tamko la kuzungumzia tukio lile lililotokea mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dk Patrice Motsepe na viongozi wengine mashuhuri walioalikwa kuhudhuria fainali ile.

Yote hayo yanatokea wakati tunaelekea kuandaa fainali za ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) Agosti, huku tukiwa na haki nyingine ya kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2027.

ZENG 05

Wakati kashfa ya rushwa ikitokea Ujerumani mwaka 2005, nchi hiyo ilikuwa inajiandaa kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2006. Ilibidi mamlaka zichukue hatua za haraka kushughulikia suala hilo ili isifikie hatua ya kuporwa haki hiyo.

Hatusubiri CHAN na Afcon ili kuona mechi na wala serikali haikuweka nguvu kwa ajili ya kuandaa mechi pekee, bali kuhakikisha ujio wa matukio hayo makubwa unatusaidia kutengeneza soka letu katika nyanja mbalimbali.

Nyanja hizo ni kama huo mfumo wa kushughulikia masuala ambayo ni hatari kwa mchezo wa mpira wa miguu, kuboresha viwango vya waamuzi, kuboresha programu zetu za maendeleo, kama vile soka la watoto, vijana na wanawake na kuboresha miundombinu.

Kama tunaelekea kuandaa CHAN na Afcon tukiwa na mifumo mibovu, basi hatujajua tunayataka matukio hayo kwa ajili gani.

Ni lazima TFF ione kuna busara kushughulikia uvunjwaji wa maadili bila ya kuonea aibu au kupendelea upande mmoja. Kama haiwezi kuwahukumu kwa adhabu hizo walizopewa wengine, basi angalau mchakato wa mashtaka ufanyike waonekane hawana mashtaka. Hapo angalau mtakuwa mmetudanganya. Lakini kwa kuwa matukio ni mengi, ni ngumu kudanganya mfululizo.