Dakika hatari za Rivers United

SAFARI ya matumaini kwa mabingwa wa soka wa kihistoria nchini, Yanga, upande wa kimataifa msimu ujao inatarajiwa kuanza wikiendi hii kwa mchezo wa raundi ya kwanza kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ambapo watawakaribisha Rivers United kutoka Nigeria.

Tofauti na Simba ambao wataanzia raundi ya pili, Yanga wana kibarua kizito cha kuhakikisha wanawang’oa Wanaigeria ili kutinga raundi ya pili ambayo itatoa timu 16 kati ya 34 ambazo zitatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi akiwa bize na kikosi chake kwa ajili ya maandalizi kukabiliana na Wanageria, Mwanaspoti linakuchambulia dakika ambazo Rivers United wamekuwa wakifungika na zile ambazo wamekuwa hatari kwa kuangalia takwimu.

Kabla ya kuichambua Rivers United si vibaya kama tutaanza kwa kuifahamu kuwa ni klabu changa nchini Nigeria ambayo ilianzishwa 2016 katika Mji wa Port Harcourt baada ya serikali ya Jimbo la Rivers kutoa ruhusa kwa klabu za Dolphins FC na Sharks FC kuungana.

Timu zote mbili ziliendeshwa na serikali hiyo na zilikuwa na matatizo ya kifedha na ndio maana ilikuwa rahisi baada ya kipindi fulani kuungana na kuundwa klabu moja ambayo ni Rivers United iliyogeuka kuwa tishio kwenye soka la nchi hiyo.


DAKIKA WANAZOFUNGIKA

Kwa mujibu wa takwimu za wapinzani hao wa Yanga katika michezo yao 10 iliyopita kwenye Ligi Kuu ya Nigeria (NPFL), wameruhusu nyavu zao kuguswa mara 12. Hiyo ina maana kwamba walikuwa na wastani wa kuruhusu bao kila mchezo.

Kati ya mabao 12 ambayo wameruhusu kwenye michezo 10 ya mwishoni mwa msimu uliopita, Rivers United ambao ukuta wao hauna mabadiliko yoyote tangu msimu wa Ligi Kuu nchini humo ulipomalizika ni mabao manane waliyofungwa kipindi cha pili.

Hiyo ina maana kwamba Rivers United wanaweza kufungika hasa kipindi cha pili kuanzia dakika ya 45 hadi 60 na 76 hadi 90.

Kama Yanga wakijipanga vyema wanaweza kutumia udhaifu huo kujihakikishia nafasi ya kutinga raundi ya kwanza wakiwa nyumbani.

Kati ya mabao manane ambayo Rivers United wamefungwa kipindi cha pili, manne ni kuanzia dakika ya 45 hadi 60 huku matatu yakiwa dakika za 76 hadi 90. Ni bao moja tu ambalo wamefungwa katikati ya kipindi hicho cha pili ambapo ni kati ya dakika ya 61 hadi 75.


DAKIKA ZA HATARI

Licha ya ukuta wa Rivers United kuwa na wastani wa kuruhusu bao kwenye kila mchezo katika michezo 10 iliyopita, wanaonekana kuwa na safu imara ya ushambuliaji, hivyo Yanga wakati wanasaka ushindi wanapaswa kuwa makini ili kuwadhibiti Martins Usule na wenzake.

Ukuta wa Yanga haupaswi kujiamini kupita kiasi maana safu ya ushambuliaji ya Rivers United imepachika mabao 16 kwenye michezo 10 iliyopita na wachezaji wao kadhaa walikuwa kwenye orodha ya nyota ambao walikuwa wakiwania kiatu cha ufungaji bora cha NPFL msimu wa 2020/21.

Rivers United wanaonekana kuwa hatari zaidi kipindi cha kwanza kwani kwenye mabao 16 waliyofunga, mabao 10 kati ya hayo wametupia kipindi cha kwanza, manne kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo hadi 15 na mawili dakika ya 16 hadi 30.

Takwimu hizo zinaonyesha kwamba kuanzia dakika ya 31 hadi 45 wametupia tena mabao manne kama ilivyokuwa kuanzia dakika ya kwanza hadi 15.


JEMBE LIMEONDOKA

Miongoni mwa wachezaji muhimu wa Rivers United msimu uliopita alikuwa ni pamoja na Godwin Aguda ambaye amejiunga na Falkenberg ya Sweden.

Aguda aliifungia Rivers United mabao tisa sawa na Usule. Hao ndio waliokuwa vinara wa mabao kwa timu hiyo, hivyo kuondoka kwa nyota huyo kunaweza kuwa pigo kwa Wanaigeria hao na faida kwa Yanga ambayo inajivua kurejea kwa straika Heritier Makambo.


WALIOBAKI BALAA

Licha ya kuondoka kwa Aguda, Rivers United ina nyota wengine ambao wanaweza kufanya mambo makubwa wakiwa na kikosi hicho akiwemo Usule.

Mbali na Usule, nyota wengine ambao walikiwasha msimu uliopita ni pamoja na Malachi Ohawuma aliyetupia mabao saba, Nelson Esor na Shedrack Oghali kila mmoja alitupia mabao sita. Nyota hao wamebeba matumani ya chama hilo kuvuka hatua hii.