Cristiano Ronaldo na oparesheni 1,000
Muktasari:
- Gwiji huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 40 kwa sasa amefikisha mabao 956 baada ya kufunga mara mbili akiwa na kikosi cha Al-Nassr wikiendi iliyopita.
RIYADH, SAUDI ARABIA: HII inaitwa oparesheni 1,000. Ndicho unachoweza kusema kutokana na mpango wa supastaa wa soka duniani, Cristiano Ronaldo kutaka kurudi Ulaya ili tu kuja kutimiza ndoto zake za kufikisha mabao 1,000 katika maisha yake ya soka.
Gwiji huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 40 kwa sasa amefikisha mabao 956 baada ya kufunga mara mbili akiwa na kikosi cha Al-Nassr wikiendi iliyopita.
Lakini, sasa swali lililopo ni muda kiasi gani umebaki kumshuhudia Ronaldo akiendelea kutamba ndani ya uwanja. Fowadi huyo veterani ameshaweka bayana kwamba fainali zijazo za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico majira ya kiangazi yajayo zitakuwa za mwisho kwake kuitumikia timu ya taifa ya Ureno.
Mkataba wa Ronaldo wenye thamani ya Pauni 492 milioni kwenye klabu hiyo ya Saudi Arabia utafikia tamati mwaka mmoja baadaye baada ya kukamilika kwa fainali za Kombe la Dunia.
Lakini, anataka kuendelea kucheza kutokana na mpango wake wa kutaka kufunga mabao zaidi na zaidi, akisema: “Haijalishi nitakuwa wapi.”
Ronaldo alishakuwa na wakati mzuri na mafanikio makubwa kwenye soka la Ulaya, akitumikia Manchester United kwa vipindi viwili tofauti, kisha Real Madrid kwa miaka tisa na alikuwamo pia kwenye kikosi cha miamba ya soka ya Italia, Juventus.
Kama atarudi kwenye Bara la Ulaya, basi bila ya shaka hilo litaibua mshtuko mkubwa kutokana na umri wake huku huu ukiwa ni msimu wake wa nne tangu alipotoka Ulaya kwenda Al-Nassr.
Wakati wake kwenye soka la Saudi Arabia umemfanya Ronaldo anyakue tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashariki ya Kati, katika sherehe zilizofanyika Dubai, Jumapili.
Lakini, kumekuwa na maelezo kwamba anaweza kuondoka kwenye ligi hiyo muda wowote. Timu nyingine ya Ulaya aliyowahi kuchezea ni Sporting Lisbon na hivi karibuni amesema: “Dhamira yangu ipo wazi na nataka kuendelea kucheza. Haijalishi ni wapi, kama ni Mashariki ya Kati au Ulaya. Nafurahia kucheza soka na nataka kuendelea kufanya hivyo. Nitafikisha mabao 1,000 kwa hakika, kama sitasumbuliwa na majeraha.”
Ronaldo ameonekana kujiimarisha huko Saudi Arabia, ambako hivi karibuni alitumia mkwanja mrefu kununua majumba mawili ya kifahari kwenye kisiwa kimoja ambacho kufika huko usafiri wake ni boti au ndege za majini. Na sasa staa huyo mshindi wa tuzo za Ballon d’Or mara tano na mpenzi wake, mrembo Georgina Rodriguez sasa watakuwa na nafasi ya kwenda kufurahia mapumziko wakati wa likizo kwenye kisiwa hicho cha Bahari Nyekundu kinachoitwa Nujuma.
Kisiwa hicho kipo umbali wa maili 800 kutoka mji mkuu wa Riyadh, mahali ambako Ronaldo anaishi kwa sasa kutokana na kuitumikia timu ya Al-Nassr. Nyumba hizo mbili amezinunua kwa Pauni 7 milioni, ambazo ni zaidi ya Sh 23,334,780,000 za Kitanzania.