Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cristiano atuache kidogo asituvuruge mara mbili

RONALDO Pict


POLE kwa Watanzania wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki wakati wa maandamano yaliyofanyika wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania. Pole kwa Watanzania wengine ikiwemo mimi ambao mioyo yao inevuja damu kufutia kile kilichotokea.


Na tulipojaribu kurudi katika maisha yetu ya kawaida sisi watu wa soka, rafiki yetu Cristiano Ronaldo ‘CR7’ akaitwa na rafiki yake mwandishi nguli, Piers Morgan, kwa ajili ya kwenda kufanya mahojiano mazuri ambayo wamekuwa wakiyafanya mara chache, lakini yanaacha mijadala mbalimbali ambayo inazua mzozo katika jamii.


Ronaldo na Morgan ni marafiki wazuri tu. Na nadhani Morgan kwa sababu naye pia ni staa katika kundi la waandishi basi anaweza kuwa mmoja kati ya waandishi wachache sana ambao wana namba ya simu ya Ronaldo na wanaweza kumuita kwa ajili ya mahojiano binafsi. Morgan pia ni shabiki mkubwa wa Ronaldo nje ya masuala ya kazi.

RONA 01

Mara ya mwisho Ronaldo kufanya mahojiano na Morgan alizusha mzozo mkubwa klabuni kwake Manchester United. Akaishambulia timu yake kwa mengi, akielezea namna ilivyokuwa na miundombinu chakavu pamoja na mambo mengine ambayo yalitushtua wengi kwa sababu Ronaldo ni kipenzi cha mashabiki wa Manchester United na walitegemea awafichie siri zao.

Akamshambulia pia kocha wake wa wakati huo, Erik Ten Hag ambaye alikuwa na uthubutu wa kumuweka benchi Ronaldo au kumtoa nje ya uwanja na kumuingiza mchezaji mwingine.

Ukweli alichafua hali ya hewa katika namna ambayo haikuthimilika. Haikuchukua muda mkataba wake ukavunjwa akatokomea zake Saudi Arabia ambako anacheza kwa sasa.

RONA 02

Na juzi Ronaldo amejaribu kutuchezea akili zetu wakati alipomwambia Morgan kwamba ni rahisi kufunga mabao Hispania kuliko kufunga mabao katika Ligi Kuu Saudia.

Nimesoma mahala hata mashabiki wake wakilalamika kwamba wakati mwingine inakuwa ngumu kumtetea Ronaldo katika kila jambo. Iweje iwe ngumu kufunga mabao Saudia. Kwa ligi ipi hasa?

Ukiniuliza kuhusu ligi mbili ngumu duniani nitakwambia kwamba ni England na Hispania. Watu wanashindana hasa kuliko Ujerumani na Ufaransa. Pale Ufaransa una uhakika wa asilimia 90 kwamba bingwa atakuwa PSG.

Pale Ujerumani una uhakika wa asilimia 90 kwamba mwishoni mwa msimu bingwa ataenda kuwa Bayern Munich. Inatokea nadra sana timu kama Bayer Leverkusen ilivyoingilia kati.

RONA 03

Inawezekana Ronaldo alikuwa anasema hisia za kweli kwa sababu hakubali kwamba mwili wake umechoka. Hakubali ukweli kwamba wakati anacheza Hispania akiwa na jezi nyeupe za Real Madrid alikuwa katika kilele cha ubora wake kimwili na kiakili.

Ni katika kipindi hicho ndipo alipokuwa anakimbizana vilivyo na hasimu wake mkuu kutoka upande wa Catalunya, Lionel Messi.

Ndani ya msimu mmoja Ronaldo angeweza kufunga mabao hata 50. Messi naye angeweza kufunga idadi kama hiyo. Leo sio kwamba ni rahisi kufunga mabao Hispania kuliko Saudia Arabia, hapana ni kwa sababu mwili wake umechoka.

Ronaldo wa Madrid angekuwa anacheza Saudia Arabia sasa hivi angeweza kufunga mabao hata 80 ndani ya msimu mmoja.

Ronaldo wa Manchester United angeweza kufunga hata mabao 90 kama angekuwa Saudia kwa sasa.

RONA 04

Yule Ronaldo ambaye alikuwa anapiga chenga za baiskeli kwa kasi ya ajabu kiasi kwamba kina Ashley Cole walijikuta wanakaa chini kabla hata hajaugusa mpira. Ronaldo wa leo anajiona ni kama yule tu.

Tatizo lake anauchukua mwili wake huu huu wa sasa anadhani ni mwili uleule aliouacha Hispania. Kwamba kwanini kule alikuwa anafunga mabao mengi kule na huku anafunga mabao machache? Tatizo sio ligi zenyewe. Tatizo ni mwili wake mwenyewe.

Ligi ya Saudia ina wachezaji wengi ambao walichoka Ulaya wakakimbilia huko. Ina kundi kubwa pia la wachezaji wengi wa nyumbani ambao hawajacheza soka katika kiwango cha juu. Hawajawahi kwenda hata Ulaya. Inakuwaje ligi ngumu kuliko ligi za Ulaya? Na ligi zenyewe za Ulaya sio zile za kawaida bali ni Ligi Kuu Hispania.

Kwamba ligi yenye Barcelona, Real Madrid, Atletico Madrid, Athletic Bilbao, Villareal, Real Mallorca na nyinginezo inaweza kuwa ligi nyepesi kuliko ligi yenye timu za Al Nassr, Al-Hilal, Al Najima, Al Kholood na nyinginezo? Ronaldo anajaribu kumdanganya nani?

RONA 05

Nadhani anajaribu tu kutujengea mazingira tuone kwamba Ronaldo ni yule yule.

Kwamba Ronaldo anataka tuamini Ligi Kuu Saudia Arabia inaweza kutoa Mwanasoka Bora wa Dunia kama yeye na Messi walivyoweza kuwa wanasoka bora wa dunia mara nyingi kupitia Ligi Kuu Hispania? Ni ukweli ambao hauwezi kuingia katika akili hata ya mtoto mdogo.

Ukweli ni kwamba yeye na hasimu wake wameisha. Yeye na Messi wameisha. Hata Messi hawezi kuja hadharani kutudanganya kwamba Ligi Kuu Marekani ni ngumu kuliko Ligi Kuu Ubelgiji.

Tutambishia. Afadhali Messi ameamua kukaa zake kimya, lakini Ronaldo anataka kutuvuruga kidogo watu ambao tumeshavurugwa na matukio yaliyopita hivi karibuni hapa nchini.

Na Ronaldo ameendelea pia kujiona bora kwa sababu kila mechi lazima acheze kule Saudia. Yeye ndiye mchezaji mwenye mvuto zaidi na mashabiki wanajaa uwanjani kwa ajili ya kumtazama.

Ni mchezaji wa kibiashara zaidi na si ajabu ana kipengele cha mkataba ambacho kinamruhusu kucheza kila mechi. Haimaanishi kwamba anakuwa mchezaji bora uwanjani lakini yeye ni sura ya ligi nzima ya Saudia.

Kule Ureno pia anacheza kwa sababu kocha Robert Martinez hataki kumuudhi mchezaji anayeheshimiwa zaidi Ureno kwa sasa.

Ronaldo huwa anafunga kule Ureno sio kwa sababu ni bora sana, lakini ukweli ni kwamba amezungukwa na kizazi fulani cha Ureno ambacho kina wachezaji wakali na wengine huwa wanakaa benchi pia kwa sababu yake.

Amezungukwa na kina Joao Neves, Vitinha, Raphael Leao, Bruno Fernandes, Bernardo Silva, Nuno Mendes, Neto na wengineo wengi.

Unapocheza na San Marino ni rahisi kufunga mabao mengi ambayo yanakujenga tamaa kwamba unaweza kutwaa Kombe la Dunia pale Marekani, Canada na Mexico ifikapo Juni mwakani. Sio kitu cha ukweli.

Namuelewa Ronaldo ni mchezaji mshindani ndani na nje ya uwanja. Hata nje ya uwanja amekuwa akitoa kauli za kwamba ni yeye ni mchezaji bora zaidi kuwahi kucheza soka akimaanisha kuliko kina Pele, Diego Maradona, Johan Cruffy, Messi na wengineo.

Hauwezi kumbishia katika mtazamo wake wa namna anavyojiona mwenyewe, lakini hili la kupima Ligi Kuu Hispania na Ligi Kuu Saudia hawezi kutudanganya tukamuacha hivi hivi.