Ronaldo: Man United kwa Amorim msitegemee miujiza
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 40, alijiunga na Al-Nassr muda mfupi baada ya kumaliza kipindi chake cha pili na Manchester United mnamo Novemba 2022.
MANCHESTER, ENGLAND: Cristiano Ronaldo amesema kwamba meneja wa Manchester United, Ruben Amorim, hawezi kufanya miujiza na kwamba klabu hiyo haipo kwenye njia sahihi.
Mshambuliaji huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 40, alijiunga na Al-Nassr muda mfupi baada ya kumaliza kipindi chake cha pili na Manchester United mnamo Novemba 2022.
Amorim, ambaye aliwahi kuwa mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Ureno, alichukua nafasi ya Erik ten Hag kama kocha mkuu mnamo Novemba 2024. United ilimaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya 15 kwenye Ligi Kuu, nafasi yao mbaya zaidi tangu washuke daraja mwaka 1973–1974.
Kikosi hicho cha Amorim kilikuwa nafasi ya 14 baada ya kupoteza michezo mitatu kati ya sita ya kwanza msimu huu, lakini sasa kiko nafasi ya nane baada ya kupata pointi 10 kati ya 12 zilizopita.
“Anajitahidi kadiri ya uwezo wake,” Ronaldo amesema katika mahojiano na Piers Morgan.
“Utafanya nini? Miujiza? Miujiza haiwezekani. Tunasema kule Ureno, ‘miujiza ipo Fatima pekee,’ na yeye hawezi kufanya miujiza.”
Kampuni ya Ineos Group ya Sir Jim Ratcliffe ilichukua usimamizi wa shughuli za soka baada ya kununua hisa asilimia 27.7 katika klabu ya Manchester United mnamo Februari 2024.
Tangu Amorim afike, United imetumia takribani pauni milioni 250 kusajili wachezaji wapya, na ingawa Ronaldo anasema wana wachezaji wazuri, anahisi baadhi yao hawajui maana halisi ya kuwa Manchester United.
“Manchester United bado ipo moyoni mwangu,” ameongeza mshindi huyo wa Ballon d’Or mara tano, aliyeshinda mataji saba makubwa na klabu hiyo kati ya 2003 na 2009.
“Ninaipenda klabu hiyo. Lakini tunapaswa kuwa wa kweli na tujiangalie na kusema, ‘sikiliza, hawapo kwenye njia sahihi.’
“Kwa hiyo wanapaswa kubadilika, na si suala la kocha au wachezaji pekee, kwa maoni yangu.”
Mkataba wa Ronaldo na United ulivunjwa baada ya mahojiano na Morgan mnamo Novemba 2022, ambapo alisema alihisi kusalitiwa na klabu na kwamba alikuwa analazimishwa kuondoka.
Pia alimkosoa Erik ten Hag, akisema hakumheshimu, na mnamo Septemba 2024 alisisitiza kuwa United wanapaswa kujenga upya kila kitu.
Ronaldo alisaini mkataba mpya msimu uliopita na Al-Nassr unaoisha mwaka 2027, na anatarajiwa kuichezea Ureno kwenye Kombe la Dunia 2026.
Alipoulizwa na Morgan lini atastaafu, Ronaldo amejibu: “Hivi karibuni. Lakini nadhani nitakuwa nimejiandaa.
“Itakuwa ngumu, bila shaka. Lakini Piers, nimekuwa nikiandaa maisha yangu ya baadaye tangu nikiwa na miaka 25, 26, 27. Kwa hiyo naamini nitaweza kukabiliana na shinikizo hilo.”