Huyu Haaland hata Ronaldo chamtoto
Muktasari:
- Straika huyo wa Norway alifunga bao lake la 18 la msimu katika ushindi huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya timu yake ya zamani. Man City ilishinda 4-1 uwanjani Etihad.
MANCHESTER, ENGLAND: STRAIKA, Erling Haaland ameandika historia ya kibabe kabisa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo hata supastaa Cristiano Ronaldo hakuwahi kuifikia baada ya kufunga dhidi ya Borussia Dortmund katika mchezo wa michuano hiyo uliofanyika usiku wa Jumatano.
Straika huyo wa Norway alifunga bao lake la 18 la msimu katika ushindi huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya timu yake ya zamani. Man City ilishinda 4-1 uwanjani Etihad.
Bao alilofunga ina maana amefunga katika mechi zote tano zilizopita za Ligi ya Mabingwa Ulaya alizocheza akiwa na kikosi cha Man City.
Rekodi yake hiyo ilianzia msimu uliopita kwenye mabao yake mawili aliyofunga dhidi ya Real Madrid kwenye mechi ya mkondo wa kwanza wa hatua ya mtoano. Hakucheza mechi ya marudiano, lakini aliendeleza moto wake wa kufunga kwenye msimu huu.
Alifunga dhidi ya Napoli, kabla ya kuwapiga mbili Monaco na kisha alifunga pia kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Villarreal, kabla ya kukabiliana na Dortmund.
Na Man City si klabu ya kwanza kwa straika huyo mtambo wa mabao kufikia mafanikio hayo. Haaland alifunga pia kwenye mechi tano mfululizo za Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati alipokuwa Dortmund na Red Bull Salzburg. Na jambo hilo linamfanya Haaland kuwa mchezaji wa kwanza kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kufunga kwenye mechi tano mfululizo au zaidi akiwa na timu nyingi tofauti.
Na sasa, jambo hilo linamfanya fowadi huyo kufikisha mabao 54 katika mechi 52 tu alizocheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo kushika namba 10 kwenye orodha ya vinara wa muda wote wa mabao.
Na sasa yuko nyuma kwa mabao matatu tu dhidi ya gwiji Thomas Muller.
Hata hivyo, Haaland bado ana safari ndefu kabla ya kumfikia kinara wa muda wote wa mabao kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ronaldo mwenye mabao 141.
Supastaa Lionel Messi anashika namba mbili kwenye orodha hiyo akiwa amefunga mabao 129.