Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chonde chonde Serengeti Boys, Ngorongoro Heroes msituangushe

Muktasari:

  • Timu hiyo ikiwa kwenye fainali za Vijana U-17 kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) yanayofanyika nchini Burundi, ilikata tiketi ya kucheza fainali kwa kuifunga Kenya kwa mabao 2-1 katika mechi ya nusu fainali ya michuano hiyo.

SERENGETI Boys, timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, imekifanya kile ambacho mashabiki wa soka nchini walikuwa wanakisubiri kwa hamu kubwa.

Timu hiyo ikiwa kwenye fainali za Vijana U-17 kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) yanayofanyika nchini Burundi, ilikata tiketi ya kucheza fainali kwa kuifunga Kenya kwa mabao 2-1 katika mechi ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Serengeti Boys keshokutwa Jumapili itashuka tena uwanjani kuvaana na Somalia waliofanya maajabu katika fainali hizo kwa kuwavua ubingwa na kuing’oa michuanoni waliokuwa watetezi wa taji hilo, timu ya taifa ya Uganda.

Mafanikio hayo ya Serengeti Boys yamekuja siku chache baada ya kaka zao za Ngorongoro Heroes ambayo ni timu ya taifa ya Vijana U20 kufuzu raundi ya pili ya michuano ya kuwania ushiriki wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa nyota wa umri huo.

Ngorongoro ilifanya kweli ugenini kwa kuwang’oa wenyeji wao DR Congo kwa mikwaju ya penalti 6-5 baada ya suluhu ndani ya michezo yao miwili na vtimu hiyo kusonga mbele na sasa inajiandaa kuvaana na Mali mwezi ujao katika raundi ya pili.

Kama Ngorongoro itapenya mbele ya Mali itakabiliana na mshindi kati ya Uganda ama Cameroon katika raundi ya tatu na iwapo itafanya kweli tena basi itakuwa imepata tiketi ya kwenda Niger katika fainali zitakazofanyika mwakani.

Kwa hakika kilichofanywa na timu zetu za vijana na hasa Serengeti nchini Burundi ni vitu vya kupongezwa na kutoa picha namna gani tumeanza kurejesha heshima katika soka la kimataifa kuanzia ngazi za chini.

Miaka mingi iliyopita timu zetu za taifa zimekuwa kama kichwa cha mwendawazimu kwa kupata matokeo mabaya ikiwamo kutolewa mapema katika kila michuano ya kimataifa inayoshiriki.

Lakini kwa miaka ya karibuni, angalau sasa mashabiki wamekuwa wakipata kile roho inachokitaka kwa timu zetu za vijana, kwani ni mwaka jana tu Serengeti Boys ilifuzu fainali za Afrika zilizofanyika Gabon.

Kama sio kuteleza katika mechi yao ya mwisho ya makundi, ingeweza kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo na kutinga moja kwa moja katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini India.

Mwanaspoti tunaungana na wadau wengine wa soka kuzipongeza timu zetu za vijana kwa mafanikio iliyopata, lakini tukiwasisitizia wakaze uzi zaidi ili kuhakikisha zinawapa Watanzania furaha zaidi kwa kunyakua taji la Cecafa kwa Serengeti na kukata tiketi ya kwenda Niger kwa Ngorongoro.

Tunaamini vijana wetu chini ya makocha wao Ammy Ninje na Oscar Milambo watajipanga kwa mechi zao zijazo dhidi ya Somalia kwa timu ya U-17 na Mali kwa ile ya U-20, kwani tayari wameshakula ng’ombe mzima, hatudhani mkia utawashinda.

Kitu muhimu wachezaji wa timu hizo wasibweteke na mafanikio waliofikia mpaka sasa kwa kutambua kuwa kuna kazi kubwa mbele yao, hivyo wajibu wao kupambana hadi dakika za mwisho ili kufika kule ambako kila shabiki anakutamani.

Watanzania wanaopenda soka wangependa kuona Serengeti Boy inarudi na taji la Cecafa na pia kuiona Ngorongoro Heroes ikienda katika fainali za Afrika za U-20 kama ilivyokuwa U-17 mwaka jana Gabon.

Hakuna kisichowezekana, maadamu tumeshayavulia maji nguo, sharti ni kuyaoga na vijana wetu wanaonekana ni askari walio tayari kuipigania nchi.

Tushirikiane pamoja kwa kuziunga mkono kwa hali na mali na kuziombea dua njema ili zipate matokeo mazuri kwa mechi zilizopo mbele yao, Serengeti Boys imalize kazi kwa kuicharaza Somalia nchini Burundi na Ngorongoro iwanyooshe Mali nje ndani kabla ya kusubiri kujua itacheza na nani kati ya Uganda na Cameroon na kufanya kweli.

Mashujaa wetu hao, lazima wajue kuwa Watanzania hasa mashabiki wa soka wamechoka kuona timu zetu zinakuwa wasindikizaji katika michuano ya kimataifa kwani ahadi ya mafanikio na hazina kubwa ya vipaji tulivyonavyo nchini ni jambo linalowapa matumaini makubwa kwa kuamini timu zetu hazipaswi kuishia njiani tu, hivyo chonde chonde timu zetu za Serengeti Boys na Ngorongoro Heroes msituangushe.

Tunaziombea kila la heri timu zetu hizo ili zipate matokeo mazuri Jumapili dhidi ya Somalia kwa timu yetu ya Serengeti Boys na baadaye Ngorongoro ipate ushindi mbele ya Mali katika mechi ya kwanza Mei 13 kabla ya kwenda kumaliza kazi ugenini wiki moja baadaye.