Prime
Camara, Ahoua waibeba Simba Caf

Muktasari:
- Simba imetinga robo fainali ikiwa kinara wa kundi A baada ya kukusanya pointi 13, ikifuatiwa na CS Constantine ya Algeria iliyomaliza na pointi 12.
WACHEZAJI Moussa Camara, Jean Charles Ahoua, Kibu Denis na Leonel Ateba wameonekana kuwa na mchango wa kipekee katika kuiwezesha Simba kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Simba imetinga robo fainali ikiwa kinara wa kundi A baada ya kukusanya pointi 13, ikifuatiwa na CS Constantine ya Algeria iliyomaliza na pointi 12.
Takwimu zinaonyesha kuwa, nyota hao wanne wameamua kwa kiasi kikubwa matokeo ya Simba katika mechi sita za hatua ya makundi iliyomalizika Jumapili iliyopita na pengine bila wao mambo yangeweza kuwa magumu kwa timu hiyo.
Kipa Camara anaingia katika orodha ya mashujaa wa Simba katika hatua ya makundi kutokana na uhodari wake wa kuokoa mashambulizi ambayo kama angalau machache tu kati ya hayo yangeingia nyavuni, pen-gine leo hii Simba ingekuwa kati ya timu zilizoaga mashindano hayo.

Katika mechi sita alizocheza, Camara ameokoa hatari 13 zilizoelekezwa kwake sawa na wastani wa kuokoa mashambulizi 2.2 kwa mechi.
Hii inamaanisha kuwa iwapo Camara angeshindwa kuokoa nusu tu ya hatari alizozuia, Simba leo hii isi-nge-kuwa imetinga robo fainali kwa vile mechi tatu kati ya nne ilizoshinda, ushindi wake ulikuwa wa tofauti ya bao moja hivyo zingemalizika kwa sare na pia hata mechi moja ambayo ilitoka sare ingeweza kupoteza.
Kudhihirisha namna ambavyo Camara amekuwa mchezaji muhimu kwa Simba katika hatua ya makundi, kipa huyo ni miongoni mwa wachezaji wa Simba waliocheza kwa dakika nyingi kwenye makundi ambapo ametumika kwa dakika 720.

Wakati Camara akiifanya kazi yake vyema kwenye safu ya ulinzi, katika nafasi ya kiungo na ushambuliaji, Ahoua, Ateba na Kibu wameitendea haki jezi ya Simba kutokana na kile ambacho kila mmoja amekifanya.
Ahoua ndiye anaonekana alikuwa silaha kubwa ya Simba katika hatua ya makundi kwani ameimaliza akiwa kinara wa kuhusika na mabao mengi ya timu yake (manne) katika makundi akifunga mawili na kutoa asisti za mabao mengine mawili.
Mabao yote mawili ambayo Ahoua ameyafunga, yameamua mechi za Simba katika hatua hiyo ambapo la kwanza liliifanya Simba kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola na la pili alifunga ugenini dhidi ya CS Sfaxien ambalo lilikuwa la kipekee katika mechi hiyo.
Kibu Denis aliiamua mechi ambayo Simba ilipata ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya CS Sfaxien kwa kufunga mabao yote, kinyume cha hapo huenda Simba ingetoka sare au kupoteza nyumbani.

Mshambuliaji huyo alifunga bao la kuongoza juzi dhidi ya CS Constatine ambalo lilikuwa la tatu kwake kwenye hatua ya makundi.
Leonel Ateba ndiye aliyeihakikishia Simba kutinga hatua ya robo fainali kwa kufunga bao la kusawazisha katika mechi ya ugenini dhidi ya Bravos ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Nyota huyo kutoka Cameroon pia alifunga katika mechi ya mwisho ambayo Simba ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Constantine.
Hii ni mara ya pili kwa Simba kumaliza hatua ya makundi ikiwa inaongoza huku ikiandika historia ya kufunga katika mechi zote sita za hatua hiyo.
NAMBA ZA SIMBA
Mchezo wa kwanza dhidi ya Bravos do Maquis kutoka Angola, ulimalizika kwa Simba kushinda 1-0. Walimiliki mpira kwa asilimia 52, huku wakifanya mashambulizi 15, kati ya hayo mawili yalielekea kwenye lango. Bravos do Maquis walikuwa na umiliki mdogo wa mpira kwa asilimia 48, na walifanya mashambulizi sita, lakini walikosa ufanisi wa kumaliza nafasi zao.
Simba walikosa nafasi nyingi, lakini pasi zao zilikuwa bora kwa asilimia 80 (310 kati ya 387), jambo ambalo lilisaidia kudhibiti mchezo na kuhakikisha wanapata ushindi muhimu.

Simba walikutana na kipigo cha 2-1 kutoka kwa Constantine ya Algeria katika mchezo wao wa pili. Ingawa walipoteza, walionyesha uthubutu mkubwa. Katika mchezo huu, walimiliki mpira kwa asilimia 49, kidogo tu nyuma ya Constantine, ambao walimiliki asilimia 51.
Simba walipiga mashuti sita, moja kati ya hayo lililenga lango, wakati Constantine walipiga mashuti tisa, na matatu kati ya hayo yalilenga lango. Pasi za Simba zilikuwa na ufanisi wa asilimia 76 (327 kati ya 432), lakini walikosa kumaliza nafasi nzuri.
Katika mchezo mwingine dhidi ya CS Sfaxien kutoka Tunisia, Simba walishinda 2-1 huku wakimiliki mpira kwa asilimia 80. Hii ilikuwa ni asilimia kubwa zaidi ya umiliki wa mpira katika michezo yao.
Simba walipiga mashuti 18, ambapo saba kati ya hayo yalilenga lango. Pasi zao zilikuwa bora, zikifika kwa asilimia 84 (540 kati ya 645). CS Sfaxien walikuwa na umiliki mdogo wa mpira kwa asilimia 20.
Katika mchezo mwingine dhidi ya CS Sfaxien, Simba walishinda 1-0, ingawa walimiliki mpira kwa asilimia 44 tu. Walipiga mashuti saba, lakini walifunga bao moja tu. Walipiga pasi 318 sahihi kati ya 433 (sawa na asilimia 73). CS Sfaxien walipiga mashuti sita, lakini walishindwa kupenya ulinzi wa Simba na hatimaye kupoteza mchezo.

Simba walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Bravos katika mechi ya tano. Walimiliki mpira kwa asilimia 56, wakipiga mashuti 25, ambapo saba kati ya hayo yalilenga lango. Pasi zao zilikuwa za kiwango cha juu, wakipiga kwa usahihi 340 kati ya 408 (sawa na asilimia 83). Sare hii ilitosha kwa Simba kufuzu robo fainali kabla ya mchezo wa mwisho kwa kuwa walifikisha pointi 10.
Katika mchezo wa mwisho wa makundi, Simba walimaliza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Constantine ya Algeria. Walimiliki mpira kwa asilimia 69 na walipiga mashuti 20, matano kati ya hayo yakilenga lango. Hii ilikuwa ni moja ya michezo bora kwa Simba, wakipiga pasi za usahihi 559 kati ya 632 (sawa na asilimia 88), kiwango cha juu zaidi cha pasi katika mechi za makundi.
MSIKIE FADLU
Kocha Fadlu Davids alisema kuwa kikosi chake kiujumla kinastahili pongezi kutokana na uwajibikaji wa kila mchezaji.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kazi nzuri ambayo wamefanya hadi tukafanikiwa kumaliza hatua ya makundi tukiwa tunaongoza. Mechi zilikuwa ngumu lakini walijitoa kuhakikisha tunafanya vizuri na hatimaye tumeweza kutimiza lengo la kuingia hatua ya robo fainali.
“Lakini kuanzia robo fainali, mashindano ndio kwanza yanaanza, hivyo tunatakiwa kusahau kwa haraka hiki na kuanza maandalizi kwa ajili ya hatua inayofuata.”
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, aliongeza kuwa: “Tulijua hatua ya makundi itakuwa ngumu, lakini timu imeonyesha uthubutu na jitihada kubwa. Tumekutana na timu bora kama Constantine, CS Sfaxien na Bravos do Maquis, lakini kwa kushirikiana, tumefanikiwa kufuzu robo fainali kwa kumaliza kinara wa Kundi A. Hii ni hatua muhimu, lakini bado safari yetu haijamalizika.
“Hatua ya robo fainali itakuwa ni changamoto nyingine kubwa. Tutakutana na timu za kiwango cha juu, lakini hatuwezi kuachia hii nafasi tuliyopata. Tunahitaji kuendelea kuwa makini katika kumaliza nafasi zetu na kuimarisha ulinzi. Tunapozungumzia Simba, tunazungumzia timu ambayo inajivunia umoja, nguvu ya pamoja na ari ya kupigania mafanikio.”