Bocco mfungaji bora wa mabao 16, kuna maswali yamejijibu

Wednesday July 21 2021
bocco pic
By Edo Kumwembe

JOHN Bocco juzi alifunga bao moja katika pambano la mwisho dhidi ya Namungo na kumaliza Ligi Kuu akiwa ni mfungaji bora. Mabao 16 kibindoni ambayo yanaacha baadhi ya maswali tukiwa tumeufunga msimu na kusubiri mwingine ujao.

Mabao 16 katika mechi 34 ni mabao machache kwa mfungaji wa ligi yoyote ile. Alipaswa kufunga mengi zaidi. Inapendeza kuwa mfungaji bora ambaye una mabao kuanzia 20 na kuendelea. Hata hivyo hauwezi kumlaumu sana Bocco. Kuna nyakati alikuwa majeruhi.

Walioshika nafasi za pili ni Chris Mugalu na Prince Dube. Wote wana mabao 14. Huyu Mugalu amecheza mechi 18 tu katika hizo ni mechi tano tu ndizo ambazo alimaliza dakika zote 90. Huyu Dube alicheza mechi 23 tu. Kuna wakati alisafiri kwenda Afrika Kusini kutibiwa.

Tunaanzia hapa. Wafungaji wetu bora walifunga mabao machache, na pia wengi wao walicheza mechi chache. Wote wamecheza mechi pungufu zaidi ya 10. Ina maana labda kama wangefikisha mechi 30 tu kila mmoja huenda tungepata mfungaji bora mwenye mabao 22 na kuendelea sio mbaya.

Swali linakuja kwa mheshimiwa Waziri wa zamani wa michezo, Dk Harrison Mwakyembe. Wako wapi hao wachezaji wa kizawa ambao walipaswa kulindwa dhidi ya wageni? Kuna nyakati hapa tuliambiwa kwamba wachezaji wa kigeni na wanadhibiti nafasi za wazawa. Wako wapi hao wachezaji wa kigeni hasa katika nafasi ya ushambuliaji?

Bocco tunamfahamu na uwezo wake. Ndiye mshambuliaji wa kizawa ambaye amekuwa akitutetea zaidi tangu kuondoka kwa Saimon Msuva. Hata yeye mwenyewe ukiangalia namba zake kwa upande wa ufungaji na dakika alizocheza huenda Mugalu angeweza kuwa mfungaji bora kama angepata nafasi zaidi kikosini.

Advertisement

Ina maana kama Mugalu angepata dakika nyingi zaidi basi angekuwa mfungaji bora ndani ya klabu yake na katika ligi kwa ujumla. Hii ina maana kwamba tungekuwa na mfungaji bora wa kigeni kama ambavyo imekuwa mara zote.

Kuna mambo mawili huwa tunajidanganya. La kwanza, Mheshimiwa Mwakyembe aliwahi kutuletea mezani kwamba inabidi tulinde vipaji vyetu vya ndani kwa kupunguza idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni. Asilimia 90 ya wachezaji wa kigeni wapo Simba, Yanga, Azam na Namungo kidogo. Hao wazawa waliopo katika timu nyingine wanafanya kitu gani zaidi? Hakuna kitu cha maana. Walipaswa kuwepo juu ya msimamo kwa sababu wengi wamecheza mechi sawa au zaidi ya hawa watatu waliopo juu.

Pale Yanga, mfungaji wao bora ni Yacouba Sogne. Amefunga mabao nane lakini pia ni mmoja kati ya wapikaji wazuri wa mabao. Hata katika timu kubwa ambayo washambuliaji wake hawakufanya vyema msimu huu bado mfungaji wao bora ametoka katika wageni.

Jambo jingine ambalo tunajidanganya ni pale ambapo kocha yeyote wa timu ya taifa huwa anapigiwa kelele kwamba anapenda sana kuchukua wachezaji wa Simba, Yanga na Azam na alipaswa kutoa jicho lake kwingine katika timu za mikoani.

Rafiki yangu, Jamal Malinzi akiwa rais wa TFF alikwenda mbali zaidi kwa kuanzisha programu iliyoitwa Maboresho. Programu iliyolenga kwenda mikoani na wilayani kusaka vipaji vya kuchezea timu ya taifa ya Tanzania. Ilikuwa kichekesho sana.

James Hardley Chase, mtunzi mahiri wa zamani wa vitabu aliwahi kuandika kitabu kilichoitwa ‘The Golden fish has no hiding place’. Alimaanisha kwamba samaki mzuri hana sehemu ya kujificha. Ni lazima ataonekana tu. Unawezaje kumuona mchezaji mzuri katika kikosi cha Mbozi huku akiwa hajaonwa na Prisons, Mbeya City, Ihefu halafu aje kucheza timu ya taifa. Inawezekana vipi? Maajabu. Ulikuwa ni upotevu wa pesa. Tusidanganyane, tuambiane ukweli kwamba kwa sasa Tanzania ina uhaba mkubwa wa vipaji.

Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ asingemaliza ligi akiwa na mabao nane katika kikosi cha Yanga. Winga kama Edibily Lunyamila alikuwa anafunga mabao zaidi ya 20. Leo Yanga ina mfungaji bora wa kigeni na ana mabao nane tu.

Zamani kuna washambuliaji ambao kabla hawajagusa Simba wala Yanga ilikuwa kila msimu wanafunga mabao 15 na zaidi. kina Ildefonce Amlima, Juma Mgunda, Duncan Butinini, Kitwana Suleiman, David Mihambo na wengineo. Leo DitNchimbi ram anafungaje bao moja msimu mzima akiwa na Yanga?

Zamani karibu kila timu ya Ligi Kuu ilikuwa na mshambuliaji mmoja ambaye alikuwa ni tishio na gumzo. Walikuwa wanazidiwa uwezo tu na kina Zamoyoni Mogella lakini bado walikuwa tishio na kama ungekwenda ovyo katika mikoa yao ungeondoka na aibu. Hata ukiwaweka wageni kando bado unagundua kuna pengo kubwa kati ya Bocco na washambuliaji wazawa. Inabidi kuliziba pengo hilo kabla haujafikiria namna ya kupambana na wageni. Nani mrithi wa Bocco kwa washambuliaji wa ndani? Simuoni.

Kuna mahala tumekwama na hatujui tunafikaje baada ya hapa. Viwango vya timu zetu nje ya Simba, Yanga na Azam vimekwenda chini na pengo ni kubwa. Timu kama ya Biashara Musoma imemaliza Ligi ikishika nafasi ya nne. Inaonekana kama ni mafanikio makubwa kwao lakini ukweli ni kwamba Biashara imefungwa mabao mengi kuliko mabao ya kufunga.

Nafasi nyeti kama ya nne lazima iende kwa timu ambayo imefunga mabao zaidi kuliko yale ya kufungwa. Waliwezaje kufika hapo? Ni kwa sababu walikumbana na timu nyingine ambazo zilionekana kuchoka zaidi yao.

Tunahitaji mjadala wa kitaifa wa kujua kwanini vipaji vimeondoka katika soka letu. Sioni namna gani ambavyo unaweza kuwazuia wageni kujaa nchini kwa aina ya wachezaji tulionao. Tutakuwa tunatengeneza ligi ya namna gani? nadhani tutakuwa na Ligi ambayo haitakuwa na mvuto.


Advertisement