BILIC: Mwamba wa Croatia mwenye vituko vyake

Muktasari:

  • Kisoka kwenye nchi hizi, ni Croatia ndiyo inayojulikana zaidi kati ya nchi hizo na imecheza fainali tano za Kombe la Dunia, mwaka 1998, 2002, 2014, 2010 na 2018.

UNAZIFAHAMU nchi za Balkan? Hizi ni Serbia, Croatia, Macedonia, Slovania, Kosovo na Montntenegro na awali zilikuwa taifa moja la Yugoslavia mwaka 1943, kabla ya kusambaratika kwa taifa hilo na kuibuka nchi hizo mwaka 1991.

Kisoka kwenye nchi hizi, ni Croatia ndiyo inayojulikana zaidi kati ya nchi hizo na imecheza fainali tano za Kombe la Dunia, mwaka 1998, 2002, 2014, 2010 na 2018.

Katika fainali za Kombe la Ulaya za 2008 Croatia iliichapa Ujerumani 2-0 na kuichezea danadana, lakini iliaga mashindano ilipofungwa na Uturuki katika robo fainali.

Katika mafanikio ya Croatia hausahauliki  mchango wa mchezaji wake wa zamani na baadaye kocha wa timu hiyo anayeitwa mdogo wa umri, mkubwa wa mambo na mwingi wa vishindo, Slaven Bilic.

Ni nyota wa kikosi kilichochukua medali ya shaba katika fainali za Kombe la Dunia za 1998 baada ya kuilaza Uholanzi 2-1.

Croatia iliitoa Ujerumani katika robo fainali kwa kuichapa 3-0. Bilic alikuwa na Davor Suker aliyekuwa mfungaji bora kwa kutingisha wavu mara sita na kufuatiwa na Gabriel Batistuta wa Argentina na Christian


Vieri wa Italia (mabao matano).

Miaka 10 baada ya fainali za mwaka 1998 ambazo Ufaransa alibeba kombe kwa kuilaza Brazil 3-0 katika fainali aliiadhibu tena Ujerumani, lakini akiwa kocha.

Bilic ambaye sasa yupo Saudi Arabia akiwa ni kocha wa klabu maaarufu ya Al-Fateh alikuwepo Ujerumani kutoa ushauri kwa Croatia ambayo ilitolewa katika mzunguko wa kwanza kwa wastani wa mabao ikiwa imeshika nafasi ya tatu na kuwa na alama tatu, nyuma ya Hispania (5) na Italia (3) na Albania (3).

Baada ya Croatia kutolewa, Bilic alisema bahati ndio adui mkubwa wa soka.

Bilic alianza na klabu ya Croatia, Hajduk Split, akiwa na miaka tisa na kuwa nayo kwa miaka sita kabla ya kujiunga na Karlsruher ya Ujerumani 1993.

West Ham ilimsajili mwaka 1996 na alipokuwa nayo alichaguliwa kujiunga na kikosi cha Croatia cha mashindano ya Kombe la Euro 1996 yaliyofanyika Uingereza na ilifika robo fainali na kufungwa na Ujerumani iliyobeba kombe.

Alijiunga na Everton mwaka 1997, lakini kila mara alipewa kadi nyekundu na 1998 alikuwemo katika kikosi cha Croatia kiliocheza fainali za Kombe la Dunia na kucheza rafu zisiosahaulika.

Kwake yeye rafu ni muhimu na kama mwamuzi sio makini hiyo ni shauri yake.

“Ukizuia bao kwa kucheza rafu au kufunga kwa mkono wewe ni mchezaji mzuri. Lililo muhimu ni matokeo ya mchezo na sio yatakayotokea baadaye,” alisema.

Baada ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 1998, Bilic aliumia goti, akaachana na Everton na kurudi nyumbani kwa matibabu.

Alipoona hatakiwi na klabu za England alibaki Croatia na klabu yake ya zamani, Hajduk Split. Alikaa nayo kwa muda mfupi na kustaafu.

Wengi walisikitika kutokumwona beki huyu aliyewakaba washambulizi kwa umahiri. Kingine kichowavutia ni maudhi yake, kama walipoifunga England na kuzunguka uwanjani na kuwaambia mashabiki; “Amkeni.. Jua la utawala wa Kiingereza limetua.”

Mojawapo ya nukuu yake mashuhuri ni ya kuwaambia wanawake: “Kinamama nisameheni. Kama nigeweza kufunga ndoa na soka na kupata watoto, mke wangu angekuwa mpira na wanangu ningewapa majina ya goli, kona na penalti.”

Bilic alipenda kuvuta sigara hata wakati wa mapumziko. Ipo siku aliumia na alipotoka nje kwa matibabu aliomba apatiwe sigara.

Kocha alikataa na kuahidi kumpa bomba zima baada ya mchezo na jambo la kwanza alilomwambia baada ya kushinda mchezo  ni kupewa bomba la sigara.

Baada ya kustaafu alikuwa kocha na kukabidhiwa timu ya vijana ya Croatia kwa michuano ya Kombe la Ulaya mwaka 2006.

Alichaguliwa kocha wa timu ya taifa mwaka 2006 na mchezo wa kwanza wa timu hiyo chini ya uongozi wake ulikuwa suluhu dhidi ya Urusi.

Bilic alilaumiwa kwa kuwafukuza wachezaji nyota Dario Srna, Ivica Olic na Nosko Balaban ambao walikwepa mazoezi, lakini alisema hawezi kuvumilia kibri katika kikosi chake.

“Mchezaji anaweza kufanya ujeuri nyumbani kwake na sio katika timu ninayoifundisha,” alisema.

Baadaye aliiongoza Croatia kukata tiketi ya Kombe la Ulaya mwaka 2008 na kushinda michezo yote mitatu ya kundi lake, lakini ilitolewa katika robo fainali na Uturuki.

Baada ya Euro, 2008  alitakiwa afundishe timu mbalimbali za taifa na klabu za Ulaya na kiingia mkataba wa miaka miwili kuifundisha Croatia hadi zilipomalizika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 zilizofanyika Afrika Kusini.

Baadaye alizifundisha FC Lokomotiv ya Moscow, Urusi  mwaka 2012 kwa mwaka mmoja, Bekistas ya Uturuki, West Ham (England), Al-Ittihad (Saudi Arabia), West Bromwich Albion (England), Bijinf Guon ya China na sasa Al Fateh ya Saudi Arabia.

Miaka minne iliyopita aliombwa arudi kuifundisha Croatia, lakini alisema: “Nimefika juu na kuwa kocha wa timu ya taifa na sasa ninafundisha klabu. Safari yangu si ya kupanda bali kuteremka mlima na nipo tayari kufundisha watoto na sio timu ya taifa.”

Bilic anayezungumza lugha nyingi, ikiwamo Kirusi, Kijerumani, Kiingereza na Kitaliana ni mwanasheria na mwanamuziki anayepiga gitaa na kuimba.

Alitunga na kuimba wimbo wa kuishangilia Croatia katika  mashindano ya Euro 2008. Nyimbo hii iliimbwa na mashabiki wa nchi yake katika fainali za Euro 2024 zinazoendelea kule Ujerumani.

Anakumbukwa kama mchezaji aliyekuwa na mengi uwanjani na nje na kweli ni mdogo wa umbo bali mkubwa wa mambo.