Bila jasho Cristiano ronaldo, Messi wapo tu

Muktasari:
- Timu nyingi zinadaiwa kuwa katika mazungumzo ya kusajili wachezaji wapya na nyingine zinafanya mpango wa kuwasainisha mikataba mipya mastaa.
FLORIDA, MAREKANI: LIGI kubwa kibao duniani zinaelekea ukingoni ambapo mbali ya timu kupambana kuwania nafasi za juu na nyingine kukwepa kushuka daraja, tayari mipango ya kufanya vizuri msimu ujao imeshaanza.
Timu nyingi zinadaiwa kuwa katika mazungumzo ya kusajili wachezaji wapya na nyingine zinafanya mpango wa kuwasainisha mikataba mipya mastaa.
Baadhi ya wachezaji wanamaliza mikataba mwisho wa msimu huu na hadi sasa hakuna mwafaka ikiwa watasalia katika au wataondoka.
Hiyo imewaweka katika orodha kuwa wachezaji wanaoweza kupatikana bure ifikapo dirisha lijalo la majira ya kiangazi na miongoni mwao ni Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Hapa tunakuletea orodha ya baadhi ya mastaa ambao watapatikana bila gharama ifikapo mwisho wa msimu.

Joshua Kimmich
Licha ya kuwa Bayern Munich inataka kumsainisha mkataba mpya utakaokuwa mnono, hadi sasa staa huyu hajafanya uamuzi juu ya hatma yake ikiwa atakubali kukaa au ataondoka.
Akiwa na umri wa miaka 29 na kwenye kilele cha uwezo wake kama mmoja wa viungo wa ulinzi bora zaidi duniani, Kimmich anawindwa na klabu lukuki dunia ikiwemo Barcelona na Man City ambazo ni miongoni mwa zile zilizoonyesha nia ya kumsajili.
Staa huyu anataka kutulia kabla ya kufanya uamuzi wa wapi atue kwa sababu ana ofa nyingi.

Alexander-Arnold
Dalili zote zinaonyesha kuwa Real Madrid wana matumaini makubwa ya kumsajili Trent Alexander-Arnold kwa usajili huru ifikapo mwisho wa msimu huu ambapo mkataba utakuwa unamalizika. Trent ambaye mazungumzo ya mkataba mpya na Liverpool hayaonekani yakifikia mwafaka ameripotiwa kuwa ameshawishiwa na ofa ya Real Madrid ambayo imekuwa ikimuinda tangu mwaka jana.
Inaelezwa hata kuwa tayari ameijulisha Liverpool nia ya kuhamia Bernabeu na kuungana na rafiki yake wa karibu Jude Bellingham.
Hata hivyo, bado Liverpool inaweza kupata kiasi kidogo cha pesa kwa kumuuza kwani Madrid itahitaji kumsajili mapema ili kwenda naye katika Kombe la Dunia la Klabu ambapo muda ambao michuano itaanza, mkataba wa Trent bado utakuwa umebakisha wiki kadhaa.

Lionel Messi
Ingawa haionekani kama atachukua uamuzi wa kuondoka katika dirisha lijalo badala yake atasaini mkataba mpya, lakini hadi sasa mambo yalivyo ni kwamba amebakisha miezi saba kabla ya kuwa mchezaji huru. Messi anaripotiwa kuyapenda mazingira ya Florida ingawa mabosi wa Inter Miami wanataka kuharakisha mchakato wa kumsainisha mkataba mpya wakihofia timu za Saudi Arabia kumpa ofa nono itakayomshawishi aondoke.

Alphonso Davies
Sakata hili limekuwepo kwa muda mrefu, lakini sasa huenda mambo yakadhihirika juu ya hatma yake kwa sababu msimu unaelekea kumalizika.
Davies ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu, kwa kiasi kikubwa amekuwa akihusishwa na Real Madrid, Man Ynited na Liverpool ambazo zote zimevutiwa sana kumsajili kutokana na kiwango chake na kuwa kwake huru. Hata hivyo, Bayern pia ipo katika mazungumzo ya mkataba mpya ili kumbakisha, hivyo lolote linaweza kutokea.

Leroy Sane
Leroy Sane huenda akawa anacheza kwa ajili ya mustakabali wake katika Bayern Munich katika miezi ijayo, baada ya kushindwa kung’ara tangu aondoke Manchester City 2020. Inaonekana kuna uwezekano mdogo kwa Bayern kuendeleza mkataba wake, isipokuwa kama kutakuwa na ongezeko kubwa la kiwango chake. Akiwa na umri wa miaka 28, hatakosa wa kumhitaji licha ya kutokuwa na uthabiti, na hivi karibuni alikiri mapenzi yake ya kudumu kwa Ligi Kuu ya England.

Cristiano Ronaldo
Kumekuwa na tetesi nyingi baadhi zikidai Cristiano Ronaldo anaweza kuungana na Lionel Messi katika kikosi cha Inter Miami, huku nyingine zinaibua kuwa anaweza kutua Manchester City iliyowahi kuhitaji saini yake kabla hajabadilisha gia angani na kwenda Manchester United.
Mkataba wa Ronaldo na AL Nassr unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu ifikapo Juni 30. Mara kadhaa mwenyewe amekuwa akieleza kwamba anatamani kuendelea kubaki katika timu hiyo ingawa vigogo wengine wameshaanza kummezea mate na kuitamani huduma yake. Hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote yaliyoripotiwa kuanza kati yake na mabosi wa Al Nassr, lakini anapewa nafasi kubwa ya kubaki.

Kevin de Bruyne
Manchester City imeshathibitisha kwamba haitomwongeza mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia na Mbelgiji huyo ataondoka mwisho wa msimu huu ikiwa ni baada ya kudumu kwa miaka 10.
De Bruyne ambaye mkataba wake unaisha mwisho wa msimu mara kadhaa amekuwa akitajwa kuwa katika rada za vigogo kadhaa wa Marekani, lakini changamoto kubwa imekuwa ni kiasi cha mshahara anachotaka.
Kwa sasa sehemu anayopewa nafasi kubwa ya kwenda ni Saudi Arabia ambako aliwahi kuwekewa ofa inayokaribia Pauni 500,000 kwa wiki na baadhi ya timu, lakini alikataa na kuamua kuendelea kusalia Man City.
Mbali ya kwenda nje ya Bara Ulaya, kiungo huyo anaweza kuamua kusalia barani humo na kucheza soka la ushindani ingawa itatakiwa akubali kupokea mshahara mdogo tofauti na ule aliokuwa anauchukua Man City.