Baada ya miaka 20 Jerry Tegete atundika daruga
Muktasari:
- Hii ni familia ya mpira, licha ya mzee John umri kuonekana kumtupa mkono, alionekana kuwa ngangari kwa kunipokea umbali wa mita 700 na kutembea naye kwa mwendo wa taratibu hadi nyumbani (Kirumba) ambako mkewe, mama, Jerryson alikuwapo kabla ya kijana wao kujumuika nasi mchana mida ya saa nne asubuhi.
KATIKA jiji la Mwanza, nyumba ya familia ya Tegete inabeba simulizi la vizazi viwili vilivyochagua soka kama maisha yao. Hapa ndipo nilipopata nafasi ya kuzungumza na nyota wa zamani wa Yanga na timu ya taifa la Tanzania, Jerryson pamoja na baba yake, mzee John.
Hii ni familia ya mpira, licha ya mzee John umri kuonekana kumtupa mkono, alionekana kuwa ngangari kwa kunipokea umbali wa mita 700 na kutembea naye kwa mwendo wa taratibu hadi nyumbani (Kirumba) ambako mkewe, mama, Jerryson alikuwapo kabla ya kijana wao kujumuika nasi mchana mida ya saa nne asubuhi.
Mzee John ni muongeaji na mchangafu kama ilivyo kwa Jerry hivyo ilikuwa ikipigwa stori moja baada nyingine kabla ya kuanza mahojiano yetu, ilianza kwa kuongelea vile alivyofanya makubwa wakati akicheza soka kabla ya kijana wake kuzaliwa.
“Niliucheza sana mpira na baadaye nilivyoona sasa imetosha ilibidi nijikite katika majukumu mengine (mtaalam wa viwanja) lakini bado niliendelea kuishi mpira, nakumbuka nilianza kuucheza nikiwa shuleni wakati huo nasoma St Peter’s, Bagamoyo, hizi hela ndogondogo nilikuwa napata sana wakati huo,” anasema mzee John na kuendelea;
“Nilisoma hadi kidato cha nne, nikakaa Shinyanga baadaye nikaona niende Kagera kwenye chuo cha kilimo, nikiwa huko niliendelea kucheza mpira hadi nikachaguliwa katika timu ya mkoa, tukacheza Taifa Cup ambako tulifika hadi robo fainali kama sijasahau hiyo ilikuwa miaka ya 1970 huko, kipa wetu alikuwa Juma Mhina tulikuwa na kikosi kizuri baada ya kumaliza kule nikarudi Mwanza, nikajiunga na Copco.”
Mzee John anaendelea kujivunia kwa kusema enzi zake alicheza dhidi ya West Brom na Aston Villa wakati ambao timu hizo ziliamua kuja Afrika kwa ajili ya maandalizi ya msimu mwingine yani pre season; “Ni miaka ya zamani sana mwanangu (mwandishi), ujue Mwanza ilikuwa mkoa mkubwa sana kisoka, ukiondoa Dar, huu ulifuata.”
Baada ya kuongea naye kwa kirefu ikabidi tuanze kuongelea miaka 20 ya mwanaye katika soka la ushindani, anatabasamu na kukiri mwanaye amefanya zaidi ya kile ambacho alifanya yeye katika uchezaji wake huku akitusimulia vile alivyokutana na mama yake (mkewe) hadi kuzaliwa wake kwa mshambuliaji huyo ambaye mbali na Yanga amezichezea pia Mwadui United, Kagera Sugar, Majimaji na Allince.
KUZALIWA KWA JERRY
Mzee John anasema kwanza kabisa alikutana na mama yake na Jerry, Shinyanga wakati huo akiwa ofisa wa michezo; “Mama Jerry alikuwa mwalimu, nilipofika tulipendana na kuamua kufunga ndoa na akawa mke wangu hadi sasa, hata kutoka Shinyanga kuja hapa Mwanza tulikuwa wote.
“Jerry ni mtoto wangu wa kwanza, alizaliwa Shinyanga, alikuwa baraka sana kwenye familia yetu na nakumbuka kipaji chake cha soka kilianza tangu akiwa mdogo, nilikuwa nikienda kwenye mihangaiko yangu na kurudi na mpira basi hapo hakuna ambacho kitafanyika hata kula wakati mwingine alikuwa anasahau, ni kucheza tu mwanzo mwisho,” anasema.
WALIPOHAMIA MWANZA
Baada ya kujipata Mzee John anasema ilibidi kuhamia Mwanza ambako alijenga mjengo wake wa kwanza wakati huo Jerry akiwa mdogo lakini aliendelea kuona vile kijana wake anaweza kufuata nyayo zake na alipomaliza shule ya msingi aliona kuna haja ya kuchukua hatua zaidi kwa ajili ya kumuendeleza.
“Wakati nikicheza soka nilifahamiana na Kanali mstaafu Idd Kipingu, hivyo niliona niongee naye kwa ajili ya kijana wangu, moja kwa ajili ya kuendelezwa kielimu pili kuendelezwa kipaji chake, ombi langu lilipokewa vizuri na ikabidi kijana sasa akaanze maisha yake rasmi huko na huo ndio ulikuwa mwanzo rasmi wa safari yake ya mafanikio,” anasema na kuongeza;
“Ilikuwa ya mafanikio kwa sababu yaliyotokea mengine yalinishangaza kwa sababu kutoka kusoma shule hadi kucheza timu ya taifa haikuwa jambo dogo, nyota yake iling’ara sana na hatimaye sasa kucheza timu ya maisha yake, Yanga, familia yetu sisi ni Yanga hivyo ilikuwa jambo kubwa sana kwa kijana wangu.”
AUKUBALI MZIKI
“Jerry amecheza zaidi yangu. Hapo nakubali, amefanya zaidi ya ilivyokuwa kwangu, mimi nilikuwa mchezeshaji zaidi, mpishi wa mabao ila kijana wangu amekuwa mfungaji mzuri, nimemtazama kiwango chake nikiri kwamba ni kikubwa sana ukilinganisha na changu,” anasema na kuongeza;
“Wakati mimi nikicheza soka nilimzidi kiwango baba yangu ambaye alikuwa akicheza soka Afrika Kusini, inawezekana watu wakawa hawajui lakini baba yangu mimi alicheza huko mpira kabla ya kustaafu na kuamua kurudi Tanzania na maisha yetu yalikuwa Zanzibar, sisi tuna undugu na familia ya Agrey Morris. Baba alikubali uwezo wangu sasa na mimi nakubali alichofanya mwanangu.”
Hakuishia hapo mzee Tegete yupo na imani kwamba atatokea kijana mwingine katika familia yao ambaye pengine anaweza kufanya zaidi ya Jerry kwa sababu siku zote rekodi zipo kwa ajili ya kuvunjwa.
KAMA ANGETUA SIMBA
Mzee John anasema kama mwanaye angetua Simba wakati ule ambao alikuwa moto wa kuotea mbali, ingembidi tu kukubaliana na matokeo kwa sababu mpira ndio kazi ya mwanaye lakini asingemsapoti katika mechi ya watani.
“Jerry ni mtu wa taaluma sana sidhani kama angechanganya kazi na mapenzi, lakini sisi ambao tupo huku tungepata tabu, robo ingekuwa ikiuma kuona kijana wangu mwenyewe ananipa mateso,” anasema mzee John huku akiendelea;
“Nashukuru Mungu kwakweli kwa sababu alicheza Yanga na nilifurahia wakati mzuri ambao alikuwa nao, alifunga na kusaidia timu kupata mafanikio hata wakati anaondoka aliondoka vizuri.”
MWAMBA ATIA TIMU
Jerry alitia timu nyumbani kwa wazazi wake huku akijua uwepo wangu hapo, tulisalimiana na kisha kumkumbusha vile nilikutana naye kwa mara ya kwanza Kinyerezi ambako nimekulia.
Alishangaa kwa sababu ni zaidi ya miaka 10 iliyopita ambapo alikuwa akipenda kwenda uwanja wa Kineyerezi shule na kufanya mazoezi akiwa na David Luhende na kuna nyakati Shomary Kapombe naye alikuwa akifanya hapo mazoezi hasa kipindi ambacho ligi imetamatika.
“Dah! Kweli aisee, kitambo sana lakini ndio maisha ya mpira yalivyo, utacheza na kuna wakati utafika wa kupisha vijana wengine, nimecheza mpira kwa miaka mingi sasa imetosha,” anasema Jerry.
“Unasema imetosha?” Ilibidi nimuulize, “Kivipi ndugu yangu? Inamaana umeamua kustaafu?” alinitazama usoni na kusema; “Ndio nimestaafu kwa sababu mpira ni mchezo wa umri, nguvu yangu ya ushindani kwa sasa ni tofauti na miaka ile ambayo uliniona Kinyerezi.”
Jerry anafichua kwa sasa yeye ni meneja wa timu ya vijana ya Pamba Jiji na anafurahia nafasi hiyo; “Nimeona sio mbaya nikiwa sehemu ya kusaidia ndoto ya vijana wengine, uzoefu niliopata utakuwa msaada katika upatikanaji wa kina Jerry wengine.”
AMTAJA MAXIMO
Jerry anakumbuka na kusimulia vile Maximo alivyofanya kazi kubwa kuhakikisha Taifa Stars inakuwa timu ya watu, timu inayocheza kwa ajili ya taifa zima. “Alitufanya tuwe familia moja, uwanjani na nje ya uwanja. Ndiyo maana mpaka leo tunamuita baba lao, kwa sababu mchango wake haukuwa wa kawaida,” anasema.
“Licha ya kutokufanya vizuri kwenye michuano ya Chan 2009, kufuzu kwenye mashindano hayo ilikuwa mafanikio makubwa sana kwa taifa letu. Ilikuwa ishara kuwa soka la Tanzania lilikuwa linapanda ngazi,” anaongeza.
Anasema mafanikio hayo yaliongeza heshima na umaarufu wa Taifa Stars nje ya mipaka ya Afrika, yakifungua milango ya kutambulika kimataifa na kuwafanya wachezaji wa Kitanzania kuaminiwa zaidi.
Anasema soka limempa mafanikio makubwa, uzoefu na heshima, japokuwa bado anaamini hajafikia malengo yote aliyojipangia. “Kuna mengi nimeyapata kupitia soka, mengine si rahisi kuyaweka wazi.”
ANGEKUWA MWANASHERIA
“Nimekuwa katika familia ya soka, baba yangu alikuwa mwanasoka na sasa ni kocha alikuwa anapenda sana nicheze soka, hivyo kuingia huko vilikuwa ni vishawishi vya baba ambaye alimzidi nguvu mama ambaye alikuwa anatamani kuona mwanae nasoma,” anasema.
“Nilikuwa napenda sana kuwa mwanasheria, lakini ndoto ilipotea baada ya kujikuta njia yangu nyeupe kufanikiwa kupitia soka,” anasema na kuongeza, tangu aanze soka hajawahi kula umeme (kadi nyekundu) kutokana na kuheshimu sheria 17 za soka.
STARS, YANGA ZIMEMBEBA
Kwenye maisha kutengeneza historia ni ngumu kama huna unachofanya, kujituma kwa Jerry kumemwingiza katika historia. Kwanza kuichezea Stars na pili kuvaa uzi wa Yanga. Anakiri ni kati ya mambo yatakayobaki kwenye kumbukumbu zake milele.
“Taifa Stars na Yanga zimeingia kwenye historia ya maisha yangu. kuitwa mara ya kwanza Stars sitakaa nisahau kwani mimi sijapita njia ndefu sana kama wengine maana kipaji changu kimeonekana nikiwa shule.”
“Kila mchezaji ana malengo ya siku moja kuichezea timu yake ya Taifa, pia kwa wachezaji wa ndani kila mmoja anatamani kucheza Simba na Yanga zikiwa ni njia nzuri za kupata mafanikio nje ya nchi japo sio wote wanapitia huko,” anasema na kuongeza, kwa Yanga hana ujanja kwani ndio timu iliyomtengenezea jina na ataiheshimu sana kumkuza kisoka.
UTAMU WA NDONDO
Jerry anasimulia utamu wa kucheza mechi za mchangani (ndondo) wakati akijitafuta kipindi hicho bado alikuwa akiishi Makongo kwa ajili ya masomo na wakati wa likizo alisafiri kwenda Mwanza nyumbani kupumzika.
Akiwa huko, aliendelea kucheza soka la mitaani kama ilivyo kawaida kwa vijana wengi wenye vipaji, bila kujua kuwa kuna mtu alikuwa akimfuatilia kwa karibu.
Anasema kulikuwa na bosi mmoja aliyekuwa akiisimamia timu ya Mwanza United ambaye alivutiwa sana na kiwango chake uwanjani. Baada ya mechi moja ya mchangani, bosi huyo alimfuata na kumuomba achezee timu yake kwenye mechi iliyofuata, akimuuliza moja kwa moja anahitaji kiasi gani cha fedha ili akubali.
Kwa kuwa bado alikuwa kijana mdogo na hana uzoefu mkubwa wa masuala ya fedha, Jerry anakiri hakuwa anajua thamani halisi ya fedha kwenye soka. Anasema bila kufikiria sana, alitamka tu Sh3 milioni kama malipo ya kucheza mechi hiyo moja, kiasi ambacho kwake kilionekana kikubwa sana kwa wakati huo.
Bila ya majadiliano marefu, bosi huyo alikubaliana na ombi hilo na kwa mshangao mkubwa wa Tegete, fedha hizo ziliwekwa moja kwa moja kwenye akaunti yake ya benki.
“Kuhusu ndondo nimecheza sana na kuna siku tuliwahi kukimbizwa, hayo ni matukio ya kawaida kwa sababu mpira wa mtaani huwa na ushabiki haswa na watu huwa na uchungu sana, nikianza kukuhadithia stori moja baada ya nyingine utachoka,” anasema.
MAXIMO AFUNGUKA
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Maximo Maximo amemtaja Jerry kama mchezaji aliyekuwa mfano wa nidhamu, kujituma na kuonyesha uzalendo wa kweli kwa timu ya taifa.
Maximo anasema Jerry alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa tayari kupigana kwa ajili ya jezi ya Stars bila kujali mazingira magumu.
“Jerry alikuwa mchezaji anayeelewa maana ya kuitumikia timu ya taifa. Alikuwa tayari kujitoa, kusikiliza maelekezo na kufanya kazi kwa ajili ya wenzake. Sio kila mchezaji ana tabia hizo,” anasema Maximo.
Maximo anaongeza kuwa kizazi walichokuwa nacho akiwamo Jerry kilibeba dhamana kubwa ya kulirudisha taifa kuiamini Taifa Stars na anasema mchango wao haupaswi kusahaulika. “Tulikuwa tunajenga timu, sio kwa ajili ya matokeo ya haraka tu, bali kwa ajili ya heshima ya taifa na kizazi kijacho,” anasema.
Akizungumzia uamuzi wa Jerry kutundika daruga, Maximo anasema ni hatua ya kishujaa inayohitaji ujasiri mkubwa. “Kustaafu wakati bado watu wanakukumbuka kwa mema ni jambo la busara.”