Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Azam Media yaiachia msala TPBRC

Muktasari:

  • Mwamakula ametakiwa kulipwa fedha za Kitanzania Sh250 milioni na Kampuni ya Azam Media Limited baada ya kushinda kesi katika Mahakama ya Kinondoni, jijini Dar es salam.

TASNIA ya mchezo wa ngumi za kulipwa nchini kwa sasa inapita kwenye kiza kinene baada ya mdau mkubwa wa udhamini wa haki za matangazo Azam Media kujiweka pembeni kutokana na kushindwa kwenye kesi ya hakimiliki aliyofunguliwa na bondia wa zamani, Amos Mwamakula.

Mwamakula ametakiwa kulipwa fedha za Kitanzania Sh250 milioni na Kampuni ya Azam Media Limited baada ya kushinda kesi katika Mahakama ya Kinondoni, jijini Dar es salam.

Kesi hiyo ya madai iliamuliwa 22 Agosti, mwaka huu na Hakimu William Kaaya kwa kosa la kampuni hiyo kufanya uvunjifu wa hakimiliki na bondia huyo aliwadai Azam Media Limited na Patrick Kahemele waliiba wazo la Boxing Kazi Kazi na kuliita Vitasa.

Kwa mjibu wa taarifa, Boxing Kazi Kazi ni vipindi vya Boxing na pendekezo (proposal) ambalo lilisajiliwa Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota) mwaka 2017, na Vitasa ikaja kusajiliwa Mwaka 2021 huku pendekezo hilo na vipindi, bondia huyo alivituma kwenye baruapepe (email) ya Patrick Kahemele ambaye wakati huo alikuwa Mkurugenzi wa Michezo Azam Media Limited na baada ya kupokea alimthibitishia awe mvumilivu itakapofika 2020 atampa nafasi lakini baada ya mwaka mmoja alianza kuona maudhui hayo yakiruka hewani kwenye runinga.

Baada ya hapo Mwamakula alipeleka shitaka lake Cosota na wakafanya kikao cha usuluhishi na kuamua Boxing Kazi Kazi pamoja na Vitasa ni mawazo mfanano ndipo mdai aliamua kwenda mahakamani ili kupata stahiki zake za msingi.

Lakini uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti unaonyesha ni wazi bondia huyo siyo wa kwanza kuifungulia kesi kampuni hiyo ambayo imekuwa mhimili mkubwa wa mchezo huo nchini.

Inadaiwa huko nyuma ilikuwepo kesi kati ya kampuni hiyo na bondia Hassan Mwakinyo lakini ilimalizwa nje vyombo vya sheria, pia yupo mmoja wa  mapromota wakubwa nchini, Juma Msangi ‘Jay Msangi’ kushinda kesi aliyofungua mahakama kuu dhidi ya kampuni hiyo kwa kilichoelezwa ni ukiukwaji wa mikataba ya haki za matangazo.

Wiki iliopita, Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Patrick Kahemele alisikika katika moja ya vituo vya redio akieleza kusitisha kwa huduma ya kurusha matangazo ya mchezo huo baada ya ushindi wa kesi ya Mwamakula huku akienda mbali kwa kueleza waathirika wakubwa katika jambo hilo ni mabondia kutokana na mtu mmoja kujimilikisha mchezo huo.

Kauli hizo zikawaibua baadhi ya mabondia ambao mapambano yao yamekuwa yakionekana Azam Media kupitia Azam Sports, Twaha Kiduku alikuwa bondia wa kwanza kuongelea jambo hilo kwenye mitandao ya kijamii kisha  akafuata Ibrahim Class.

Lakini haikuishia hapo, ukafanyika mkutano wa vyombo vya habari kwa baadhi ya mabondia kuomba msamaha na kuwasihi Azam Media wasijitoe kuonyesha mchezo huku wakimuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan kuingilia kati jambo hilo kwa kuwa Azam imekuwa msaada kwa mabondia wengi.

Wakati mkutano huo unamalizika, akaibuka Mwenyekiti wa Chama cha Mabondia na kusema kilichoongolewa na mabondia hao haukuwa msimamo wa chama katika sakata hilo pamoja na kudai watawachukulia hatua mabondia wote waliokuwa kwenye mkutano huo.

Kutokana na sekeseke hilo, Mwanaspoti limefanya uchunguzi wa kutosha na kuongea na wadau mbalimbali ambao hawakuwa tayari kutajwa majina yao halisi kwenye jambo hilo huku wakitoa suluhu ya mwisho wa jambo hilo pamoja na kukomesha madudu yote kwenye mchezo huo.

Khamisi Rashid (siyo majina halisi ya mdau) lakini ameanza kwa kueleza moja ya tatizo kubwa katika mfumo wa ngumi ukiondoa kesi ya Mwamakula na Azam Media ni urasimu uliotengenezwa na wakuzaji (mapromota) katika kupata mikataba ya udhamini wa haki za matangazo.

“Ukiangalia suala la hili namna linavyoenda ni mbegu mbaya ambayo ilipandwa na wakuzaji wenyewe kwa sababu ndiyo wateja wakubwa wa  mdhamini na wala siyo chama cha ngumi za kulipwa.

Wakuzaji ndio wanapeleka pendekezo ‘proposal’ la mabondia gani wacheze kwenye pambano lake na kiasi gani cha fedha apewe kwa ajili ya kuendesha jambo husika ambayo ndiyo chanzo cha migogoro mingi kwenye mchezo huo.

“Tatizo kubwa lilikuwa hilo, jambo li;lilosababisha urasimu kubwa mkubwa wa kuangalia nani ndiye anayeweza kutimiza matakwa ya msingi ingawa wakati fulani walitoa kwa wakuzaji ambao walikuwa na kashfa nyingi na kusababisha kuharibu mapambano yenyewe.

“Unaona lile pambano la kwanza la Hassan Mwakinyo namna mzozo uliozuka au pambano lingine ambalo limefanyika mwaka huu lakini shida ikawa ndiyo ipo vilevile kwa sababu aliyepewa jukumu alikuwa tatizo na mambo yakavurugika.

Hayo yote ndiyo yamesababisha kesi za ajabu kuzuka na hata ukiangalia kesi ambayo imewafanya wasitishe kutoa huduma imekuwa ya mtindo huo na bado kumekuwa na madai mengi katika jambo hilo, naamini yatakwisha ila mikakati bora lazima ijengwe.


Nini kifanyike?

Mwanaspoti liliongea na mdau mwingine mkubwa ambaye hapa anatajwa kwa majina ya Emmanuel George ambaye ameanza kwa kutaka kumalizwa kwa kesi hiyo ambayo inaelezwa imekatiwa rufaa.

“Kitu cha kwanza ni kumaliza kesi iliyokatiwa rufaa halafu baada ya hapo Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa TPBRC wanatakiwa kuja na mkakati mkubwa wa mradi wa muda mrefu wa kujenga mchezo wa ngumi.

“Hawa TPBRC kwanza wanatakiwa kuja na mpango ‘project’ mkubwa na endelevu ambao utakuwa mwanga mzuri wa kupunguza haya mambo ya urasimu na udalali uliopo kwa sasa.

“TPBRC kupitia Baraza la Michezo la Taifa wanatakiwa kukaa na mdhamini mkubwa wa haki za matangazo ya runinga na kisha wao kuingia nao mkataba wa moja kwa moja wa haki za matangazo mchezo huo labda kwa miaka mitano ambao thamani yake ni bilioni sita.

Lakini mkataba huo, malengo yake ni kugawa miezi 11 ya mwaka ambayo mdhamini anaonyesha mapambano ya mchezo husika kisha kazi ya mkuzaji gani anapata nafasi ya kupewa hiyo haki ya pambano kubwa, inabaki kwa TPBRC na mdhamini husika.

“Hapa TPBRC atakachotakiwa kufanya ni kuandaa sheria au kanuni kwa wakuzaji (promota) ambao hawazidi 50 lakini nafasi ya mdhamini kwa mwaka ni maonyesho 11 pekee.

“Kanuni ambayo itahitaji mkuzaji kupata pambano kubwa kwa mwaka lazima kwanza awe na uwezo wa kuweka ‘bond’  labda ya shilingi milioni 35 kwa mwaka ambayo inakuwa kwenye akaunti muda wote.

“Lakini  kanuni iwaeleze wakuzaji lazima kufanya mapambano manne na moja kati ya hayo ndiyo yatapata udhamini wa haki za matangazo ambao thamani yake itategemea na watavyokuwa wamekaa kati yake, TPBRC na mdhamini wa haki za matangazo.

“Lakini itasaidia kwa wakuzaji kujua ni wakati gani anakuwa na pambano kubwa ambalo litakuwa na haki za matangazo ya runinga kwa mwaka ambayo itamsaidia kuweza kujipanga kutafuta mapema wadhamini wengine watakaosimamia mambo mengine.

“Mara nyingi uthibitishwaji umekuwa ukichelewa kufanyika kwa sababu mbalimbali lakini ikitumika njia hiyo itasaidia wakuzaji wengi kupata wadhamini wakubwa wengi kwa wakati husika na kuweza kufanya mapambano makubwa kwa ukubwa.

“Lakini faida nyingine itapunguza mlolongo wa mdhamini wa haki za matangazo kupokea ‘propasal’ nyingi ambazo zimekuwa zikitajwa ni sehemu ya migogoro mingi inayotokea mara kwa mara.

 “Ukiondoa suala hilo kumekuwa na kashfa nyingi za mabondia wengi kwenda nje kupigana kwa mapambano ya kuuza yaani wanaenda kuachia jambo ambalo siyo picha nzuri kwa taifa kuonekana taifa linazalisha mabondia wa kupigwa nje.

“TPBRC wanaweza kuweka sheria ya bondia akienda nje na kupigwa ndani ya mapambano matatu kwa mwaka basi anafungiwa kwenda nje kwa mwaka mzima hatorusiwa kupigana nje ya mipaka ya Tanzania.

“Hii itapunguza safari za mabondia ambao wamekuwa wakitajwa kuhusika na mapambano ya aina hiyo.

“Mwisho lazima TPBRC ihakikishe, idara na kamati itakazoziunda zinafanya kazi kwa ukubwa na umakini kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake ambayo itapunguza misukosukumo itajitokeza kwa sasa.”


TPBRC Wanasemaje?

Mwanaspoti limemtafuta Mwenyekiti wa muda wa Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa nchini TPBRC, Emmanuel Saleh ili kupata msimamo wa kamisheni hiyo.

Kiongozi huyo amesema: “Nikuambie, kwa sasa tunajipanga na muda ukifika tutatoa msimamo na mikakati yetu kila kitu kinachoendelea, nadhani tuvute subira,” alisema.

Saleh alisema wanajua kinachoendelea la wao kama wasimamizi wanajipanga kabla ya kuja na kauli yao ya mikakati  gani ifanyike ili kuzirudisha ngumi kwenye nafasi yake.