Prime
Aucho: Injini ya Yanga inayozeeka na utamu wake

Muktasari:
- Hata hivyo, nyota huyu wa kimataifa wa Uganda, ufundi bado upo na ubongo wake amekuwa mhimili mkubwa katika kikosi cha Yanga tangu alipojiunga na timu hiyo msimu wa 2021/22 akitokea Misr Lel Makkasa SC ya Misri, licha ya kuonekana umri unasonga.
DAKTARI wa mpira. Ndiyo jina maarufu kwake kutokana na umahiri wake katika kuituliza timu licha ya umri kumtupa mkono.
Hata hivyo, nyota huyu wa kimataifa wa Uganda, ufundi bado upo na ubongo wake amekuwa mhimili mkubwa katika kikosi cha Yanga tangu alipojiunga na timu hiyo msimu wa 2021/22 akitokea Misr Lel Makkasa SC ya Misri, licha ya kuonekana umri unasonga.
KIUNGO MUHIMU
Kiungo huyo mkabaji fundi ni mmoja wa wachezaji muhimu Yanga kiasi inaonekana anapokosekana utofauti unakuwepo uwanjani.
Eneo la kiungo katika timu hiyo limejaa watu wakiwamo Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua, Clatous Chama katika ushambuliaji, huku eneo la ukabaji wakiwamo Salum Abubakar 'Sure Boy', Duke Abuya, Jonas Mkude, huku wenye uhakika wa namba ni Aucho na Mudathir Yahya.
Aucho amekuwa panga pangua katika kikosi cha Uganda 'The Cranes' na tangu ajiunge na Yanga alianza kucheza sambamba na Yanick Bangala ambaye amemwacha kikosini na hadi sasa ni muhimili mkubwa na amekuwa bora licha ya kuwepo na ushindani.
Anasifika kwa uwezo wake wa kutuliza dimba la kati na kutoa pasi za uhakika, ubora huo umewafanya mashabiki na wadau wa soka kuamua kumpachika jina la utani kwa kumwita 'Daktari'.
Ana uwezo pia wa kupunguza mashambulizi yanayokwenda upande wao akisaidia mabeki wanaoongozwa na nahodha msaidizi Dickson Job na Ibrahim Hamad 'Bacca', na amekuwa bora kwenye eneo hilo la kulinda kuliko kutoa pasi za mwisho za mabao.

HANA MPINZANI
Aucho ambaye hana mambo mengi nje ya uwanja, umuhimu wake umeonekana kutokana na kukosekana kwa mbadala wake hali inayosababisha mashabiki kumwona ni wa kipekee na hana mshindani kwenye nafasi anayocheza huku wakiona timu ikiyumba kila anapokosekana.
Ujio wa nyota Mkenya, Abuya ulionekana kama ungempa changamoto Aucho lakini ameishia kukaa benchi na amekuwa akiwapisha yeye pamoja na Mudathir.
Pia kuna Mkude ambaye alitokea Simba na ilionekana ndiye ambaye angempa changamoto Aucho kutokana na kucheza kwa ubora akiwa na kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, lakini ameendelea kukaa benchi na kushindwa kumng'oa Mganda huyo kutokea Jinja.
Sure Boy pia licha ya uzoefu mkubwa wa ligi kuu, amejikuta akitokea benchi au kutocheza kabisa kutokana na uwepo wa Aucho.
Hata hivyo, amekuwa mtamu zaidi akianza na Mudathir na juu yao kukiwa na Pacome, Maxi Nzengeli na Azizi Ki wenye uwezo mkubwa wa kukaa na mpira, kupiga chenga na kusalisha pasi za mabao.
Nyota wengi wa eneo la kiungo wamekuwa wakihofia kwenda Yanga kutokana na uwepo wa Aucho na wanaona wanaenda kukaa benchi.
Hii ni kutokana na nyota wengine wa nafasi hiyo waliopo katika timu hiyo, kukaa benchi na Aucho ndiye anayeanza.
Katika nafasi yake unahitaji kufanya kazi ya ziada ili kulishawishi benchi la ufundi kukupa nafasi na muda mwingi wa kucheza kuliko yeye.

AUCHO VS BANGALA
Kabla ya ujio wa Aucho Yanga, kulikuwa na Bangala aliyeonyesha ubora mkubwa katika kikosi hicho msimu wa 2020/21 na kubeba tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu 'MVP kutokana na uwezo wake alioonyesha.
Hata hivyo, hakudumu kwenye nafasi moja kama kiungo na wakati mwingine alicheza kama beki kwa ubora tofauti na ambaye anamudu zaidi kucheza kiungo na anajua kukaba na ana pasi za uhakika.
KASI INAPUNGUA
Licha ya ubora alionao na akili ya soka, kasi yake uwanjani imeanza kupungua na hivyo kuipa kazi Yanga ya kusaka mbadala wake kwani mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu.
ASAKWE MBADALA WAKE
Yanga inatakiwa kutafuta mbadala wa Mganda huyo na atakayegombea naye namba na kumpa changamoto hasa kutokana na umri wake kuanza kumtupa mkono ili kumpunguzia majukumu mkongwe huyo ambaye mkataba wake unakaribia ukingoni.

WENZAKE WANAWEZA KUMRITHI
Wakati mkataba wake unakwenda ukikingoni na kasi yake kupungua, Yanga inahitaji mbadala wake na hapo ndipo linapokuja swali la nani atavaa viatu vyake.
Hata hivyo, inatakiwa ianze kuamini nyota wake waliopo ambao wamekuwa wakicheza endapo Aucho ataanzia benchi au akiwa na majeraha kabla ya kuamua kuingia sokoni kuleta mwingine.
Kuna Abuya, Mkudena Sure Boy viwango vyao ni vizuri na wakiaminiwa na kupewa muda wa kucheza watazoea na kuonyesha viwango vyao na kuondoa kasumba ya kumtegemea mchezaji mmoja.
Duke anaweza kupambana sana kwenye kukaba, huku Mkude na Sure Boy ni wazuri kwenye utoaji wa pasi sahihi kama ilivyo kwa Aucho.

MASHABIKI SALUTI
Kutokana na uwezo wake mkubwa, mashabiki wanaona kuna wakati hatendewi haki kwa kutopata tuzo na hivyo waliamua kumchangia pesa kutoikana na kumkubali nyota wao huyo ambaye hana makuu uwanjani.
Katika mchezo dhidi ya KenGold, ulipomalizika alizunguka uwanja kukusanya pesa zilizochangwa na mashabiki na aliwashukuru kutokana na kuona mchango wake kwenye timu.
Ni wazi kutokana na ubora wake, mashabiki hawatamsahau nyota huyu hata akija kiungo mwingine kwani alichowaonyesha ni zaidi ya burudani hadi kumbatiza jina la 'Daktari'.
Mchezaji mwingine atahitaji kufanya vitu vingi sana kwa usahihi ili mashabiki wengi wasahau kuhusu Khalid Aucho kwa sababu nguvu na ufanisi wake unaipa Yanga umbo zuri sana la uzuiaji.
HAWA WANGEWEZA, LAKINI...
Viongozi wa Yanga walitaka kuwashusha nyota wawili wa nafasi hiyo, na katika madirisha mawili yaliyopita walimsaka Adolf Mtasingwa, lakini dili hilo lilikwama kutokana na kuongezewa mkataba Azam na dirisha dogo walijaribu kwa Yusufu Kagoma ambaye naye ilishindikana baada ya Simba kuingilia na kumsajili na sasa anakipiga huko na wote walionekana wangeweza kuwa mbadala wa Aucho.
Sasa wadau na mashabiki wa Yanga wanasikilizia nini watakifanya viongozi wao mwanzoni mwa msimu ujao kama wataendelea kumbakisha Aucho pekee au wataongeza staa mwingine ambaye atampa changamoto mkongwe huyo.
Haimbwi sana kwenye mitandao ya kijamii, lakini miguu yake ndiyo inaimba uwanjani, hivyo mbadala au ongezo jipya linatakiwa kuwa sahihi.

TIMU ALIZOPITA
2009–2010 Jinja Municipal
2010–2012 Water
2012–2013 Simba
2013–2014 Tusker
2015–2016 Gor Mahia
2016 Baroka
2017 Red Star Belgrade
2017 OFK Beograd
2017–2018 East Bengal
2018–2019 Churchill Brothers
2019–2021 Makkasa
2021– Yanga
WASIFU WAKE
Kuzaliwa: August 8, 1993 (umri 31)
Mahali: Jinja, Uganda
Urefu: 1.80 m (5 ft 11 in)
Nafasi: Kiungo
Klabu: Yanga
Jezi : Namba 8