Arsenal, Man United... Huku kaja Jorginho, kule kaletwa Sabitzer ngoja tuone!

LONDON, ENGLAND.ARSENAL macho kwenye taji la Ligi Kuu England. Ni hivyo pia kwa wapinzani wao Manchester United, wanasikilizia itakavyokuwa kwenye vita hiyo.

Katika kufukuzia ubingwa, Arsenal chini ya kocha Mikel Arteta imeongeza silaha nyingine muhimu kwenye vita yao baada ya kumnasa kiungo wa Kitaliano kutoka kwa mahasimu wao wa London, Chelsea, Jorginho baada ya kulipa Pauni 12 milioni.

Ujio wa Jorginho kikosini unampa Arteta upana wa kutosha kwenye safu yao ya kiungo, ambapo kwa sasa Thomas Partey na Granit Xhaka watakuwa wameletewa mtu wa maana. Jorginho ataleta ushindani wa namba kikosi na hilo ndilo Arteta analotaka katika afya ya timu yake uwanjani.

Na mashabiki wa Arsenal wameanza kusubiri kwa hamu namna staa huyo wa zamani wa Napoli atakavyoingia kwenye chama. Itakuwaje?

Kocha Arteta amekuwa akitumia fomesheni ya 4-3-3 karibu msimu wote hadi sasa, lakini ujio wa Jorginho utaleta mabadiliko kidogo ya kimchezo, ambapo bosi huyo wa Arsenal sasa anaweza kuja na fomesheni ya 4-2-3-1.

Lakini, kumwingiza Jorginho kwenye kikosi hiyo ina maana mmoja kati ya Xhaka au Partey atalazimika kukaa nje. Na hilo linaonekana litamkuta zaidi Xhaka kwa kuwa Partey amekuwa mchezaji muhimu zaidi kwenye kikosi cha Arsenal na kipenzi. Hilo linaweza kuwa jambo gumu kwa Xhaka kutokana na kiwango chake cha msimu huu, lakini kwa Arteta itakuwa nzuri kwa sababu atakuwa na chaguo bora kabisa kwenye benchi lake.

Kwenye kikosi chao moto cha kwanza, golini atakuwa Aaron Ramsdale, atakayelindwa na mabeki Ben White, Gabriel, William Saliba na Oleksandr Zinchenko. Kwenye ukuta ule wa wakali wanne wa mbele, utaundwa na Bukayo Saka, Martin Odegaard, Gabriel Martinelli na Eddie Nketiah - ambaye amekuwa kwenye kiwango bora kabisa tangu alipoingia kikosini kuchukua nafasi ya majeruhi Gabriel Jesus.

Arsenal ipo kileleni kwa sasa ikiongoza ligi kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Manchester City na mechi ijayo kwenye ligi watakipiga na Everton, kisha Brentford na baadaye Man City kipute kitakachopigwa Emirates, Februari 15.

Huko Man United, kocha Erik ten Hag alikuna kichwa kufuatia kuumia kwa kiungo wake, Christian Eriksen na hapo akaangia sokoni kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili kunasa saini ya kiungo mpya kuja kuziba pengo.

Ten Hag amemnasa Sabitzer kwa mkopo, ambaye bila ya shaka atakuja kuunda kombinesheni matata na Mbrazili Casemiro kwenye kuimarisha sehemu hiyo ya katikati ya uwanja. Ujio wa Sabitzer kikosini, utamfanya Fred na Scott McTominay kuendelea kukaa kwenye benchi.
Hata hivyo, Fred ndiye anaonekana kumvutia zaidi kocha Ten Hag, hivyo kama ataamua kumweka benchi Sabitzer, ataanza na Mbrazili huyo katika kombinesheni ya Wabrazili wawili kwenye eneo la kiungo.

Kuhusu ishu ya kuziba pengo la Eriksen, Ten Hag alisema kuhusu Sabitzer: “Nadhani hataziba pengo kwa sababu kila mchezaji ni tofauti, ana mambo yake na namna yake tofauti ya uchezaji - lakini hiyo haina maana hatafanikiwa. Haina kificho Christian Eriksen alikuwa akileta viwango vya juu kwenye kikosi chetu na hiyo ni ngumu kupata mbadala, yale madhara yake anayosababisha kwenye goli la wapinzani anapokuwa na mpira.”

Kwa kumpanga Sabitzer na Casemiro kwenye sehemu ya kiungo, kocha Ten Hag ataendelea kucheza fomesheni yake pendwa ya 4-2-3-1, ambapo kwenye safu ya mabeki, kipa ataendelea kuwa David De Gea, ambaye atalipwa na Luke Shaw, Raphael Varane, Alesandro Martinez na Aaron Wan-Bissaka, wakati kwenye fowadi ya miamba hiyo ya Old Trafford - Bruno Fernandes kwenye Namba 10, huku Marcus Rashford upande wa kushoto na kulia ni Anthony na kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati atasimama Mdachi, Wout Weghorst.

Man United imeshinda mechi 11 kati ya 13 za mwisho ambapo Ten Hag alitamba na fomesheni hiyo ya 4-2-3-1, Eriksen akihusika uwanjani. Wanatarajia kuendeleza hilo wakiwa na huduma ya Sabitzer, ambapo ndani ya mwezi huu miongoni mwa mechi zao watakipiga na Barcelona kwenye Europa League.

Mechi za Februari za Arsenal
-Februari 4 vs Everton (ugenini)
-Februari 11 vs Brentford (nyumbani)
-Februari 15 vs Man City (nyumbani)
-Februari 18 vs Aston Villa (ugenini)
-Februari 25 vs Leicester City (ugenini)

Mechi za Februari za Man United
-Februari 4 vs Crystal Palace (nyumbani)
-Februari 8 vs Leeds United (nyumbani)
-Februari 12 vs Leeds United (ugenini)
-Februari 16 vs Barcelona (ugenini)
-Februari 19 vs Leicester City (nyumbani)
-Februari 23 vs Barcelona (nyumbani)
-Februari 26 vs Brentford (nyumbani)