Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Arajiga, wengine 74 waamuzi CHAN 2024

Muktasari:

  • Unapotaja waamuzi bora Tanzania kwa sasa, hutaacha kumtaja Arajiga aliyezaliwa mkoani Manyara, Julai 3, 1991, akiwa ana familia yenye mke na watoto watatu, ambapo amejizolea umaarufu ndani na nje ya mipaka ya nchi kutokana na uchezeshaji wake.

Zikiwa zimesalia siku 12 kabla ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN), Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewatangaza rasmi waamuzi watakaochezesha michuano hiyo.

Katika orodha hiyo yenye jumla ya majina 75, Tanzania inawakilishwa na Ahmed Arajiga wa Manyara na Ally Hamdani Saidi kutoka Mtwara, ambapo michuano ya fainali hizo zinatarajiwa kutimua rasmi vumbi kuanzia Agosti 2 hadi Agosti 30, 2025.

Tanzania ni wenyeji wa mashindano haya makubwa Afrika kwa wachezaji wa ndani kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, ambapo kupitia makala haya, Mwananchi linakuletea wasifu wa waamuzi Arajiga, Hamdani na wengine maarufu kutokana na rekodi zao.


AHMED ARAJIGA

Unapotaja waamuzi bora Tanzania kwa sasa, hutaacha kumtaja Arajiga aliyezaliwa mkoani Manyara, Julai 3, 1991, akiwa ana familia yenye mke na watoto watatu, ambapo amejizolea umaarufu ndani na nje ya mipaka ya nchi kutokana na uchezeshaji wake.

Kwa misimu miwili mfululizo, mwamuzi huyo ametwaa tuzo ya refa bora wa Ligi Kuu Bara, huku mechi ya 'Kariakoo Derby', kati ya Yanga na Simba zikimpa heshima zaidi katika majukumu yake, kutokana na kusimamia weledi wa kutafsiri vyema sheria.

Arajiga alianza kuchezesha mechi ya watani wa jadi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la FA, Julai 25, 2021, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, ambapo Simba ilitwaa taji kwa kuifunga Yanga bao 1-0, la Taddeo Lwanga.

Baada ya hapo akachezesha nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) iliyopigwa Mei 28, 2022, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ambapo Yanga iliifunga Simba bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Feisal Salum 'Fei Toto'.

Katika Ligi Kuu Bara, Arajiga alicheza mechi mbili za watani wa jadi, ambapo zote Yanga ilishinda, ikianza na mabao 5-1, Novemba 5, 2023, kisha ikaibuka tena na ushindi wa 2-1, zilipokutana Aprili 20, 2024, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. 

Arajiga alipata beji ya uamuzi ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mwaka 2022, ambapo kuanzia hapo amekuwa ni miongoni mwa waamuzi bora, mzoefu na mwenye ustadi wa kuzitafsiri na kuzisimamia vyema sheria 17, za mpira za miguu.

Kiwango hicho bora cha Arajiga kimempa fursa ya kuchezesha mechi kadhaa za kimataifa kwa mashindano ya ngazi ya klabu na timu za taifa.

Mechi yake ya kwanza ya kimataifa ilikuwa ni Septemba 10, 2022, iliyozikutanisha ASAS ya Djibouti na AS Kigali ya Rwanda katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika iliyomalizika kwa miamba hiyo kukosekana mbabe baada ya kulazimishana suluhu.

Kiwango chake kizuri cha uchezeshaji hakina shaka kimelishawishi Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kumteua pia kuchezesha fainali hizi za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN) zitakazoanza kurindima Agosti mwaka huu.

Jmbo la kufurahisha ni kwamba kutakuwa na waamuzi watatu wa kike ambao ni  Bouchra Karboubi kutoka Morocco na Shamirah Nabadda raia wa Uganda, huku waamuzi wasaidizi wakiwa ni Diana Chikotesha (Zambia) na Atezambong Fomo Carine (Cameroon) ambaye ni mmoja kati ya waamuzi wanawake wenye uzoefu wa kutosha kuchezesha mechi kubwa.


ALLY HAMDANI

Mwamuzi mwingine wa Tanzania aliyetutoa kimasomaso katika fainali za CHAN mwaka huu, ni Ally Hamdani Said kutoka Mtwara ambaye hivi karibuni alijumuishwa katika mashindano ya kombe la Afrika (AFCON) chini ya umri wa miaka 20, zilizofanyika Misri.

Hamdani alikuwa ni mwamuzi pekee kutoka Tanzania aliyehusika katika fainali hizo zilizofanyika Misri kuanzia Aprili 27 hadi Mei 18, 2025, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kupata mafunzo ya CAF ya kuwajengea uwezo zaidi katika taaluma hiyo.

Mwamuzi huyo wa pembeni, alizaliwa Juni 22, 1996, huku akianza uamuzi rasmi mwaka 2009, katika kituo cha Twalipo Temeke jijini Dar es Salaam, ambapo baada ya kusota kwa muda mrefu alipandishwa daraja kutokana na kiwango bora alichoonyesha.

Hamdani alianzia Ligi Daraja la Kwanza (FDL), kwa sasa ni Ligi ya Championship, kisha baada ya miaka sita alipandishwa ili kuchezesha Ligi Kuu Bara na waliokuwa waamuzi, wakiwemo, Israel Nkongo, Leslie Liunda, Soud Abdi na Samwel Mpenzu.

Mwamuzi huyo alianza kuchezesha rasmi Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2019-2020, ambapo amekuwa mahiri katika uchezeshaji wake na kujizoelea umaarufu mkubwa wa kupata nafasi katika mechi kubwa hapa nchini zikiwemo za watani wa jadi Yanga na Simba.

Ubora wake ulimfanya kupata rasmi beji ya FIFA mwaka 2023, ambapo shauku ya kusimamia vyema weledi katika majukumu yake uwanjani yamemfanya kuendelea kuaminiwa na kupewa nafasi mbalimbali, jambo ambalo kama Tanzania tunaendelea kujivunia.


DAHANE BEIDA

Mwamuzi huyo kutoka Mauritania, amekuwa na matukio mengi yenye utata huku hivi karibuni akikumbukwa alipochezesha mechi ya fainali mkondo wa pili ya Kombe la Shirikisho la Afrika, kati ya Simba iliyotoka sare ya bao 1-1 na RS Berkane kutoka Morocco.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan Complex visiwani Zanzibar Mei 25, 2025, Simba ilikosa taji baada ya kupoteza Morocco mabao 2-0, huku ikishuhudiwa nyota wa kikosi hicho cha Msimbazi, Yusuph Kagoma akipewa kadi nyekundu.

Beida aliyezaliwa Desemba 31, 1991, alipata rasmi beji ya FIFA mwaka 2018, huku akikumbukwa sana pia msimu wa 2023-2024, ambapo alikataa bao la aliyekuwa nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki dhidi ya Mamelodi Sundowns katika Ligi ya Mabingwa hatua ya robo fainali.

Beida anakumbukwa kwa tukio la Aprili 5, 2024 lililozua gumzo baada ya shuti la Aziz Ki alilopiga dakika ya 58 dhidi ya Mamelodi waliokuwa wenyeji wa mechi ya pili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa huko Afrika Kusini.

Katika mechi hiyo, licha ya mpira kuonekana kudundia ndani, lakini refa huyo alikataa bao baada ya kwenda kujiridhisha kwenye VAR na kusababisha kutoka suluhu (0-0), kufuatia kushindwa kutambiana Dar es Salaam na Yanga kutolewa kwa penalti 3-2.

Katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia iliyofanyika mwaka huu Marekani na Chelsea kuchukua ubingwa huo, Beida alikuwa miongoni mwa waliochezesha mechi kadhaa ikiwemo ya hatua ya makundi kati ya Inter Milan ya Italia na Urawa Reds ya Japan Juni 21.


ABONGILE TOM

Mwamuzi huyo kutoka Afrika Kusini alizaliwa Desemba 16, 1991 ambapo alipata rasmi beji ya FIFA mwaka 2020, akionyesha kiwango kizuri na kuchaguliwa kusimamia mechi mbalimbali, ikiwemo mashindano ya CHAN yaliyofanyika mwaka 2022, Algeria.

Mwaka 2023, Tom alikuwa ni miongoni mwa waamuzi wawili kutoka Afrika Kusini walioingia makubaliano ya kimkataba na CAF, akichezesha Kombe la Dunia la vijana chini ya umri wa miaka 20 mwaka 2023 na michuano ya African Football League mwaka 2023.


ISSA SY

Sy aliyezaliwa Julai 22, 1984 nchini Senegal, ni miongoni mwa waamuzi maarufu waliochezesha mechi nyingi na kubwa za CAF, zikiwemo Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Kombe la Shirikisho Afrika na ile ya michuano ya African Football League.

Mwamuzi huyo, alianza kupata beji ya FIFA mwaka 2015, amejizoelea umaarufu mkubwa katika mashindano mbalimbali, ambapo ni mahiri ndani na nje ya mipaka ya Senegal, jambo lililowavutia tena CAF kuendelea kumuamini pamoja na umri wake mkubwa akisimamia upande wa VAR.


ATCHO RIERRE GHISLAIN

Mwamuzi huyo anakumbukwa na mashabiki wa Simba hivi karibuni wakati alipochezesha mechi ya mkondo wa kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo kikosi hicho cha Msimbazi kilichapwa na RS Berkane ya Morocco mabao 2-0, Mei 17, 2025.

Atcho aliyezaliwa Gabon Oktoba 10, 1992, alipata beji ya FIFA mwaka 2018, akichezesha michuano mbalimbali, ikiwemo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho Afrika, CAF Super Cup na African Football League iliyofanyika mwaka 2023.

Siyo mwamuzi ambaye mashabiki wengi watampenda kwa kuwa anatajwa kuwa mmoja kati ya wale wenye maamuzi ya utata, lakini akiwa na hasira sana kwenye maamuzi yake, anatajwa kuwa mmoja kati ya waamuzi wenye uwezo wa juu wa kumwaga kadi.


WAAMUZI WA KATI

Waamuzi wa kati ni Ahmed Arajiga (Tanzania), Adissa Abdoul Raphiou Ligali (Benin), Messie Jessie Oved Nvoulou (Congo), Kpan Clement Franklin (Ivory Coast), Malala Kabanga Yannick (DR Congo), Ahmed Nagy Mosa Mahmoud (Misri), Tsegay Teklu Mogos (Eritrea), Jammeh Lamin (Gambia), Nyagrowa Dickens Mimisa (Kenya), Ahmed Abdulrazg (Libya), Diakhate Ousmane (Mali), Milazare Patrice (Mauritius), Loutfi Bekouassa (Algeria), Diouf Adalbert (Senegal), Jelly Alfred Chavani (Afrika Kusini), Aklesso Gnama (Togo), Melki Mehrez (Tunisia), Lucky Razake Kasalirwe (Uganda), Vincent Kabore (Burkina Faso), Brahamou Sadou Ali (Niger), Brighton Chimene (Zimbabwe), Mefire Abdou Abdel (Cameroon), Bouchra Karboubi (Morocco), Shamirah Nabadda (Uganda), Kech Chaf Mustapha (Morocco) na Houssam Benyahya (Algeria).


WAAMUZI WASAIDIZI

Ally Hamdani Said (Tanzania), Ngila Guilain Bongele (DR Congo), Lucky Kegalogetswe (Botswana), Sanou Habib Judicael Oumar (Burkina Faso), Emery Niyongabo (Burundi), Rodrigue Menye Mpele (Cameroon), Amaldine Soulaimane (Comoros), Alao Salim (Benin), Fasika Biru Yehualashet (Ethiopia), Jawo Abdul Aziz (Gambia), Addy Roland Nii Dodoo (Ghana), Mwangi Samuel Kuria (Kenya), Joel Wonka Doe (Liberia), Nassiri Hamza (Morocco), Yacouba Abdoul Aziz (Niger), Dieudonne Mutuyimana (Rwanda), Omer Hamid Mohammed Ahmed (Sudan), Wael Hanachi (Tunisia), Ronald Katenya (Uganda), Eleyeh Robleh (Djibouti), Ettien Eba Medard (Ivory Coast), Abeigne Ndong Amos (Gabon), Sirak Samuel (Eritrea), Malondi Chany (Congo), Adel Abane (Algeria) na Diana Chikotesha (Zambia).

Kwa upande wa wakufunzi kuna Mohammed Guezzaz (Morocco), Janny Sikazwe (Zambia), Evarist Menkouande (Cameroon), Mohamed Houssein Ali (Djibouti) na Boubaker Hannachi (Tunisia).


WAAMUZI UPANDE WA VAR

Katika VAR, kuna Mahmoud Ashour (Misri), Dahane Beida (Mauritania), Lahlou Benbraham (Algeria), Bamlak Tessema Weyesa (Ethiopia), Samir Guezzaz (Morocco), Hamza El Fariq (Morocco), Issa Sy (Senegal), Atcho Prierre Ghislain (Gabon), Daniel Lareya (Ghana), Abongile Tom (Afrika Kusini), Yasir Abdalaziz (Sudan), Viana Letticia (Eswatini), Maria Rivet (Mauritius), Akhona Zennith Makalima (Afrika Kusini), Jermoumi Fatiha (Morocco), Ghorbal Mustapha (Algeria), Stephen Yiembe (Kenya) na Atezambong Fomo Carine (Cameroon).

Katika orodha ya CAF yenye majina ya watu 75, waamuzi wa kati ni 26, waamuzi wasaidizi 26 na wakufunzi 5, huku upande wa VAR wakiwa 18.

Morocco ndiyo nchi iliyotoa watu wengi kwenye orodha hiyo ambao ni saba, ikifuatiwa na Algeria (6), kisha Cameroon (4), huku wenyeji Tanzania ikiwa na wawili tu, wakati Kenya na Uganda zinazoshirikiana kuandaa zikiwa na watatu kila mmoja.

Fainali hizo za CHAN 2024 zitashirikisha timu za taifa kutoka nchi 19, ambapo ufunguzi wake ni Agosti 2, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ikizikutanisha wenyeji Tanzania dhidi ya Burkina Faso zinazotokea kundi la B.

Mbali na mechi ya ufunguzi, CAF imepanga fainali itachezwa kwenye Uwanja wa Kasarani Kenya, Agosti 30 kuwania taji hilo, huku ile ya kuwania mshindi wa tatu itachezwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, uliopo huko Uganda, Agosti 29, 2025.

Kundi A mechi zake zitachezwa kwenye Uwanja wa Kasarani, zikishirikisha Kenya, Morocco, Angola, DR Congo na Zambia, huku kundi B zikichezwa Dar es Salaam, zikiundwa na Tanzania, Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mechi za kundi C ambazo zitachezwa Uganda, zitashirikisha Uganda, Niger, Guinea, Afrika Kusini na Algeria, huku kundi D ambalo mechi zake zitapigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, litashirikisha Senegal, Congo, Sudan na Nigeria.

Mashindano ya CHAN 2024 yatafuatiwa na ya AFCON 2027, ambapo Tanzania itakuwa tena mwenyeji, ikishirikiana na Uganda na Kenya.