Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ALLY KAMWE: Namshawishi Mayele arudi, 5-0 za Simba zilinitesa

Muktasari:

  • Wakati mwingine unaweza kupokea taarifa za mambo fulani na usijue kwa nini zinakuja kwako na sio kwa wengine, kumbe ndio maandalizi hayo unayoyapitia kuhusu kesho yako.

KUNA muda kwenye maisha unajiwekea mipango yako au kudhania sehemu fulani inawahusu watu wa aina tofauti na wewe kumbe haiko hivyo.

Wakati mwingine unaweza kupokea taarifa za mambo fulani na usijue kwa nini zinakuja kwako na sio kwa wengine, kumbe ndio maandalizi hayo unayoyapitia kuhusu kesho yako.

Lakini, pia yapo maneno ambayo huwa tunayasema kutokana na wakati husika au hisia ya jambo fulani, bila kujua kuwa mdomo unaweza kuumba kila tunachokitamka bila kujali ulikisema lini.

Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, kijana aliyeanzia uandishi wa habari za michezo kabla ya kuibukia katika nafasi aliyo nayo.

ALI KAMWE AFUNGUKA KABLA YA KUTANGAZWA KWAKE YANGA, HUYU NDIO ALITAKIWA KUWA OFISA HABARI

Mwanaspoti ilifunga safari hadi zilipo ofisi ya Klabu ya Yanga na kukutana na Ally, na kulieleza gazeti hili kuwa aliwahi kusema atakuwa katika nafasi ya uongozi ndani ya timu hiyo kwa sababu tu ya hasira za ushabiki.

Huku akiweka wazi kuwa katika nafasi hiyo Yanga ilishafanya makubaliano na mtu mwingine akiwa ni mwanamke, ambaye alikuwa rafiki na mshauri wake katika maisha ya kawaida, lakini mambo yakabadilika ghafla.

Ungana na Mwanaspoti ili ufahamu ilikuaje kuhusu nafasi ya ofisa habari kuwa yeye na sio yule wa awali na pia aliwezaje kuwa na ushabiki na Yanga huku akifanya kazi ya michezo inayokataza kuwa na upande wowote, bila kusahau masuala ya maisha nje ya kazi na uhusiano wa kimapenzi ulivyomtesa.


ALIVYOINGIA YANGA

Kamwe anasema kabla yake Yanga ilishafanya makubaliano ya kila kitu na mtu mwingine katika nafasi hiyo, lakini alikataa ndipo likatolewa tangazo na hakutaka kufanya maombi.

"Huyu mtu alikuwa mwanamke na mimi nilikuwa mshauri wake kabisa kuhusu yeye kwenda Yanga na nilikuwa najua kila kinachoendelea. Siku moja akaniambia hayuko tayari kwa sababu kuna presha kubwa na anaamini kuwa mimi ndio mtu sahihi, ila nilimkatalia," anasema.

"Nilimkatalia kwa sababu nilishajiona niko vizuri kwenye eneo langu la uchambuzi na niliamini nitapata mafanikio, ila siku moja tupo kazini nikamuuliza Ali Mayai kuwa nafaa kweli kuwa ofisa wa Yanga, akaniambia alitaka kuzungumza nami kuhusu hilo.

"Kuniamini kwake kulinipa hamasa nikaamua kutuma maombi, Mungu akasaidia japokuwa nilichelewa ila riziki ikawa upande wangu. Naamini siku moja tutakuwa na ofisa habari mwanamke kwa sababu sitakuwepo kwenye nafasi hii milele, hivyo ni maombi yangu kwa Mungu Yanga iweke historia hiyo japokuwa tuna viongozi wa kike ila wanakwepa sana majukumu haya ya kuongea."


REDIO NA YANGA

Msemaji huyo anasema baba yake alikuwa akiishabikia Simba, lakini haikumkaa moyoni, ndipo siku moja aliisikia mechi ya kwanza redioni dhidi Mamelodi Sundowns na Yanga.

"Mimi ni mshabiki mtiifu kabisa wa Yanga kila mtu ana tukio lake la kwanza lililomfanya awe na mapenzi na timu husika," anasema.

"Familia yetu baba alikuwa Simba, kwa hiyo alikuwa anatununulia jezi na kutupeleka uwanjani, ila mimi sikuvutiwa sana

Siku moja nasikiliza mpira redioni wachezaji ni kina Edibily Lunyamila mechi ikatoka 3-3 na Mamelodi, ugumu wa ule mchezo ukanifanya niikubali Yanga."


UANDISHI VS USHABIKI

Kuhusu ishu ya uandishi dhidi ya ushabiki, Kamwe anasema ushabiki ulitangulia kabla ya kazi, lakini havikuwahi kuingiliana huku akisema haiwezekani mfuatiliaji wa michezo asiwe na timu anayoshabikia.

"Kwanza ukweli mchungu ni kwamba waandishi wote wa michezo huwa wana timu zao kati ya Simba na Yanga. Kwa hiyo mtu yeyote lazima awe upande mmojawapo, ila taaluma inatuzuia," anasema.

"Lakini mtu alikuwa akisikiliza au kusoma kazi zangu, alikuwa hawezi kujua niko upande gani. Nakumbuka mechi ya FA Yanga anafungwa mabao manne na Simba niliumia, nikashindwa kujizuia, nikaondoka na kifaa cha sauti cha ofisi baada ya kuchambua."

JEZI SH200,000

Kamwe anasema kuwa zipo jezi nyingi ambazo zimewahi kutolewa na Yanga kutokana na msimu, lakini ipo moja ambayo aliinunua akiwa mwandishi wa habari kwa sababu ya mapenzi.

"Kuna jezi Yanga ilitolewa ni ya kijani kama ina vimajengo majengo na kola, pili ni ile ya kimataifa ina jina la mdhamini 'Haier' msimu wa kwanza kabisa alipoingia Yanga kama daki buluu na ya tatu ni hii ya sasa ya rangi ya dhahabu.

"Sasa hii jezi ya kijani wakati nikiwa mwandishi kuna ambayo niliipenda sana nikaamua niinunue na kuivalia ndani tu baadae nilipopewa hiki cheo nikajikuta nilishaipoteza...basi nilinunua kwa shabiki baada ya kuitafuta na kuikosa. Siku moja ndio nakutana na mtu akasema anayo na ameshaivaa nikamuomba aniuzie kwa gharama yoyote.

"Alipokubali tu nikampatia Laki Mbili, lakini akaniambia kuwa ipo nyumbani nikamuongezea Elfu Hamsini amlipe bodaboda akaichukue, nikaipata na sasa ninayo. Ni kumbukumbu nzuri kwangu na bado ni jezi bora zaidi," anasema Kamwe.

MECHI ILIYOMUUMIZA

Ofisa huyo wa habari wa Yanga akizungumzia mechi iliyomtesa moyoni anasema, "tuliwahi kufungwa na Simba mabao 5-0. Nilikuwa niko uwanjani nimekaa chini naona tunavyopigwa, nimetoka hapo nina hasira sana nikawaza nifanyaje. Tukatembea mpaka Jangwani nikasikia mechi imeuzwa.

"Kwa hiyo niliondoka na hilo kuwa kuna viongozi wameuza mechi nikasema ipo siku nitakuwa kiongozi wa hii timu na hiki kisasi tutakilipa. Wanajua ninaofanya nao kazi nilishawahi kuwaambia, kwa hiyo tulivyokuja kuwalipa ilikuwa sherehe kubwa sana kwangu na kila Novemba 5 ni maadhimisho."


ASICHOSAHAU

Akizungumzia kile asichoweza kukisahau maishani mwake, Kamwe anasema wakati anaanza kazi alikuwa na moto wa maneno kwa sababu anaufahamu mpira vizuri jambo lililomfanya kuanza vibaya.

"Nilitaka kuwaonyesha watu kwamba najua, nikapiga suti yangu safi ya buluu. Ratiba inaonyesha mechi inayofuatia ni Yanga na AL-Hilal na mimi ndio msemaji. Yanga inaonekana wadhaifu kwa Hilal, nikawasoma vizuri tukaja na msemo wa Mandonga 'tutawapiga kama ngoma', unajua ulimi unaumba kumbe jamaa wanajua Kiswahili wakasikia. Kwa hiyo wakati wanasalimiana wakawa wanawaambia kina Mayele kuwa ngoja tuone nani ngoma," anasema.

"Tukaanza kufunga sisi dakika chache wakatufunga mechi ikaisha sare ya 1-1, mechi ya pili tukapigwa Sudan nikajiona sina bahati. Tulipokutana na Club Africain katika Uwanja wa Mkapa ulikuwa hautabiriki nikakimbia mapema dakika ya 75."


HERSI NA MAKUNDI

Kamwe ana mengi ndani ya Yanga na hapa anazungumzia ishu ya hatua ya makundi klabu hiyo ilipotinga fainali msimu uleee wa Kombe la Shirikisho Afrika.

"Mechi na Club Africain tulienda kinyonge kwa sababu hatukuwa na uhakika wa kutoboa wakati tunafika mazoezi ya mwisho Bernard Morrison akamuona mtu anayemdai, akaanza kupigana basi nikajiona nimeanza kazi na gundu," anasema Kamwe.

"Usiku wa mwisho kuamkia mechi akaja Injinia Hersi, ile mechi aliyeibadilisha alikuwa yeye kabla hajaongea na timu akaongea na mimi akasema shida ni nini? Nikalalamika sana ila mwisho akaniambia kuwa hii ni kazi na sio rahisi, lakini anaelewa kwamba bado mimi ni mchanga.

"Kesho yake jioni kiongozi akaongea na wachezaji akasema hii mechi sio ya kushindwa, ila kama ikitokea hivyo kila mtu atashika hamsini zake. Asubuhi inayofuata akazungumza tena na kuongeza bonasi kwa wachezaji, basi Mungu akasaidia tukatinga makundi kwa kufunga 1-0. Nilielewa umuhimu wake anaposafiri na timu, mambo huwa ni mengi ukiwa nje huwezi kuelewa.

"Baada ya kushinda hapo Yanga ilianza kuuwasha moto kuanzia makundi mpaka fainali, huko kwenye ligi ndio balaa, ni kama mkosi ule ulitutoka."


BALAA LA MAYELE

Msemaji huyo anasema moja kati ya mastaa walioisaidia timu hiyo wakati huo hasa katika michuano ya kimataifa alikuwa straika Fiston Mayele.

"Mayele alikuwa anajiamini sana, tulivyotinga makundi tu mechi zote aliwaambia wachezaji wenzake wamletee mipira tu kazi iliyobaki atafanya yeye.

"(Mayele) sio mchezaji wa kucheza rafu wewe chapa anakuja tu... kwa hiyo mechi zilimalizika vizuri na tukatinga hatua ya fainali. Ujue Mayele ni mchezaji ambaye natamani hata leo arudi Yanga na ninamshawishi sana."


CHANGAMOTO

Ofisa huyo wa habari wa mabingwa wa kihistoria anasema kuwa shida inakuja sehemu moja kama sio mbili, kwani wengi wanaamini matokeo ya klabu ndio kila kitu na wanayahusianisha na idara zingine.

"Arsenal mpaka sasa ina miaka mingi haijachukua ubingwa wa ligi yao, lakini ukienda kutafuta klabu iliyofanya vizuri katika maendeleo ya soka la vijana na sehemu zingine ipo. Tanzania iko tofauti, timu inapokosa alama tatu kila kitu kinasimama. Watu wa masoko watashindwa kufanya kazi zao na kama kuna mkataba walitaka kusaini unaweza hata kusitishwa. Wadhamini watasema mnatafuta matangazo ya nini wakati hamshindi," anasema Kamwe.

"Kwa hiyo kama idara kuna vitu tunafanya na vinaangushwa wakati mwingine na mambo kama hayo inabidi tugeuke wote tuelekeze nguvu kwenye matokeo, lakini naamini tutatoka huko.

"Mfano katika idara ya habari toka tumeanza kushiriki kimataifa, jinsi watu wanavyofanya ni tofauti kabisa na sisi. Ujue tuna mtaji wa watu wanaopenda mpira, lakini toka nimeingia sijawahi kuona maofisa wa klabu zetu zinazoshiriki wakifuatilia vikao vya CAF ambavyo vinatoa elimu ya mambo hayo. Sasa hivi tunapambania lugha ya Kiswahili kutumika CAF."


MSIBA MZITO

Katika furaha wakati mwingine hujikuta huzuni inavamia ghafla na kuharibu utamu wa sherehe na hilo Kamwe pia lilimgusa katika tukio mojawapo kazini kwake.

Anasema tukio jingine ambalo hatalisahau ni kupata msiba akiwa nje ya nchi akiwa amesafiri na timu.

"Nilipata taarifa ya msiba wa mtoto wangu nikiwa safarini, alikuwa na miezi sita na binti ambaye nilipata mtoto ana asili ya Rwanda na Tanzania. Kwa hiyo akawa amepata mtihani mama yake pia alikuwa anaumwa sana Rwanda na hawezi kumuacha mtoto. Kwa hiyo anafika tu kwao ananitumia ujumbe mzazi wake amefariki, asubuhi akaniambia hali ya mtoto pia imebadilika.

"Ndani ya siku mbili nilimpoteza mama mkwe na mtoto, hivyo hata tukisema tusafirishe isingefaa au mimi ningeenda ningechelewesha tu msiba. Hivyo nikashauriwa niache tu mambo yaende nitoe tu baraka. Nilikuwa naingia chumbani nalia sana natoka nje najikaza tu. Mtandaoni nilikuwa naambiwa maneno ya hovyo na ukizingatia ni mgeni wa kazi, kwa hiyo ilikuwa ngumu kwangu."


UKARIBU NA AHMED ALLY

Unapomtaja Ahmed Ally mbele ya Kamwe ni watu wawili tofauti katika misingi ya kikazi, lakini mtaani ni washkaji na ni marafiki wa karibu.

Kamwe anasema kabla ya majukumu waliyo nayo walikuwa wakifanya kazi pamoja kama waandishi wa habari wa kituo kimoja cha redio na runinga.

"Sisi ni marafiki kabla na hiyo imetutengenezea kinachotusaidia mpaka leo kwa sababu tunaheshimiana na kuwa na mipaka hata ya utani wetu. Ahmedy alinitangulia kwenye hizi kazi za ofisa habari na wakati anakwenda aliniambia, nikamshauri kama rafiki. Kwa hiyo ilivyotokea kwangu pia akaniambia, ushauri ulionipa na wewe utumie.

"Kwa hiyo tunajua tulipotoka tangu kipindi hicho mpaka sasa. Hivyo Usimba na Uyanga umekuwa sio vita, ila utani unaoleta raha."


MAOKOTO BALAA

Kamwe anaweka anasema kipato anachokipata sasa ni kikubwa kuliko alivyokuwa mwanahabari na anashukuru kwa hilo.

"Huku kwa sasa kipato ni kikubwa na nimetimiza ndoto nyingi ambazo sikuwahi kuzifikiria. Yako mambo makubwa nimeyafanya kutokana na hii nafasi niliyopo. Shida ni kwamba sijazaliwa kujitutumua, napenda kuwa wa kawaida kwa sababu nimetoka kwenye maisha ambayo ilihitaji ujasiri kuvumilia dharau," anasema.


KUHUSU KUOA

Kila binadamu huwa ndoto nyingi maishani na kwa wengi kuoa ni miongoni mwa jambo ambalo hupanga litokee na Kamwe anasema amekuwa akikumbana na changamoto kwenye suala la ndoa na uhusiano ndio maana hataki kabisa na hana lengo hata kuwa na mwenza kwa sasa.

ALI KAMWE: SITAOA HADI NIFIKE MIAKA 55, MAHUSIANO NA HAMISA MOBETTO? HUU HAPA UKWELI

"Kuoa sio malengo yangu na nilishawahi kuoa, kwa hiyo naelewa ninachokisema. Kila mtu lazima atambue uimara na udhaifu wake. Mimi kwangu mahusiano ni udhaifu na yameshanishinda. Kwa hiyo bora niwe mnyonge kuliko kulazimisha nimeamua nitulie kwanza baadaye huko nitaoa nikiwa na miaka 55, nitaoa ili (ndoa) ikiniua nikiwa na (miaka) 59 basi mtajua ni magonjwa ya kiutu uzima."