Aliyosema Scholes juu ya Carrick yamgeukia
Muktasari:
- Scholes alibaki ameshtushwa kufuatia ukosoaji mkubwa uliomkumba baada ya chapisho lake hilo, kwa mujibu wa rafiki yake, Nicky Butt.
MANCHESTER, ENGLAND: KAMA ingekuwa Bongo basi ingekuwa rahisi kusema kwamba huo ni zengwe. Supastaa wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes ameshangazwa na kuvunjika moyo baada ya kukosolewa kuhusu ujumbe wake aliouandika mitandaoni kumhusu kocha wa sasa wa timu hiyo, Michael Carrick
Scholes alibaki ameshtushwa kufuatia ukosoaji mkubwa uliomkumba baada ya chapisho lake hilo, kwa mujibu wa rafiki yake, Nicky Butt.
Mkongwe huyo alizua mjadala baada ya United kufungwa na Newcastle United wiki iliyopita katika mechi ya Ligi Kuu England ugenini, ambapo katika ujumbe wa Instagram ambao baadaye aliufuta, aliandika kuwa mastaa wa United wamekuwa “wabaya sana**” katika mechi za hivi karibuni licha ya Carrick kupata matokeo mazuri.
Katika ujumbe huo, Scholes aliandika: “Michael bila shaka ana kitu cha kipekee… kwa sababu United wamekuwa wabaya katika mechi nne zilizopita… usiku mwema.” Pia aliweka emoji ya busu na kuandika jina la kiungo wa Newcastle United, Sandro Tonali likifuatiwa na alama ya moyo.
Baadaye Scholes alijitetea akisema ujumbe wake ulitafsiriwa vibaya, lakini inaonekana athari yake ilikuwa kubwa zaidi kuliko alivyotarajia.
Akizungumza juzi, Nicky Butt alieleza kwamba Scholes hakumaanisha neno “vibaya”, bali alimaanisha vinginevyo. Butt alisema kwenye mahojiano na Paddy Power kwamba watu wasiomfahamu Scholes binafsi wanaweza kudhani alikuwa akiponda mbinu ya mchezaji mwenzake huyo wa zamani ambaye amekabidhiwa ya kuifundisha United hadi mwisho wa msimu.
Alieleza kuwa Scholes alimaanisha kuwa Carrick ana bahati kama kocha, jambo ambalo mara nyingi ni muhimu kwa mafanikio ya kocha.
Butt alisema: “Nilipozungumza na Scholesy alisema, ‘kwa kweli siamini watu wamechukia vibaya kiasi hiki’. Ameshtuka na amevunjika moyo. Anampenda sana Michael Carrick kama rafiki, mchezaji mwenzake na kocha.”
SCHOLES: CARRICK HAKUKASIRIKA
Akizungumza kwenye podikasti yake The Good, The Bad & The Football, Scholes alisema alimwandikia Carrick ujumbe kumweleza kuwa hakumaanisha kumkosea heshima. Alisema: “Michael ni mmoja wa watu wazuri zaidi utakutana nao kwenye soka. Ndiye mtu wa mwisho ningependa kumkosea.”
Scholes pia alisema Carrick alimwambia hakukasirika na kwamba, watu walielewa vibaya juu ya kile alichomaanisha.
Alisema kuwa ingawa United hawajacheza vizuri katika mechi nne zilizopita, bado wanapata matokeo, jambo ambalo hata kocha wa zamani wa kikosi hicho, Alex Ferguson aliwahi kusema hutokea kwa timu kubwa – wakati mwingine bahati huwa sehemu ya ushindi.
WENGINE WAGAWANYIKA
Wachezaji wengine wa zamani wa kikosi hicho wanaonekana pia kugawanyika na wamekuwa wakijadili sana juu ya mwenendo wa mkongwe mwenzao Carrick katika suala la mbinu anazozitumia.
Gary Neville na Roy Keane wamekuwa wakihoji uwezo wa Carrick katika wiki za hivi karibuni, wakidai bado timu hiyo haijajipata ipasavyo licha ya kwamba inaendelea kupata matokeo mazuri uwanjani.
Hata hivyo, Patrice Evra na Rio Ferdinand wanamtetea kocha huyo wakisema ameivusha timu yao na kwamba, hivi sasa imegeuka kuwa gumzo na tishio kwa timu nyingi ambazo kabla ya kukutana nayo zimekuwa zikiumiza vichwa kukabiliana nayo.
Evra anasema anashangazwa na ukosefu wa sapoti kwa Carrick, akisisitiza kuwa anafanya kazi nzuri, huku akiwakumbusha wakongwe wenzake kuwa ni rahisi kukosoa ukiwa kwenye televisheni kuliko kufundisha timu kwa mafanikio.
MASHABIKI
Kwa upande wao, mashabiki wengi wa Manchester United wanaamini kwamba Carrick ameipatia timu hiyo kimbinu kwani matokeo inayoyapata siyo ya kubahatisha, hivyo asivunjwe moyo na maneno ya wachezaji wenzake wa zamani.
“Asibabaishwe kabisa. Unajua ni rahisi kupigana kuliko kunyamaza katika mazingira ya ukosoaji usio na maana kama huu. Fikiria kwamba timu ilikuwa haieleweki, lakini leo inaanza kupata matokeo mazuri kisha mnaponda. Hii haiwezekani,” aliandika shabiki mmoja katika mtandao wa X (zamani Twitter).
Shabiki mwingine alidai, “mbona wenyewe wameshindwa katika timu walizogusa kufundisha na sasa wamekalia kukosoa wenzao tu. Waache buana.”
Mwingine aliandika: “Kuna jambo la kujifunza, si bure. Haiwezekani mtu anakosoa jambo linalofanyika vizuri. Huyu mtu anapata ushindi, kazifunga timu zote kubwa alizokutana nazo. Iweje sasa wamshambulie?”