Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ALAA KUMBE! Kilichopo nyuma ya miwani ya vioo vyekundu wanayovaa mastaa England

MIWANI Pict

Muktasari:

  • Hivi karibuni, masupastaa wa Manchester City, straika wa mabao Erling Haaland na kiungo wa Pauni 100 milioni, Jack Grealish walionekana wakiwa kwenye mtoko huo wa miwani yenye vioo vya rangi nyekundu.

LONDON, ENGLAND: HABARI ya mjini kwa sasa kwenye Ligi Kuu England ni mastaa wake kuvaa miwani yenye vioo vya rangi nyekundu.

Hivi karibuni, masupastaa wa Manchester City, straika wa mabao Erling Haaland na kiungo wa Pauni 100 milioni, Jack Grealish walionekana wakiwa kwenye mtoko huo wa miwani yenye vioo vya rangi nyekundu.

Kwanini miwani yenye vioo vyekundu? Unaambiwa hivi, imefichuka kwamba miwani hiyo ina faida kubwa kiafya na hicho ndicho kinachofanya mastaa wa Ligi Kuu England kukimbilia kuvaa kwa wingi. Umekuwa mtindo.

Wakali hao wawili kutoka kwenye kikosi cha mabingwa wa England walionekana kwenye mtoko huo wakiwa kwenye ndege.

Na winga wa zamani wa Manchester United, anayekipiga kwenye kikosi cha Nottingham Forest kwa sasa, Anthony Elanga naye alionekana pia kwenye mtindo huo, akiwa amevaa miwani yenye vioo vyekundu.

Elanga alionekana kwenye mtoko huo wakati alipokwenda kuitumikia Sweden kwenye soka la kimataifa, ambapo alipigilia miwani ya vioo vyekundu.

Baada ya kuonekana kama umekuwa mtindo kwa mastaa wa Ligi Kuu England, ikatafutwa kwanini wachezaji hao wanakimbilia miwani yenye vioo vyekundu.

Kilichogundulika ni kwamba si mambo ya fasheni tu, bali miwani hiyo ina faida kubwa kiafya.

Ndiyo, kuna faida kubwa kiafya. Kinachoelezwa ni kwamba vioo hivyo vya rangi nyekundu vinaongeza homoni zinazojulikana kama melatonin mwilini.

MIWA 01

Na kazi kubwa ya homoni hiyo ni kwamba ina mchango mkubwa katika kumsaidia binadamu kupata usingizi mzuri na si ule wa kulala na kushtukashtuka.

Kiwango cha homoni hizo zinadaiwa mwili unapata chache sana wakati wa mchana wa jua kali na zinakuwa nyingi wakati jua linapozama. Hivyo kupigwa na jua sana kuna athiri mwili kutengeneza homoni hiyo kwa wingi na kusababisha tatizo la kupata usingizi mzuri.

Homoni hizo zinapokuwa nyingi kiasi cha kutosha inamfanya mtu kupata usingizi mapema na hivyo kulala kwa usingizi mzuri na kuufanya mwili kurudisha nguvu yake iliyopotea.

Elanga alisema: "Inanisaidia kulala. Ni muhimu kutunza macho na mwisho wako, hasa unapocheza mechi nyingi. Hii sio mitindo yangu kabisa."

Kiungo wa zamani wa Uholanzi, Edgar Davids, alionekana akiwa na miwani ya aina hiyo yenye vioo vya rangi nyekundu wakati anacheza, hasa kwenye fainali za Euro 2004.

Hata hivyo, staa huyo wa zamani wa AC Milan na Juventus, Davids alivaa miwani hiyo ya vioo vya rangi nyekundu kwa sababu tofauti kabisa.

Straika, Haaland aliwahi kufunguka na kueleza sababu za yeye kuvaa miwani hiyo yenye vioo vya rangi nyekundu, alisema: "Nadhani kulala ni kitu muhimu zaidi hapa duniani.

"Hivyo, kupata usingizi mzuri, vitu vya aina hiyo, miwani ya vioo vya rangi ya bluu vinazuia, vinazuia miale yote.”

MIWA 02

Kwa maana hiyo, Elanga, Haaland na Grealish si wachezaji wa soka wa kwanza kuvaa miwani yenye vioo vya rangi nyekundu.

Kiungo wa boli, Edgar Davids alivaa sana miwani ya aina hiyo, tena kwenye mechi. Lakini, gwiji huyo wa Kidachi alikuwa na sababu tofauti kabisa. Staa huyo, aliyewahi kuichezea Barcelona alipata tatizo la ugonjwa wa macho wa glaucoma, hivyo alihitaji kufanyiwa upasuaji kumaliza tatizo hilo na ndipo hapo alipoanza kucheza akiwa amevaa miwani. Davids alianza kuvaa miwani hiyo mwaka 1999 na tangu wakati huo ilibaki kuwa staili yake, alionekana hivyo uwanjani kwenye mechi, akicheza akiwa na miwani ya vioo vyekundu.


Kuhusu Melatonin

Utafiti unafichua kwamba homoni ya melatonin kwenye mwili wa mwanadamu inamsaidia kupata usingizi mzuri wakati wa kulala. Umuhimu wa usingizi umesababisha hadi baadhi ya watu kuhitaji kumeza dawa za kuwasaidia kulala, jambo ambalo wakati mwingine huwaletea madhara kiafya.

Lakini, sasa kumbe homoni hiyo inaweza kupatikana tu kwa kuvaa miwani yenye vioo vya rangi nyekundu vinapoza mwanga wa jua na kutengeneza homoni hizo kwa wingi mwilini. Ukosefu wa usingizi ni hatari kwa afya, wakati mwingine inaweza kusababisha kisukari au kuongeza homoni ya njaa na kumfanya mtu awe anakula kupita kiasi. Wanasayansi bado wanapambana kutambua umuhimu wa melatonin, licha ya kuelezwa kwamba inasaidia kulala.

Wanasoka wanahitaji kulala vizuri ili kufanya miili yao kujijenga upya baada ya uchovu wa mazoezi au mechi.