AKILI ZA KIJIWENI: Ubelgiji imenipa majibu mazuri

BAADA ya kuingia pale Casablanca, Morocco usiku, asubuhi yake ndugu yangu nikasogea zangu katika jiji maarufu la Rabat.

Ukibisha hili itakuwa umeamua tu kujitia uchizi maana pale kuna watu wawili ambao walikuwa mastaa wakubwa hapa Tanzania tena siku chache zilizopita ambao ni kocha Nasreddine Nabi na winga Bernard Morrison.

Watanzania wote tunaofuatilia habari za michezo tunafahamu kuwa hao wawili wako zao pale Rabat wakiitumikia FAR Rabat hivyo jiji hilo lazima liwe linatajwa na wengi hapa nchini mara kwa mara.

Sasa kule Rabat nikafikia hoteli moja ya kiandamizi inaitwa Mercure ambayo ni kati ya hoteli kubwa katika lile jiji.

Kumbe katika ile hoteli ilikuwa imefikia timu ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 20 ya Ubelgiji ambayo Jumapili ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Morocco na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Baada ya kuwaona wachezaji nikataka kujaribu kufanya nao mahojiano ili wanipe mawili matatu ambayo yanaweza kuwa na faida kwa Tanzania lakini uongozi wao ukanikatalia na ukanipa sababu mbili.

Sababu ya kwanza ni kwamba vijana wale ni wadogo bado hawawezi kufanya mahojiano ya kushtukizwa ambayo hayakuwekwa katika mpangilio wa safari yao kwani wanaweza kuzungumza kitu ambacho kitaleta shida ama kwao au kwa timu.

Lakini jambo la pili ni kwamba pale ni hotelini sio mahali pa kufanyia mahojiano na badala yake ilipaswa iwe uwanjani au katika eneo maalum lililotengwa kwa ajili hiyo.

Baada ya majibu hayo, yale maswali niliyokuwa najiuliza kwamba kwa nini wenzetu wana nidhamu ya kuzungumza, yakapata majibu kwamba ni jambo wanaloandaliwa tangu chini.