AKILI ZA KIJIWENI: Simba, Azam atakayefungwa leo aanze kusahau ubingwa
KWENYE Uwanja wa CCM Kirumba leo kuna moto utawaka wakati miamba miwili ya soka nchini, Simba na Azam FC itakapoumana katika mechi ya Ligi Kuu Bara.
Mechi hii katika miaka ya hivi karibuni imepewa jina la utani la ‘Mzizima Derby’ ikimaanisha kwamba timu hizo mbili zinatoka hapa Dar es Salaam ambapo zamani paliitwa Mzizima.
Hii ni mechi hasa na naamini dakika 90 zitakuwa za aina yake kwani timu hizo mbili zimekuwa na ushindani mkubwa pindi zikutanapo na kila moja ina wachezaji wazuri ambao wanaweza kuamua matokeo wakati wowote.
Hapana shaka utakuwa ni mchezo wa kisasi kwa kila upande kwani kwa Simba, inataka kumaliza unyonge wa kutopata ushindi kwa muda mrefu dhidi ya Azam FC kwani haijapata ushindi dhidi yao katika misimu miwili mfululizo iliyopita.
Kwa Azam FC nayo inataka kupunguza idadi ya michezo iliyopoteza dhidi ya Simba pindi zikutanapo kwenye ligi kwani historia inaonyesha kuwa yenyewe imepata vipigo vingi kutoka kwa wapinzani wao hao kulinganisha na idadi ambayo wao wamepata ushindi.
Ushindani mkubwa wa mechi hiyo naamini utatokana na nafasi ambayo kila timu ipo kwenye msimamo wa ligi pamoja na idadi ya pointi ambazo imekusanya hadi sasa ambapo Azam FC iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 31 wakati Simba iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi 29.
Hesabu za kimpira zinaonyesha kuwa timu ambayo itapoteza leo itakuwa na nafasi finyu ya kutwaa ubingwa kutokana na aina ya washindani wake wa mbio za ubingwa pamoja na msimamo utakavyokuwa baada ya mechi ya leo.
Simba ikipoteza maana yake itakuwa nyuma ya Yanga na Azam kwa pointi tano huku ikiwa na idadi sawa ya mechi na Yanga ambayo imekuwa haiangushi pointi kizembe.
Azam ikipoteza itawapa nafasi Simba kuwa sawa nao huku wapinzani wao hao wakibaki na mechi moja mkononi kama itakavyokuwa kwa Yanga hivyo haitokuwa rahisi kutoboa mbele ya wakubwa wawili ambao wamekuzidi pointi huku wakiwa na mechi mkononi.