AKILI ZA KIJIWENI: Mayele anataka noti tu sio kingine

MABAO yake msimu huu yameshangiliwa sana na Yanga katika Ligi Kuu Bara na labda itokee miujiza asiwe mfungaji bora kwani sioni uwezekano wa anayemfuatia kufunga mabao saba katika raundi mbili zilizobakia.

Fiston Mayele, mabao yake yameshangiliwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambako Yanga haikutoboa kuingia katika hatua ya makundi lakini mwamba akafumania nyavu mara saba.

Haya akahamia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambako kashaweka nyavuni mara saba na kuna uwezekano finyu asiibuke mfungaji bora wa mashindano hayo kwani anayemfuatia kwa ukaribu, Ranga Chivaviro tayari timu yake

Marumo Gallants imetolewa katika mashindano hayo.
Kwani unadhani ni mashindano hayo tu ambayo Mayele ameleta balaa? Hapana kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kule Singida wakati kila mmoja akiamini mechi yao dhidi ya Singida Big Stars ingeamriwa kwa dakika za nyongeza au mikwaju ya penalti, jamaa akaingia akitokea benchi, akaiweka timu mgonghoni na kufunga bao pekee la Yanga lililoipeleka Yanga, fainali.

Huku mtaani kila kona unayokutana na Mwanayanga anatamba na Mayele, kona nyingi za Afrika leo hii zinamtazama na kumfuatilia bwana Mayele.

Wahenga wanasema papa anakaangwa na mafuta yake mwenyewe ndicho nakiona kinaweza kutokea kwa Mayele. Wakati Yanga wanapomshangilia anapowatesa makipa na mabeki wa timu pinzani wanapaswa kujiandaa kisaikolojia na kifedha.

Huyu Mayele hayo mabao yote anayofunga na shughuli anayoifanya ana jambo lake moyoni ambalo sio lingine bali ni kutafuta fedha.

Watu wasidhani atashawishika kubakia Yanga kwa sababu tu watu wanamuimba kila siku na kumshangilia bali kwa kupewa fungu kubwa la fedha kuanzia la kusaini mkataba mpya, mshahara pamoja na bonasi nyingine.

Kuna timu zenye pesa nyingi kwa sasa zinamnyemelea huyo mchezaji ambazo huwa haziogopi kutumia mzigo ikiwa kuna mchezaji zinamuona anafaa kusajiliwa katika vikosi vyao.

Hizo ndio tishio kwa Yanga hivyo kama inamhitaji Mayele iandae mzigo wa kutosha hasa. Kwa daraja alilotengeneza, sio jambo la ajabu kusikia hata kuna timu imemuwekea mezani ofa ya mshahara wa zaidi ya Sh 50 milioni kwa mwezi ambao Yanga italazimika tu kumpa au ikishindikana haitokuwa na nguvu ya kumbakiza.