AIBU TUPU KUAHIRISHWA MECHI YA SIMBA NA YANGA

Muktasari:

KITENDO cha kuahirishwa kwa pambano la Simba na Yanga lililokuwa lichezwe jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kumewafanya wadau wa soka kucharuka na kudai ni aibu kubwa kwa soka la Tanzania, kwa mechi kuahirishwa kienyeji kwa sababu za kisiasa, huku wengine wakisema kuna kitu nyuma ya kilichotokea.

KITENDO cha kuahirishwa kwa pambano la Simba na Yanga lililokuwa lichezwe jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kumewafanya wadau wa soka kucharuka na kudai ni aibu kubwa kwa soka la Tanzania, kwa mechi kuahirishwa kienyeji kwa sababu za kisiasa, huku wengine wakisema kuna kitu nyuma ya kilichotokea.

Wadau mbalimbali wakiwamo wachezaji wa zamani, makocha sambamba na mastaa wamelizungumzia tukio hilo wakisema linaoonyesha ndani ya TFF na Bodi ya Ligi (TPLB) kuna mambo yanayohitaji kuondolewa ili soka lisonge mbele.

Mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, George Masatu alisema: “Yanga wamefuata taratibu za ligi zinavyoelekeza, muda ulikuwa saa 11 mechi ianze, wamefika na wamefanya ‘warm-up’ na kusubiri dakika zinazotakiwa.

“Wametoka baada ya kumaliza taratibu za uwanjani na kwenda vyumbani, wapo sahihi maana sababu ya msingi haijawekwa wazi, uamuzi ama kama kuna adhabu kwa Yanga kuondoka uwanjani itajulikana baadaye.

“Ni aibu kubwa sana kwa wasimamizi wa soka nchini kutozingatia kanuni na sheria za ligi zinavyoelekeza, maana zipo wazi kwamba kama kuna mabadiliko yoyote yafanyike kabla ya saa 24 za mechi, kwanza ni lazima mabadiliko hayo yatolewe kwa maandishi sio kupigiana simu.”

Kocha wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa amesikitishwa na wasimamizi wa ligi kutofuata kanuni zinavyoelekeza na kubadilisha ratiba kwa namna wanavyotaka.

“Kubadilisha muda wa mechi ghafla kama hakuna sababu za msingi sio jambo linaloleta afya kwenye mpira, kwani hata kwenye timu yangu iliwahi kunitokea, huwa inaumiza sana, kiukweli hawazingatii wala kujali kanuni zinasemaje.

“Yanga wameingia uwanjani kwa mujibu wa kanuni inavyoelekeza kuwa timu ifike saa 1.30 kabla ya mechi kuanza, Bodi ya Ligi na TFF walikuwa na muda wa kufanya mabadiliko jana (juzi) kama kuna jambo la msingi lilikuwepo na sio kutoa taarifa muda mfupi kabla ya mechi kuanza.

“Ikumbukwe kwamba mashabiki waliingia uwanjani mapema sana, wengine wakiwa na watoto wadogo, kuna suala la kufuturu hilo wanaliangalia vipi, watu wameingia hasara kwa kulipa viingilio, ni aibu sana,” alisema Mkwasa.

“Wamesema kuwa wamepokea taarifa kutoka serikalini, je serikali inafanya mambo yake ghafla namna hiyo, nadhani nao wana muda ambapo wangetoa taarifa toka jana (juzi). Yanga wameheshimu ratiba na muda uliopangwa ingawa labda wangetumia busara tu kusubiri muda walioamua wenye mpira, maana haiwezekani ukae na wachezaji muda mrefu baada ya kupasha.”

Mchezaji wa zamani wa Simba, Azizi Nyoni alisema: “Yanga haikupaswa kutoka uwanjani kama timu ilikuwa imejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo, soka letu tunalijua wenyewe namna linavyoendeshwa.

“Haya mambo hayajaanza miaka ya sasa, hata enzi zetu mambo kama haya yalikuwepo sema tu watu waliona kama vitu vya kawaida.”

Upande wake Emmanuel Gabriel, nyota wa zamani wa Simba na Stars alisema: “Kisheria Yanga si ipo sahihi? Hata mimi nililifikiria sana jambo hili, TFF wamechemka aisee.

“Hadi hapa nashindwa kuzungumzia, ina maana asubuhi hawakukaa kikao (pre match meeting)? Hayo yote yalikuwa yazungumzwe hapo na sio vinginevyo.”


MITANDAONI KWALIPUKA

Mwanasiasa maarufu hapa na mbunge wa Bumbuli aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa: “Kwa kutambua kwamba inawezekana mamlaka za mpira zisifanye maamuzi sahihi, umewekwa utaratibu wa malalamiko. Kama timu haikubaliani na maamuzi ya mamlaka husika, inaweza kucheza ‘under protest’ huku ikiwa imeweka malalamiko kwa maandishi, kama kanuni zinavyoeleza.”

Mchambuzi wa soka kutoka Wasafi Fm, George Ambangile aliandika: “Muda wa kifo tu ndio unacheleweshwa, lakini lazima leo mmoja atachinjwa ...sijui nani huyo, eti wadau nani anakufa leo kwa Mkapa baada ya futari.”

Edo Kumwembe, mchambuzi wa Mwanaspoti na Wasafi FM alituma picha ya mchekeshaji Joti kisha aliandika: “Joti sisi watu wa mpira hautuwezi...mpira wetu unachekesha kuliko wewe.”

Mchambuzi wa kituo cha redio cha E Fm, Oscar Oscar ‘Mzee wa Kaliula’ aliandika hivi: “Timu zote zinapaswa kugomea haya mabadiliko ya kiholela, mpaka sasa Simba na viongozi wake ndo wamepost mabadiliko hayo kwenye kurasa zao rasmi, lakini Yanga hawajasema chochote, katika hili viongozi wangu wa Simba wameonyesha kutokututhamini sisi mashabiki tulioingia uwanjani kuanzia asubuhi, labda kwa kuwa wao wanaingia na ving’ora hawajui shurba ya hili jua kuitafuta saa 11. Mpira wa miguu ni kwa ajili ya wanamichezo na siyo mali ya kiongozi yeyote wa kisiasa. Timu zote zinatakiwa ziheshimu mashabiki au washinikize mechi ichezwe muda uliopangwa au isichezwe kabisa.”

Mchezaji wa zamani wa Taifa Stars na mchambuzi wa E Fm, Jemedari Said Kazumari aliandika: “Wadau mmepokeaje taarifa hii kutoka TFF? Weka comment yako hapa chini. Mimi nasema hii ni hali ya kukosa mpangilio (disorganized). Kuna dharura gani? Vinginevyo mambo yanafaa kutabirika na kwenda kwa mtiririko uleule.

“Halafu kubadilishwa kwa lisaa hiyo sawa, lakini saa 8 tuko kiwanjani tunaambiwa mechi ni saa 1 jioni masaa zaidi ya manne.

“Kiwanja hakina miundombinu ya kupata vitu muhimu kama vyakula (futari) kwa waliofunga, mazingira hayawezi pia kukupa wasaa mzuri wa kukaa hapa kwa hayo masaa manne. Kiwanja chetu ni kuja kuona soka unaondoka.”

Msaani wa muziki wa Bongo Fleva ambaye ni shabiki maarufu wa Arsenal na Yanga, Madee aliandika: “Kwa Mkapa tayari...Yanga wawili na kimkia kimoja..mechi yetu ni saa 11:00. Saa moja tunajua ni Manchester City na Chelsea.”

Zitto Kabwe, kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo pamoja na John Heche wa Chadema wamefagilia uamuzi wa Yanga waliouita wa kijasiri na kutaka waliohusisha kulichezea na kulivuruga pambano hilo iwe wizarani au TFF na Bodi wachukuliwe hatua kali kurejesha furaha ya mchezo wa soka nchini, sawa na alivyotoa kifagio Boniface Jacob, aliyewahi kuwa meya wa Ubungo aliyedai yeye ni Simba damu kama kina Heche na Zitto, lakini amefagilia walichokifanya Yanga.

Ahsateni Wananchi ahsanteni watani wa jadi.