Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afya ya akili inavyowatesa mastaa

Muktasari:

  • Mahojiano yaliyofanywa na Mwanaspoti kwa madaktari, wanasaikolojia na baadhi ya waathirika yanaonyesha baadhi ya dalili na namna za kukabiliana nazo kabla ya kuathirika.

KUTOKANA na mabadiliko ya kimaisha kunachangia watu wengi kujikuta wakikumbana na changamoto ya afya ya akili, kitaalamu inashauriwa kutibu dalili mapema kabla ya tatizo kuwa kubwa.

Mahojiano yaliyofanywa na Mwanaspoti kwa madaktari, wanasaikolojia na baadhi ya waathirika yanaonyesha baadhi ya dalili na namna za kukabiliana nazo kabla ya kuathirika.

Kati ya dalili zilizotajwa ni kuhisi upweke, kelele kichwani, wasiwasi bila sababu, kuonewa na wakati mwingine kuanzisha ugomvi. Kuhusiana na wachezaji madaktari wameshauri timu kuajiri wanasaikolojia ili wahusika wakikumbana na changamoto iwe ni rahisi kuzifanyia kazi, ila kwa zile ambazo hazina uwezo wa kuwalipa watalaamu hao, waweke utaratibu wa kuwapeleka kliniki angalau mara moja kwa mwezi.

Baadhi ya wahanga wa changamoto hiyo ambayo Mwanaspoti imezungumza nao, wamefafanua namna walivyojinasua kabla hawajaathirika sana.

Msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Ferooz Mrisho aliyetamba na wimbo wa Starehe anasema tangu akiwa mdogo alikuwa anakumbwa na changamoto mbalimbali zilizompa msongo wa mawazo, lakini aliwahi kutibu tatizo kabla halijawa kubwa.

Jambo la kwanza alilolifanya ni kukubaliana na kila hali katika maisha mfano miaka ya nyuma baada ya kutoa wimbo wa Starehe jina lake lilikuwa linatajwa kila kona, hivyo kipindi cha ukimya wake kila mtu alisema lake na isingekuwa kuthibiti mawazo ingemletea shida. “Kitu kilichonisaidia nasoma sana vitabu kama ‘Managing Stress’ ambavyo vinatoa maelekezo nini ukifanye ili kuepukana na hali hiyo, vitabu vya mashairi, siwezi kuvitaja vyote ni vingi sana, hivyo vilinisaidia kuona kila kitu ni kawaida,” anasema Ferooz.

“Kama kuna kitu kigumu wanapitia mastaa wengi ni mashabiki kutaka kuishi maisha yao.

Ikiwa una moyo mdogo unaweza ukachizika mfano mimi siogopi kupanda bajaji, bodaboda na navaa nguo zilizopo ndani ya uwezo wangu sijali watasema nini.

“Kupitia hilo nipo kwenye mchakato wa kuandaa kitabu cha maisha yangu ambacho kitawasaidia wengine kutoogopa maisha kupanda na kushuka kitu kinachowatesa wengi na kujikuta wanakumbana na afya ya akili.”

Kuna wasanii ambao walijotokeza kukiri kuwahi kukumbwa na tatizo hilo kama msanii wa vichekesho, Gladness Kifaluka ‘Pili wa Kitimutimu, msanii wa Hiphop, Rosa Ree aliyefanya mahojiano na chombo cha habari nchini.

Msanii wa filamu, Julius Charles anasema akiwa na miaka 16 huko Mwanza, kutokana na urefu wake ambao jamii ilikuwa haimuoni kama mtu wa kawaida, ulimfanya ajifungie ndani zaidi ya wiki tatu, na aliyekuwa anampa moyo ni mama yake mzazi aliyemtaka awe anatembea mitaani azoeleke. “Mama yangu mzazi na kupenda michezo kumenisaidia kujiona wa kawaida hadi nimepata nguvu ya kuingia katika mahusiano ambayo niliyaanza nikiwa na miaka 27 na sasa miaka 30,” anasema.

Ukiachana na hao kuna wachezaji mojawapo ni beki wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars, Idrisa Said Rajabu ambaye yupo kituo cha Mikwambe, Twangoma, Kigamboni, Dar es Salaam (SOBA) kwa uangalizi wa afya.

Rajabu alipata changamoto ya afya ya akili akiwa na AFC Leopards ya Kenya katika mazoezi ambapo alionekana kuchanganyikiwa hadi kuufanya uongozi kuwasiliana na ndugu zake waliowahi kumuuguza Hospitali ya Mirembe - Dodoma na Butimba, lakini bado hali yake ikawa inajirudia.

Staa wa zamani wa Simba, Kagera Sugar, Ruvu Shooting na Taifa Stars, Christopher Edward anasema: “Nimekuwa nikikumbana na kejeli kutoka kwa watu mbalimbali wanaoniambia nimefeli maisha nikiwa Simba kutokana na starehe za wanawake bila kujua ukweli halisi.

“Mtu anaweza akakukuta umekaa sehemu unakunywa kinywaji sehemu za starehe ili kupunguza mawazo anaanza kukukejeli mbele za watu. Kinachonifanya niwe imara huwa namsikiliza sana mwanamuziki Linex katika mahojiano yake mbalimbali anachosema,” anasema Edo. “Linex anasema watu wanapaswa kukubali maisha yanapanda na kushuka na kuikubali hali, usipokuwa na uwezo wa kupanda bodaboda panda daladala hayo ndio maisha yako halisi. Maneno yake yamekuwa yakinipa moyo ipo siku nitafanikiwa.”

Beki wa zamani wa Azam na Taifa Stars, Said Morad anasema baada ya kusitishiwa mkataba na timu hiyo 2015/16 akiwa anategemea kupata kipato cha kuendesha maisha alijikuta anapitia changamoto ya afya yake, lakini aliidhibiti hali hiyo mapema.

“Japokuwa nilipata timu zingine baada ya hapo, ila haikuwa rahisi kwangu. Nilikumbana na changamoto ya familia, ndugu, jamaa na marafiki, ambayo ilinifunza kujua maisha halisi nje na kile ambacho wanakupendea, maana wale ambao niliowasaidia asilimia kubwa ndio waligeuka maadui,” anasema.

“Kilichonisaidia kurejea haraka katika hali yangu ni baada ya kupata mtoto nikaona napaswa kujituma kwa ajili ya kumtengenezea maisha yake. Nikawa napuuzia vitu ambavyo vinaniumiza, ila wengi wanapitia changamoto ya afya ya akili wanaogopa kujiweka wazi.”


MADAKTARI

Akizungumzia suala hilo, Daktari wa Mtibwa Sugar, Lawrance Mushi anasema unapozungumzia afya ya akili maana yake ni utimamu wa mtu kiakili, japo inapoonekana kuna upungufu kiakili sababu kubwa inayochangia kwa wachezaji ni kutokana na matokeo mabaya ya timu.

“Zipo sababu nyingi kwa mfano matokeo yasiyoridhisha, majeraha au maumivu ya muda mrefu. Hii inatokana na mchezaji kuwaza kupitiliza kwa sababu ni kazi anayoitegemea maishani mwake,” anasema Dk Lawrance.

Anasema changamoto nyingine kwa mchezaji ni matatizo ya kifamilia kwani miongoni mwao huathiriwa na hali inayosababisha kushuka hata kwa viwango uwanjani.

“Kazi yoyote inayohusu kikundi cha binadamu ni lazima kuwe na wataalamu wa akili. Hata ukienda ofisi nyingi utakuta hawa watu wapo kwa sababu wanasaidia kumjenga mchezaji au mtu wa kawaida tu anayekutana na kadhia ya namna hiyo,” anasema.

Lawrance anasema licha ya baadhi ya timu kutokuwa na uwezo wa kuajiri wataalamu wa saikolojia, lakini ni muhimu kuwepo na watu wa aina hiyo, kwani husaidia  kumjenga na kumrejesha katika hali ya kawaida, hasa inapotokea suala hilo.

“Sio lazima awe ameajiriwa na klabu kwa sababu sio wengi wanaoweza kumlipa. Wanaweza kumkodi wanapofanya kliniki kuliko kumkosa kabisa. Madaktari pia husomea saikolojia ingawa tatizo linapokuwa kubwa ni lazima mtaalamu mwenyewe awepo.”

Daktari wa Singida Black Stars, Shima Shonde anasema zipo sababu nyingi zinazochangia kutokana na kitendo cha kubadilisha aina ya mazingira ya kuishi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“Kiufupi ni vitu vingi kutokana na mazingira anayoishi. Kwa mfano timu nyingi zinataka mchezaji muda mwingi awe kambini, ingawa ukiangalia sehemu aliyotoka labda alikuwa sana huru, sasa hiyo inaweza kumsababishia changamoto hilo,” anasema.

Dk Shonde anasema suala lingine linalochangia ni mfano mchezaji aliyeonyesha kiwango bora akiwa na Pamba Jiji na baada ya hapo Simba au Yanga zikamtaka na kujiunga na timu mojawapo, kisha akashindwa kuendeleza alichokuwa nacho.

“Inapofika hatua ya namna hiyo ni lazima benchi la ufundi liwe karibu sana na yeye, ni lazima limwambie kwa nini hachezi au ni vitu gani vinasababisha asicheze. Hii itasaidia kumpa motisha ya kupambana kuliko kumuacha pekee.”


BOHARI YA DAWA (MSD)

Bohari ya Dawa (MSD) imefafanua kuhusiana na afya ya akili.

MSD inaeleza visababishi vya changamoto hiyo ni mchanganyiko wa mambo mengi kama sababu za kurithi, msongo wa mawazo ya kimaisha, mazingira na utamaduni unaoishi na matatizo ya afya yanayoathiri ubongo.

Imetaja aina za ugonjwa huo kuwa ni wasiwasi, magonjwa ya hali kama vile kuwa na huzuni sana (mfadhaiko) au shauku sana (wazimu), matatizo ya haiba na kushindwa kudhibiti mawazo na misukumo.


YANAYOCHANGIA

Saldin Kimangale, mwanasaikolojia ataja sababu akisema: “Hatuna takwimu zinazoweza kutuonyesha hali ipoje kwa upande wa wanamichezo. Kwa hivyo majibu yangu yataegemea zaidi kwenye vihatarishi na vichochezi; shinikizo la ushindi na matokeo, presha ya kupata matokeo mazuri ni kihatarishi kunako changamoto za afya ya akili, hasa wakishindwa na majeruhi na kuwekwa benchi, majeraha huathiri si tu mwili, bali pia huleta huzuni, hasira, na kupoteza mwelekeo wa maisha, na mara nyingi hupatiwa matibabu yamajeraha ya kimwili lakini majeraha ya kihisia yanachukuliwa kwa uzito mdogo.

Hata akikosa nafasi ya kucheza (akikosa namba) inaweza kumletea msongo wa mawazo na kujiona labda hawezi na michezo ni eneo lenye ukosoaji mbaya sana wa washabiki na mitandao ya kijamii, wanamichezo  hukumbana na matusi, kejeli, au shinikizo kwenye mitandao, jambo linaloweza kuathiri ustawi wao kisaikolojia; upweke, kujitenga na familia ni changamoto nyingine inayoweza kuhatarisha afya ya aki ya mchezaji, safari za mara kwa mara na ratiba ngumu huwafanya wakose uhusiano wa karibu wa kijamii na familia zao na kukosa muda wa kupumzika, moja ya mbinu za kuboresha afya ya akili ni kupumzika, michezo ni kama vita, kupumzika ji nadra sana, na mazoezi ya kupindukia huathiri mfumo wa neva, usingizi, na kuleta msongo wa kudumu.”


NINI KIFANYIKE

Wanamichezo na makocha wanapaswa kufundishwa kuhusu afya ya akili ili watambue dalili za changamoto, kuwepo na semina za mara kwa mara na ushauri nasihi ni muhimu.

Pia  klabu ziwe na wataalamu wa afya ya akili na wanasaikolojia wa michezo, zizingatie maendeleo binafsi katika michezo na mchakato badala ya matokeo ya mwisho kwa timu,  ratiba iwe na muda wa kupumzika, likizo na usimamizi mzuri wa mzigo wa mazoezi.

 Imeandikwa na Daudi Elibahati, Olipa Assa na Victoria Melkiad