ADEBAYOR: Huyu Samatta apewe heshima yake

Muktasari:

  • Adebayor aliyekuwa mjini Unguja, visiwani Zanzibar katika fainali za michuano ya kuwania Ubingwa wa Afrika kwa timu za Shule (ASFC) 2024 alifunguka juu ya Samatta na kutaka nyota huyo apewe heshima kwa kazi kubwa aliyoifanya kuitangaza Tanzania kupitia miguu, huku akistaajabisha na vipaji vya soka nchini.

WAKATI ombi la Mbwana Samatta kutaka kustaafu kuichezea timu ya taifa, Taifa Stars likisubiri baraka za Shirikisho la Soka nchini (TFF), nyota wa zamani wa kimataifa wa Togo aliwahi kuwika na klabu za Real Madrid, Arsenal, Man City na Spurs, Emmanuel Adebayor amemkingia kifua nahodha huyo wa Tanzania.

Adebayor aliyekuwa mjini Unguja, visiwani Zanzibar katika fainali za michuano ya kuwania Ubingwa wa Afrika kwa timu za Shule (ASFC) 2024 alifunguka juu ya Samatta na kutaka nyota huyo apewe heshima kwa kazi kubwa aliyoifanya kuitangaza Tanzania kupitia miguu, huku akistaajabisha na vipaji vya soka nchini.

Mwanaspoti lilifanya mahojiano maalumu na mshambuliaji huyo wa zamani wa Togo na kufunguka mambo kadhaa ikiwamo kukiri anachizishwa mno na nyimbo za miondoko ya singeli. Ebu tiririka naye...!


SAMATTA NA VIPAJI ADHIMU

Adebayor aliyenusurika katika tukio la timu ya taifa ya Togo kushambuliwa eneo la Cabinda Angola wakitokea Conmgo Brazzaville walipokuwa wakienda katika Fainali za Afcon 2010, amesema hakuwahi kujua kama Tanzania kuna vipaji vikubwa vya soka kama alivyovishuhudia katika fainali hizo za ASFC.

Ukiondoa vipaji vya wachezaji hao, alimtaja Samatta kwa kiwango alichokionyesha katika mataifa aliyocheza, anaona anastahili heshima mbele ya Watanzania, kwani amekuwa kioo cha kuitambulisha nchi yake ina vipaji vya soka.

“Angekuwa sio mchezaji mzuri asingeweza kucheza nje na timu kubwa kama Genk, Aston Villa, Fenerbahçe, Royal Antwerp na sasa PAOK. Hizi klabu zina wachezaji wakubwa na alikuwa akicheza, hilo ni jambo la kujivunia Watanzania,” anasema Adebayor na kuongeza;

“Samatta amelitambulisha soka la Tanzania, maana kiwango alichokuwa anakionyesha,kinafsiri nchi aliyotokea ina vipaji vikubwa.”


ISHU YA EMMANUEL EBOUE

Anamzungumzia mchezaji wa zamani wa ASEC Mimosas, Beveren, Arsenal, Galatasaray, Sunderland, Emmanuel Eboue ni mchezaji mwenye vituko na alikuwa rafiki yake.

“Muda wote anatamani mcheke, haruhusu makasiriko, pia ameacha funzo kwa vijana wengi, kujua namna ya kuishi na ustaa, ndio maana naona ipo haja ya kuwajenga hao watoto wawe na misingi mizuri,” anasema huku akikumbusha mwaka 2006  akiwa na timu ya taifa ya Togo wakishinda mabao 3-2 dhidi ya timu ya taifa ya Congo, wakapata nafasi ya kwenda kucheza michuano ya Kombe la  Dunia na kudai haisahaulika kwake.

“Kumbukumbu hii haitasahaulika maisha mwangu, nilifunga bao la kwanza dakika 40 na pambano lilkaisha kwa ushindi huo wa mabao 3-2, tukapata nafasi ya kwenda Fainali za Kombe la Dunia 2006 kule Ujerumani ilikuwa bahati kwani tangu hapo hatukuwahi kubahatisha tena, kushiriki michuano hiyo,” anasema.


YEYE NA SINGELI

Humwambii kitu kuhusiana na muziki wa singeli, kwani midundo yake inampa vaibu la kucheza na kuyafurahia maisha yake.

Anasema nje na singeli ni shabiki wa miziki ya Afrika, ambayo inazingatia tamaduni, anapoisikia ikipigwa haoni aibu kunyenyuka na kucheza akitaja baadhi yaka kama Misso Misondo na Amapiano.

“Wakati nipo na Abdi Kassim ‘Babi’ tukiwa kwenye kozi ya grass root, ulikuwa ukipigwa muziki wa Kitanzania una ladha tofauti, ulikuwa unaniona nikisimama na kucheza bila aibu, kwani ndio kitu kilichokuwa kikinipa raha,” anasema Adebayor na kuongeza;

“Kwa upande wa waimbaji wa Togo navutiwa sana na King Mensahana  kusikiliza muziki wake.”


ANFIELD KIBOKO

Adebayor anasema licha ya kucheza kwenye viwanja tofauti vya soka, lakini anautaja Uwanja wa Anfield unaotumiwa na Liverpool kuwa ndio bora kwake akitaja sababu ni shangwe wakianza kucheza zinakuwa mwanzo, mwisho.

“Nimecheza viwanja mbalimbali duniani ila Anfield ndio uwanja bora kwangu mashabiki wake wanashangilia bila kikomo, hali inayotufanya wachezaji kupambana zaidi ili kupata matokeo na pia nilikuwa najiona niko nyumbani nikicheza pale,” anasema Adebayor.


PROGRAMU ZA CAF

Kutokana na mafanikio makubwa, aliyoyapata enzi anacheza, inakuwa rahisi sana, watoto kumuelewa ushauri wake. “Ni zao la Afrika, nimefanikiwa kucheza timu kubwa mbalimbali, hakuna miujiza hapo, isipokuwa ni bidii, nidhamu na misingi sahihi, kwani soka halidanganyi. Anaongeza”Nimechaguliwa na Shirikisho la Soka Afrika(CAF) kama legendari, ili kuwapa uzoefu watoto, kujua maisha ya soka ni ya aina gani, ndio maana nafanya kwa moyo mmoja.”


SOKA NA UWEKEZAJI

Anasema ana uzoefu na mastaa wengi, wanaokula starehe, wakiamini wanaweza wakafa muda wowote ule, ila ajabu wapo wanaoishi kwa muda mrefu, wanaanza kuwasumbua wengine, wasiposaidiwa wanakuwa na malalamiko mengi.

“Hakuna kitu kibaya, wakati mastaa wanaponda maisha jamii inawatazama, inapotokea wakafilisika, wanaanza kuombaomba, wakinyimwa, inakuwa shida kuona hakuna anayewajali, ifikie hatua kuwafundisha mastaa wajao, kwamba hakuna mtu mwenye dhamana ya maisha yao, isipokuwa yapo mikononi mwao.

“Ustaa unakuwa na mambo mengi, wasipofunzwa mapema ukawajia ghafra, huko mbele wanaweza wakaharibu ndoto zao ama wakawa watu wa ajabu ajabu, ndio maana kuna haja Mashirikisho ya nchi mbalimbali,yawe na misingi thabiti kutengeneza mastaa wenye misingi sahihi.”

Anasema kupitia uchezaji wake, amejifunza vitu mbalimbali ambavyo anatamani awape ama kuwajenga vijana kwa kadri awezavyo, kuhakikisha wanakuwa watu wa kuigwa kwenye jamii. “Wenzetu wana watu wa saikolojia, ambao wanawajenga ikitokea majina yao yanakuwa makubwa, ngumu kuondoka kwenye mstari wa malengo,” anasema.

Ila anatoa angalizo kwa C|F akiitaka kuzingatia umri wa watoto ambao wanaibua vipaji vyao, ili huko mbele waweze kucheza kwa muda mrefu na kuondoka na matatizo ya kudanganya umri.

“Watoto wakianzishwa kwenye umri sahihi, hamtasikia udanganyifu wa mchezaji mara kesho anakutajia huu, siku nyingine anataja vingine, yanatokea hayo kulingana na misingi mibovu wanayotokea na kwa sababu wanakuwa wanataka mafanikio ya kimaisha wanakosa namna zaidi ya kudanganya.

“Misingi sahihi itawasaidia watoto wakija kukua watakuwa wanajielewa, tofauti na wale ambao umarufu na mafanikio yanakuja kwa ghafra, mwisho wao mara nyingi siyo mzuri, wanajikuta wanafanya sana starehe na kuishia maskini.”

Anasema soka halina njia za mkato, jambo ambalo analipongeza CAF, kuanza programu za watoto ambao, watakuwa mfano huko duniani.

“Nimeona pia warsha mbalimbali kama vile za marefa wadogo,makocha na nyinginezo nyingi hizi zitasaidia future ya mpira wa bara letu kwa sababu hawa Watoto wataanza kujiamini tangu katika umri hii nah apo mbeleni tutakuwa na marefa wazoefu tangu wakiwa watoto†Anasema.


SPECIAL ONE

Anasema katika maisha yake ya soka, hawezi kumsahau José Mourinho kwa sababu ya uwazi wake na kuwaamini wachezaji kutoka bara la Afrika, kisha kuwapa nafasi kwani huwa anasema siku zote anatamani wachezaji hao wachague kucheza katika timu za mataifa ya Afrika kuliko kuchagua Ulaya.

“Kwangu Mourinho ni kocha wangu bora wa muda wote, ingawa sikukaa naye muda mrefu, ila anaamini katika wachezaji wa kiafrika anawapa nafasi za kucheza na mara zote huwa anashangaa wanapochagua kuchezea timu za mataifa ya Ulaya na kuacha Afrika, anaamini  Afrika tuna vipaji vikubwa zaidi duniani,” anasema Edebayor anayemtaja Cristiano Ronaldo kama ndiye mkali wake katika soka duniani.

Anasema mara nyingi amekuwa akiulizwa nani mchezaji bora wa muda wote kwake na haoni aibu kumtaja CR7 kutokana na nidhamu ya kazi, amekuwa mfano wa kuigwa na vijana wengi.

“Maisha ya Ronaldo kayaweka wazi, kuanzia familia aliyotokea hadi anaibadilisha na kuwa ya thamani, anavyofanya mazoezi utadhani ndio kwanza anayasaka mafanikio na kuwashinda vijana wanaokuja nyuma yake, jamaa ana vitu vingi vya kujifunza kutoka kwake.

“Marafiki zangu wengi na waandishi wamekuwa wakiniuliza nani mchezaji bora kwangu wa muda wote, leo basi nataka kupitia chaombo hiki wajue, mimi ni timu Ronaldo, sina maana kwamba simkubali Messi ila chaguo langu ni hilo.”