Adam Adam ana lake jambo msimu huu

ADAM Adam wa JKT Tanzania ni miongoni mwa mastraika wazawa wenye mabao mengi Ligi Kuu Bara (mabao saba), jambo linalompa ari ya kupambana kuhakikisha msimu huu anaacha alama itakayomfanya akumbukwe.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Adam anafunguka kwamba ndani ya misimu mitatu mfululizo yupo kwenye kiwango kizuri kilichomfanya afikishe mabao 27 akiwa na timu tofauti na anaahidi kufanya makubwa zaidi yatakayomjengea heshima kama ilivyo kwa nahodha wa Simba, John Bocco.
“Ukitaja straika wa kizazi chetu mzawa ambaye ana mabao mengi ni Bocco, hicho ni kitu kikubwa sana kwake kwenye maisha ya mpira. Natamani na mimi niwe na kitu changu cha kutambulisha uwepo wangu,” anasema.
Straika huyo anafunguka mengi kuhusiana na kazi yake ikiwemo jinsi ambavyo Stars ilivyompa heshima mtaani na pia ilivyomfundisha kuwa mchezaji wa mitazamo tofauti katika kazi.
STARS ni HESHIMA
Adam anasema baada ya kuitwa Taifa Stars chini ya kocha aliyetimuliwa, Etienne Ndayiragije, ilimjengea heshima mtaani, ambako awali alionekana si chochote kwa baadhi ya watu na aliwahi kukatishwa tamaa na watu kwamba hatafika popote kwa kazi ya soka, badala yake walimshauri bora angeshika zaidi elimu.
“Ukiachana na heshima, nimejifunza namna ya kuishi kama mchezaji, kujiandaa kisaikolojia kabla na baada ya mechi, kucheza mpira wa ushindani, jinsi ya kuzungumza mbele ya jamii inayotazama kazi zangu na maisha yangu kwa ujumla, kuwa mfano kwa wengine wanaokuja nyuma yangu kuonyesha soka ni ajira.”
Anasema maisha ya kambini na kikosi cha Taifa Stars yalikuwa tofauti na namna alivyozowea kuishi akiwa na timu yake, jambo ambalo limemkaa kichwani na anaamini litakwenda kuzaa matunda.
“Kwanza mnakutana wachezaji wa timu tofauti, wapo waliofanikiwa zaidi na wengine ndio kwanza tuliitwa kwa mara ya kwanza na ilikuwa faraja kubwa sana kwangu, hivyo nilikuwa naona baadhi yao jinsi ambavyo wamejitoa asilimia mia kwenye kazi hiyo,” anasema.
MAUMIVU AsiyoYASAHAU
Msimu wa 2018/19, Mei 28, Adam alivunjika mkono baada ya kuisaidia Tanzania Prisons kusalia Ligi Kuu Bara, akifunga mabao mawili timu ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Lipuli ambayo tayari imeishashuka daraja. Ilikuwaje? Anasimulia kama ifuatavyo: “Wakati nakwenda kufunga niligongana na kipa wa Lipuli dakika ya 85, nilidondoka chini na mkono wangu wa kulia ulipinda palepale, nakumbuka sikunyanyuka tena, nilibebwa hadi Hospitali ya Keizi ipo maeneo ya Mafyati - Mbeya, huko nikafanyiwa upasuaji ndipo nikakaa sawa.”
Anasema: “Japokuwa niliumia mwishoni mwa msimu, iliniumiza ni kitu ambacho siwezi kusahau dakika, tarehe, siku na mwaka. Kiukweli kabla sijafanyiwa upasuaji nilikuwa naangalia mkono wangu hadi naogopa, ila msimu huu nilimaliza na mabao 11, 10 nikifunga na Prisons, moja nilitoka nalo African Lyon ambako nilicheza miezi sita ndipo nikajiunga nao.”
Msimu uliofuata wa 2019/20, Adam alijiunga na JKT Tanzania na alimaliza na mabao tisa, japo anasema hakucheza mechi zaidi ya 10 kutokana na kusumbuliwa na majeraha na msimu huu tayari amefunga saba.
“Ndani ya misimu mitatu mfululizo kiwango changu kilikuwa kizuri, nadhani ndicho kilichangia niitwe Stars, japokuwa wengi wanadhani ni kwasababu ya hat-trick niliyofunga dhidi ya Mwadui timu yangu ikishinda mabao 6-1, lakini pia nilifunga mabao mawili Namungo,” anasema.
AGREY ANAVYOMPA TABU
Adam anasema japo beki wa Azam FC, Aggrey Morris anamtoa jasho wanapokutana kwenye mechi, lakini hataacha kukiri kuwa ni bora kwa muda wote katika Ligi Kuu Bara kwa kipindi anachocheza.
“Aggrey ni beki anayenipa tabu sana nikijua tunakwenda kucheza na Azam FC ananifikirisha, ukimsogelea anakukanyaga hadi wakati mwingine natamani kumuuliza kaka umenipania, lakini ni beki mahiri kabisa kwangu na namkubali kiwango chake akiwepo uwanjani, safu ya timu yake inakuwa nzito.”
Ndani ya miaka mitano aliyocheza Ligi Kuu Bara, Adam anakumbuka pesa zake za kwanza kubwa kuzishika kuwa zilikuwa Sh4 milioni alizoipata akiwa na Majimaji ya Songea alizoziwekeza kwenye mambo ya maendeleo.
“Pesa zote ninazopata kwenye soka huwa nawekeza kwenye maendeleo ingawa siwezi kuyaweka wazi, ikiwemo niliyopata wakati tumekwenda kucheza Chan (mashindano ya soka wachezaji wa ndani Afrika nikiwa kwenye kikosi cha Stars,” anasema.
VIPI ISHU YA UTURUKI
Adam hataki kuongelea ishu ya kwenda kufanya majaribio nchini Uturuki, ingawa anakiri kuwa ni kweli alikwenda na kwamba mwenye mamlaka ya kulizungumzia hilo ni wakala wake anayeishi nje.
“Ninachojua Aprili kila kitu kitakuwa wazi, ila siwezi kuzungumza ni kwa namna gani, lakini pia nilijifunza mengi sana Uturuki kwa muda wa wiki mbili nilizokaa huko, kama kujitambua na kuishi maisha sahihi ya soka, mtazamo wangu kuwa mpana kuliko kushindwa na vitu dhaifu,” anasema.