Abbas Kuka - 1: Siku mchezaji wa Simba alipofia uwanjani

NIMEZALIWA wakati Abbas Said Mhunzi maarufu kwa jina la Abbas Kuka akiwa mchezaji maarufu wa klabu ya Simba. Hata hivyo, kama ungetuona wakati tunafanya mazungumzo ungedhani pengine tunapishana miaka michache. Kuka bado ana mwili mkavu usio na kitambi. Miaka mingi ya utamaduni wa kula kwa adabu na mazoezi tangu angali akiwa mchezaji umemfanya abaki na mwili ambao ukimtazama tu utabaini kwamba ni mtu anayetazama vyema mwili wake.

Jina lake mashuhuri la Kuka alipewa tu na mashabiki wa soka na halikuwa jina halisi. Kuka ni matamshi ya lugha ya Kiswahili ya neno la Kiingereza Cooker linalomaanisha mpishi au jiko na lina sababu yake.

Enzi zake akiwa mchezaji wa Simba – katikati ya miaka ya 1970 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980, Kuka alikuwa akicheza katika nafasi ya kiungo na katika mahojiano yake haya na MwanaSpoti, alisema staili yake ya uchezaji inafanana sana na ya kiungo wa sasa wa Wekundu wa Msimbazi kutoka Uganda, Thaddeo Lwanga.

Lakini inaonekana yeye alikuwa ‘fundi’ kidogo. Maana jina hilo la mpishi alipewa kutokana na namna alivyokuwa ‘akiwapikia’ wenzake nafasi ndani ya uwanja. Baadaye, katika siku zake za mwisho za uchezaji alicheza kama mlinzi wa kati na ndiyo sababu kuna mashabiki ukiwaambia aliwahi kucheza kama kiungo watakubishia.

Kuka ni mmoja wa wachezaji muhimu katika historia ya Simba. Yeye alishiriki katika mechi mbili ambazo historia yake haitafutika katika dunia ya soka la Tanzania. Alishiriki katika pambano la mwaka 1979 jijini Lusaka, Zambia, ambako Simba iliweka historia ambayo haijavunjwa hadi leo barani Afrika kwa kuifunga Mufulira Wanderers mabao 5-0.

Kwa matokeo hayo, Simba iliitoa mashindanoni Mufulira – ambayo ilishinda katika mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam kwa kuifunga Simba mabao 4-0. Kuka hajasimuliwa kuhusu mechi hii, alikuwa sehemu ya waliocheza. Historia ya pili ambayo Kuka anayo kwa Simba ni kwamba yeye alikuwa uwanjani katika siku ile ya Jumapili, Mei 13, 1979, wakati mchezaji mwenzake Hussein Tindwa alipoanguka ghafla uwanjani katika mechi dhidi ya Racca Rovers ya Nigeria na kufariki dunia wakati akipelekwa kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Tindwa anabaki kuwa mchezaji pekee wa Simba kufia uwanjani katika historia ya klabu. Ni msemo maarufu unaotumiwa na wachezaji, mashabiki na viongozi wa klabu mbalimbali kuwa wako tayari kufia uwanjani lakini ni Tindwa pekee ambaye hili limemkuta kwa vitendo. Na hapa ndipo hasa nilipoanzia mazungumzo yangu na Kuka.

“Nakumbuka tukio zima la kifo cha Tindwa kana kwamba lilitokea jana. Kwanza nikwambie kwamba mimi Hussein alikuwa rafiki yangu na mara nyingi tulikuwa tukilala chumba kimoja wakati Simba ilipokuwa kambini.

“Yeye, kama mimi alikuwa akicheza kama mlinzi wa kati na ndiyo sababu ya kuwa na urafiki wa karibu. Siku anafariki dunia tulikuwa tunacheza mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika baada ya kuwatoa Mufulira. Tulicheza na Racca Robers kutoka Nigeria waliokuwa mabingwa wa nchi hiyo wakati huo.

“Simba iliweka kambi Kibaha kujiandaa na mechi. Mimi nakumbuka kwamba tangu asubuhi Hussein hakuwa na furaha. Nilimuuliza asubuhi kwamba mbona leo umeamka kama vile hauna furaha au kuna kitu kimekutokea? Alinijibu kwamba hana tatizo lolote na hajui kwanini yuko hivyo.

“ Tulikwenda kucheza mechi ile na alipangwa kama mmoja wa walinzi wa kati. Alicheza vizuri tu na nakumbuka tatizo lilitokea karibu kabisa na muda wa mapumziko. Ulipigwa mpira wa juu naye akaruka kuokoa na kuanguka chini. Nakumbuka ule mpira ulipookolewa tu ndiyo mwamuzi akapuliza kipyenga cha mapumziko.

“ Wakati tunatoka kwenda vyumbani kwa ajili ya mapumziko nilimwuliza Mohamed Kajole ‘Machela’ (marehemu), kwamba nini kimetokea kwa sababu Tindwa hakuwa ameamka. Kajole alitujibu kwa ishara tu kwamba alikuwa na kizunguzungu. Tukajua ni jambo la kawaida tu na atapata nafuu. Hakupata nafuu na tukaja kuambiwa baada ya mechi kumalizika kwamba alifariki wakati anapelekwa hospitali.

“Maana yake ni kwamba wakati sisi tunaendelea na mechi pale Uwanja wa Uhuru (zamani Uwanja wa Taifa), mwenzetu alikuwa anapigania maisha yake na kukata roho. Sitasahau hali ya huzuni kwangu, wenzangu na mashabiki baada ya msiba huo. Alikufa akiwa kijana kabisa,” anasimulia Kuka huku akiwa anaangalia mbali ya uso wangu.

Kuna uchungu umejificha katika kona fulani ya moyo wake. Kizazi cha wachezaji wa kina Kuka wanaona kwamba mchango wao kwa klabu haujawahi kutazamwa walau kwa jicho tu linalostahili na mashabiki, viongozi na klabu kwa ujumla.

Sio ajabu ananiambia Kuka, kwamba ukiwauliza mashabiki wa Simba ni mchezaji gani aliyewahi kufa akiwa anachezea klabu yao watakutajia kwa haraka jina la Patrick Mafisango au hawatataja kabisa jina.

Mafisango, mchezaji kiraka aliyekuwa akitumiwa zaidi kama kiungo kwenye klabu ya Simba alifariki dunia kwa ajali ya gari Mei, 2013. Wakati anafariki dunia, mimi nilikuwa mmoja wa viongozi wa juu wa klabu na lazima nikiri kwamba wakati ule ningeweza kabisa kutumia msiba ule kukukumbushia vizuri msiba wa Tindwa.

Mwaka 1979, serikali, mashabiki wa soka, wafanyakazi wa iliyokuwa Wizara ya Michezo wakati huo, Baraza la Michezo la Taifa na hata kilichokuwa Chama Cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT), wote walichangia msiba huo. Tangu wakati huo, jina la Tindwa limekuwa likitajwa mara moja moja tu; tena kila kinapotokea kifo cha mchezaji mpira – ndani au nje ya nchi. Lakini, Tindwa kama mojawapo ya alama za kihistoria za klabu, jina lake huwa halipo.


SIMBA VS MUFULIRA

Kuka ni mmoja wa vijana wadogo wa Dar es Salaam waliokuwa wakienda kucheza soka katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa miaka ya 1970. Huko kwenye soka la watoto ndiko kipaji chake kilipoonekana hadi kuchukuliwa kuchezea kikosi cha vijana cha Simba 1972 na baadaye kupata nafasi katika kikosi cha wakubwa.

Wakati kina Kuka wakiibuka Simba ndiyo ilikuwa imetengeneza kikosi kinachohesabika kuwa bora zaidi katika historia ya klabu. Kama isingekuwa fitna za Wamisri 1974 kwenye mechi dhidi ya Mehalla El Kubra huenda Simba ingetwaa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika wakati ule.

Golini kulikuwa na Athumani Mambosasa, anayetajwa kama mlinda mlango bora kabisa kuwahi kuzaliwa Tanzania. Walinzi wa pembeni walikuwa watu wa aina ya Shabani Baraza na Mohamed Kajole – beki tatu ambaye inaelezwa hana mfanowe katika historia ya kabumbu hapa Tanzania.

Timu ilijinasibu kwa kuwa na watu wa aina ya Willy Mwaijibe (marehemu) kwa mara nyingine, winga wa kulia ambaye mfanowe hakuna tangu kuumbwa kwa Tanzania. Na bado walikuwapo nyota wengine wa kiwango cha juu kama kina Adam Sabu, Dilunga na wengine.

“ Haikuwa mchezo kwa mchezaji kutoka timu yoyote, achilia mbali sisi wa timu ya watoto kuja kucheza Simba wakati ule. Ushindani ulikuwa mkali kiasi kwamba siku nawe ukiambiwa sasa uko tayari kuvaa jezi ya timu ya wakubwa, ujue kweli wewe umeiva,” anasimulia Kuka. Namchokonoa kidogo kwa swali la kizushi. Hivi kati ya Mambosasa na Omar Mahadhi bin Jabir, nani alikuwa bora kumzidi mwenzake langoni? “Hilo swali gumu aisee. Nadhani Mambosasa. Lakini kuna wakati hata kocha alikuwa hajui ampange nani. Alikuwa anawaambia ninyi wenyewe mtaamua. Kwa hiyo sisi wachezaji tulikuwa tunaangalia mazoezi yao tu. Yule ambaye tunaona anateswa zaidi na mwenzake mazoezini, tunajua ndiye atacheza”.


IMEANDIKWA NA EZEKIEL KAMWAGA