ABAS KUKA -2: Huyu Manara bonge la staa

Thursday May 19 2022
kuka pic
By Mwandishi Maalum

Katika mahojiano na kiungo wa zamani wa Simba, Abbas Kuka alieleza mambo mbalimbali, lakini pia nilimuuliza swali namna gani alivyowaona mastaa wa zama zile wakiupiga mwingi.. SASA ENDELEA


VIPI kuhusu Sunday Manara na Abdallah Kibadeni? Kuka, ambaye aliwahi pia kucheza na kuwa nahodha wa klabu ya Nyota Nyekundu ya jijini Dar es Salaam, anawaza kidogo na kuja na jibu la kiutu uzima; “Walikuwa wanacheza namba mbili tofauti. Mmoja alikuwa kiungo na mwingine mshambuliaji. Kwa hiyo ni vigumu kukwambia kwa haki nani alikuwa zaidi ya mwenzake.

“Hata hivyo, kuna jambo moja ambalo naweza kukwambia. Sunday alikuwa bonge la mtu. Akiwa na mpira mguuni kumnyang’anya ni shida. Na akiwa na mpira miguuni anaweza kufanya nao kila kitu; atatoa pasi za maana, atapiga chenga, atapiga mashuti yaani kila kitu.

“Kibadeni alikuwa na mwili mdogo tu lakini alikuwa na nguvu sana. Uta-shangaa kwamba katika enzi zake, wengi wa mabeki walikuwa watu wa miraba minne na wenye kutumia nguvu lakini Kibadeni alikuwa anaruka nao na kupambana nao. Kwenye boksi, Kibadeni alikuwa balaa. Lakini kwenye starehe na burudani ya mpira, Manara ni wa pekee,” anasimulia Kuka. Katika mechi zote mbili dhidi ya Mufulira, Abbas Kuka alicheza kama kiungo wa ulinzi. †

Anakumbuka kwamba katika mechi ya

Advertisement

kwanza, kikosi cha Simba kilichoanza kilipangwa ifuatavyo; Athumani Mambosasa, Daudi Salum, Filbert Rubibira, Hussein Tindwa, Kuka, George Kulagwa, Ismail Mwarabu, Abdallah Mwinyimkuu, Thuwein Ally na Ali Hussein.”Nakumbuka kwamba hatukufanya vizuri kabisa katika mechi ya kwanza. Baada ya kipyenga kupulizwa huku tukiwa tumepigwa nne, hadi washabiki wetu wenyewe walitununia.

“Sikumbuki kama tulicheza vibaya sana kwenye ile gemu lakini wenzetu walitumia vizuri karibu nafasi zote walizopata. Kwenye soka, ukipata siku ya namna hiyo ambayo kila anachofanya mwenzako kinakubali, ujue ni siku mdefu hiyo,” anasema Kaka.

Ni muhimu kufahamu kwamba Mufulira pia ndiyo ilikuwa kwenye kilele chake kama mojawapo ya timu bora za Kusini mwa Afrika nyakati zile. Huend benchi la ufundi la Simba halikuwa hata na mkutano mmoja wa kujadili mazuri na upungufu.

Rubibira ambaye naye alicheza mechi zote mbili, alitaja mambo kadhaa yaliyosababisha Simba iweze kushinda 5-0 na kuwa timu pekee kwenye historia ya Afrika kufanya jambo la namna hiyo.

Jambo la kwanza lilikuwa ni maneno ya kutia faraja kutoka kwa viongozi wa timu na kocha wa wakati huo, Joel Bendera. Pia klabu ilikuwa na Katibu Mkuu aliyeitwa Sanga ambaye naye alikuwa akiwatia moyo.

Maneno ya mara kwa mara ya kuwatia moyo ya Katibu Mkuu na Bendera aliyefariki dunia miaka michache yaliwapa hamasa kubwa wachezaji. Ili kuondoa presha ya washabiki na vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kuzoea mazingira ya Zambia mapema, Simba iliondoka Tanzania wiki moja kabla ya mechi.

“Tulipofika Zambia ilikuwa ni mazoezi tu. Tulikuwa tunafanya mara moja kwa siku yalikuwa mazoezi makali. Masaa matatu hadi manne ya kujifua. “Nadhani Mufulira hawakujiandaa vema na marudiano. Wao waliona mechi kama waliimalizia Dar. Siku moja kabla ya mechi, ndiyo nilipata picha ya kwanini nasema hivi. Simba ilifikia hoteli moja inaitwa Andrewís pale Lusaka. Usiku wa kuamkia kwenye mechi, tukaona wachezaji na viongozi wa Mufurira nao wamekuja kulala tunapolala sisi.

“Walipotuona wakawa kama wanatufanyia utani tu wa kutuambia kwanini tumepoteza muda kwenda Zambia. Wakajua wanatupiga nyingi sana. Hawakujua kwamba sisi wiki nzima tulikuwa tunajifua kwa ajili yao,î anasema Rubibira.

Kwa watu niliowahoji, kuna mkanganyiko kuhusu muda ambao magoli yalifungwa. Kuka na Rubibira wote wanakumbuka kwamba Thuwein na Kulagwa ndiyo walifunga magoli yote matano; Thuwein mawili na Kulagwa ambaye mashabiki wakimwita Best kwa kumlinganisha na George Best wa England alifunga mabao mawili.

Hata mzee wa mtaani kwangu amenipa tu taarifa kwamba mechi ile haikutangazwa moja kwa moja na Radio Tanzania (RTD) na badala yake washabiki walikuwa wakidokezwa kidogo tu kuhusu matokeo kutoka Zambia.

Taarifa inayokubalika na wote ni hii; Thuwein kupiga hatrick na kuweka rekodi ambayo haijavunjwa hadi sasa ya Mtanzania kufunga bao tatu ugenini. Na kwamba hadi wakati wa mapumziko, Simba tayari ilikuwa inaongoza kwa mabao matatu. Na Rubibira anasema anakumbuka maneno ya mwisho ya Bendera kabla hawajaingia †uwanjani siku ile.

Aliwaambia wachezaji kwamba wao wanatakiwa kupata ushindi mdogo tu ili kulinda heshima yao. Lakini, baada ya kuona wanaongoza bao 3-0 na Uwanja wa Independence ukiwa umepoa mbele ya aliyekuwa Rais wa Zambia wakati ule, Kenneth Kaunda, Bendera akabadilika kwa kuwaambia †sasa wanaweza kufunga magoli mengi zaidi na kuitoa Mufulira.

Kwa hiyo, kama Simba wana cha kujifunza leo kwenye mechi yao dhidi ya Kaizer ni kwmba wachezaji wanatakiwa kuaminishwa kwamba mechi bado haijaisha. Pili wafanyishwe mazoezi yanayoendana na mechi yao ya leo. Wataalamu wote wa mpiira waliona kwenye mechi iliyopita kwamba aina ya magoli walofungwa Simba ilikuwa karibu inafanana. Pamoja na umuhimu wa mazoezi, ilionekana ni muhimu kwa wachezaji kufanya mazoezi yanayoendana na matatizo yaliyojitokeza mwenye mechi ya awali. Kina Kajole, Thuwein na Kulagwa walikuja kushangaa kuona umati uliokuja kuwalaki Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kama mashujaa. Wachezaji waliopewa kila aina ya majina mabaya, †ghafla wakageuka mashujaa. Kuka anakumbuka vitu viwili kuhusu pambano hilo la aina yake; shuti kali la Thuwein lililoipa Simba bao la tano na la kufuzu na washabiki kulazimisha gari isiendeshwe wakati walipofika nyumbani. Wao walitaka isukumwe tu hadi makao makuu ya klabu yaliyopo Mtaa wa Msimbazi. Baada ya kuondoka Simba, Kuka alitua Nyota Nyekundu na alistaafu mwanzoni mwa miaka 1990 na sasa anaishi Magomeni, Dar es Salaam.


IMEANDIKWA NA EZEKIEL KAMWAGA

Advertisement