Abal Kassim: Mudathir akili mingi, Maxime bab’kubwa

Muktasari:
- Nyota huyo ambaye pamoja na kushindwa kuhudumu kwenye timu amekuwa akionyesha ubora na kuvivutia vilabu vingine kuhitaji saini yake na amekuwa akifanikiwa kusaini, Abal amecheza timu sita hadi sasa huku Pamba Jiji ikiwa ya saba.
UKITAJA nyota sita waliocheza timu zaidi ya tano Ligi Kuu Bara na hawadumu kwa muda mrefu ndani ya timu hizo huwezi kusita kutaja jina la kiungo Abal Kassim ambaye sasa anakipiga Pamba Jiji.
Nyota huyo ambaye pamoja na kushindwa kuhudumu kwenye timu amekuwa akionyesha ubora na kuvivutia vilabu vingine kuhitaji saini yake na amekuwa akifanikiwa kusaini, Abal amecheza timu sita hadi sasa huku Pamba Jiji ikiwa ya saba.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na kiungo huyo ambaye amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sababu kwanini anashindwa kukaa muda mrefu ndani ya timu huku Mtibwa Sugar ikiwa ndio timu aliyocheza kwa muda wa miaka miwili.
THAMANI YA WAZAWA
Kiungo huyo ambaye alianza kucheza Tanzania Prisons kwa timu za Ligi Kuu amesema sababu za kushindwa kuhudumu kwenye timu kwa muda ni timu hizo hasa ambazo zina nyota wa kigeni kushindwa kuthamini wazawa.
“Sisi wachezaji wa Kitanzania hatupewi thamani haswa kwenye pesa na ndio maana wachezaji wamekuwa wa kuhama hama kinachotafutwa ni fedha na sio kingine kama uwezo wa kucheza kila mmoja anaona,” anasema.
“Kinachobadilika kwetu na wachezaji wa kigeni ni uraia tu, lakini wenzetu wanapewa kipaumbele sana na kujaliwa kwenye kila kitu na kuna wengine wanakaa benchi, lakini kiasi cha fedha wanacholipwa ni kikubwa. Hii sio nzuri kwa afya ya mpira hasa kwetu.”
MUDATHIR AKILI MINGI
Licha ya viungo wengi bora waliopo ndani ya ligi ya Tanzania Bara Kassim amemchagua Mudathir mchezaji wa Yanga kuwa ndio kiungo wake bora kutokana na upambanaji na utulivu alionao akiwa na umiliki wa mpira.
“Ni kweli ligi yetu ina viungo wengi bora wa ndani na kutoka mataifa mbalimbali lakini kwangu Mudathir ni bora licha ya kutokuwa mtulivu lakini upambanaji wake umekuwa ukimpa nafasi ya kuonekana mchezaji bora na muhimu,” anasema na kuongeza:
“Mudathir ni mpambanaji sio mchezaji wa kukubali kushindwa amekuwa imara na ndio maana kila kocha ambaye amepita ndani ya kikosi cha Yanga tangu ameungana nayo amekuwa akipata nafasi ya kucheza.”
MILIONI 3 HADI BARA
Licha ya kucheza timu nyingi za Bara, Abal ni kiungo kutokea Zanzibar na alipata bahati ya kuvuka Bara baada ya kuushawishi uongozi wa Tanzania Peisons kutokana na ubora wake uwanjani na ndio timu iliyomvusha maji.
“Nilijiunga na Tanzania Prisons nikitokea Zanzibar, walinisajili kwa Sh3 milion ambazo nakumbuka nilifanyia mahitaji yangu ya mpira kama viatu na kuanzia maisha ya kujitegemea nikishirikiana na dada yangu,” anasema.
“Hiyo ndio ilikuwa pesa yangu kubwa ya soka niliyowahi kupewa tangu nimeanza kucheza soka nilifurahi sana na niliahidi kupambana zaidi ili kukuza kiwango cha fedha pale timu nyingine zitakaponihitaji nafurahi imekuwa ivyo sasa lakini bado nahitaji kupambana zaidi.”
NAMBA YA JEZI HAICHEZI
Kwa mujibu wa kanuni wachezaji wote wanaocheza mechi yoyote ya mashindano wanatakiwa kuvaa jezi zenye namba mgongoni na wengi wamekuwa wakivaa kwa maana fulani ilhali wengine ni kutokana na kufuata nyayo za mastaa waliowatangulia, lakini Abal ni tofauti. “Ni kweli kila mchezaji anavaa jezi namba kwa sababu huku wengine ikiwa ni tarehe au mwezi wa kuzaliwa kwangu haipo hivyo navaa jezi yoyote bila kujali au kumtazama mtu,” anasema.
“Jezi haichezi upambanaji na kujituma uwanjani ndio siri ya mafanikiio mimi sijawahi kuchagua jezi namba kila timu niliyowahi kucheza na huwa sijawahi kuamini katika jezi namba fulani.”
NI MTIBWA TU MIAKA 2
Kiungo huyo mshambuliaji ambaye anatambulika kwa kuhudumu muda mrefu Mtibwa Sugar ambayo amecheza kwa muda mrefu na kaweka wazi sababu za kufanya hivyo.
“Nimecheza Mtibwa Sugar misimu miwili kwa ubora ni baada ya kutolewa kwa mkopo kutoka Azam FC ambapo nilikosa nafasi ya kucheza mara kwa mara hivyo ili kurudi sokoni niliamua kuwekeza nguvu na kupambana ili nipate nafasi ya kutoka tena,” anasema.
“Pia niliaminiwa na kupewa nafasi tofauti na timu nyingine nilizopita ubora na upambanaji wangu ilinifanya nihudumu muda mrefu ndani ya timu hiyo kabla haijashuka daraja.”
AITAJA NJOMBE MJI
Kiungo huyo mshambuliaji ni fundi wa kupiga mashuti makali nje ya 18 na mwenyewe anasema kwenye mabao mengi aliyofunga bao lake bora ni dhidi ya Njombe Mji akiwa Tanzania Prisons.
“Nimefunga mabao mengi bora na magumu lakini bao langu bora la muda wote nililifunga kwenye mchezo dhidi ya Njombe Mji nikiwa Prisons,” anasema.
“Namna nilivyofunga ni ngumu kidogo kuelezea kwa walioutazama ule mchezo wanaweza kuelewa kwanini nimelichagua kuwa bao langu bora hadi muda huu licha ya kufunga kwenye timu nyingine tano nilizopita baada ya kuondoka huku.”
MAXIME MIPANGO
Sio nyota wote ambao wakitolewa kwa mkopo wanaweza kuendeleza ubora wengi wao wa nashtuka zaidi viwango vyao, lakini Abal yupo tofauti kama anavyodai mwenyewe.
“Nilisajiliwa na Azam FC baada ya kuonyesha uwezo mzuri nikiwa Kagera Sugar sikuwa na wakati mzuri ndani ya timu hiyo kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara hadi hapo walipoamua kunitoa kwa mkopo Mtibwa Sugar.
“Nilifurahia kujiunga na Mtibwa Sugar ambayo ilikuwa chini ya kocha Mecky Maxime ambaye aliniamini na kunipa nafasi ya kucheza nilikuwa na furaha sana kwani nilikuwa nacheza na ndio sababu ya kuhudumu kwa muda mrefu,” anasema mchezaji huyo.
Abal anasema amepita chini ya makocha wengi lakini Mexime kwake ni bora kwa sababu alimuamini na alikuwa anapenda sana aina ya uchezaji wake hivyo alikuwa sehemu sahihi na wakati sahihi kitu ambacho kilimfanya arudi kwenye ubora wake.