Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

2022 ulikuwa mtamu kwa Simbu, mchungu kwa Mwakinyo

WAKATI mwaka 2022 ukielekea ukingoni, siku 365 za mwaka huu zimefuatana na matukio mbalimbali ya kufurahisha na kusikitisha kwenye maeneo tofauti ikiwamo michezo.

Mwaka huu haukuwa mzuri kwa nyota wa ndondi, Hassan Mwakinyo huku nyota wa mchezo wa riadha, Alphonce Simbu akiumaliza kwa mafanikio.

Mbali na nyota hao, mwaka 2022, pia umeiweka Tanzania kwenye rekodi mpya ya kuwa kati ya mataifa yaliyoshiriki Olimpiki ya majira ya baridi.

Nzumbe Nyanduga alikuwa Mtanzania wa kwanza kushiriki Olimpiki ya barafu ambayo ilifanyika nchini China, hapa nchini ilizinduliwa Februari 5 kwenye ubalozi wa China.

Nyanduga, mwanamichezo anayeishi Uswisi, alitajwa kuiwakilisha nchi kwa mara ya kwanza kwenye Olimpiki hiyo ya barafu.

“Anakimbia mbio za nyika na maandalizi yake alifanyia nje ya nchi na kufuzu Olimpiki, huyu ni Mtanzania wa kwanza kushiriki Olimpiki ya barafu,” alisema Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi.


MWAKINYO AANZA KUPOROMOKA

Ulikuwa ni mwaka mgumu kwa Mwakinyo ambaye aliuanza kwa kuporomoka kwenye renki, Februari 11, Mwakinyo aliporomoka kwa nafasi tano kutoka ya 10 ambayo ilikuwa ni rekodi ya juu kwake kwenye ubora.

Mwakinyo mwaka 2018, alipanda hadi nafasi ya 14 ya ubora alipomchapa kwa Technical Knock Out (TKO), Sam Eggington aliyekuwa namba nane wa dunia kwenye uzani wa super welter.

Baadaye alipanda hadi kwenye 10 bora kabla ya kuanza kuporomoka kuanzia Februari mwaka huu, ingawa mwenyewe alikaririwa akisema kuporomoka huko siyo kwa kiufundi na ana matarajio ya kurejea upya kwenye renki, lakini hadi anafunga mwaka, bondia huyo alizidi kuporomoka nchini, Afrika na kidunia na kupoteza nyota moja kati ya nne alizokuwa akimiliki.


MWAKA WA SIMBU, NDONDI TAIFA

Kwa Simbu ilikuwa mwaka wa neema baada ya kushinda medali ya fedha ya Jumuiya ya Madola. Alivunja rekodi ya miaka 16 ya riadha, ambayo mara ya mwisho kutwaa medali ilikuwa 2006, kwenye michezo ya Australia.

Mbali na Simbu, mabondia Kassim Mbundwike na Yusuph Changalawe walitwaa medali za shaba kwenye mashindano hayo yaliyofanyika nchini England.


MTANZANIA ASHTUA MAREKANI

Kiwango cha mwanariadha bingwa wa taifa wa mbio za mita 800 na 1500, Regina Mpigachai kilimshtua kocha wa timu ya riadha ya chuo cha Northern Colorado, Wayne Angel, anaposoma mwanariadha huyo aliyepata ofa ya masomo na michezo nchini Marekani akitokea sekondari ya Filbert Bayi.

Wiki kadhaa baada ya kuwasili chuoni hapo, Regina alivunja rekodi ya chuo hicho ya dakika 10:01 alipokimbia kwa dakika 09:49 mbio za mita 3000 kwenye mashindano ya ndani ya chuo cha Texas Texh huko Lubbock, Texas.

Kabla ya rekodi hiyo, Regina alikimbia mita 800 na kutumia dakika 02:12:08 kwenye mashindano ya chuo cha Nebraska ambako alitwaa medali ya fedha.


SERIKALI YATANGAZA NEEMA

Utakuwa ni mwaka wenye kumbukumbu nzuri kwa timu zilizoshiriki michezo ya Jumuiya ya Madola baada ya Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kutangaza kubeba jukumu la kambi ya timu hizo.

Hiyo ilikuwa ni Februari 14, katibu mkuu wa BMT, Neema Msitha alipotangaza Serikali kubeba jukumu hilo kwa timu zilizoiwakilisha nchi kwenye Madola na vyama vya michezo husika kupunguziwa mzigo.


RAIS WA FINA AZURU TZ

Machi 14, Rais wa Shirikisho la kuogelea la dunia (Fina), Husain Al Mussalam akiwa na viongozi wengine walifanya ziara nchini.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Inviolata Itatiro alisema ziara hiyo iliambatana na warsha ya mchezo huo ambao iliwahusisha wadau mbalimbali.


KAMBI YA MADOLA YAVUNJIKA

Kati ya matukio yaliyoacha fedheha ni la kambi ya riadha kuvunjika na wachezaji waliokuwa kambini wakijiandaa na michezo ya Jumuiya ya Madola kurudi nyumbani.

Japo Serikali kupitia kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Singo na kaimu katibu mkuu wa RT, Jackson Ndaweka walikuwa na kauli tofauti juu ya kambi hiyo kuvunjika wakidai sio kweli, baadhi ya wanamichezo walifichua kwamba hawakuona sababu ya kuendelea kubaki kambini hapo huku wakinyanyasika.

“Tumeamua kurudi nyumbani, wale wa mikoa mingine nje ya Arusha pia walilala kwa kiongozi wakisubiri nauli kutoka kwa rais wa RT ili nao waondoke,” alisema mmoja wa wachezaji, ingawa baadaye walirudishwa kambini na kuendelea na mazoezi huku madai ya kutolipwa posho zao pia yakiibuka, jambo ambalo lilirekebishwa baadaye.


CLASS, MWAKINYO WAVULIWA UBINGWA

Upepo mbaya uliendelea kumwandama Mwakinyo ambaye alivuliwa ubingwa wa WBF sanjari na Ibrahim Class.

Class alishinda taji hilo Januari 29, 2021 alipomchapa Denis Mwale na kuwa bingwa wa Mabara wa WBF kwenye uzani wa light wakati Mwakinyo alilitwaa Agosti 14, 2020, alipomchapa Bebe Rico Tshimanga na kulitetea Novemba 12, 2020 kwa Jose Carlos Paz kwenye uzani wa super welter

Wote walivuliwa mataji hayo Januari 20, mwaka huu na kutangazwa sio mabingwa tena wa WBF.

Miezi michache baadaye Mwakinyo alivuliwa ubingwa mwingine wa Afrika (ABU) ikiwa ni wiki chache kabla ya kupigwa na Liam Smith kwa TKO huku akiporomoka mara kadhaa kwenye ubora.


MANDONGA AMPIGA MBELWA KO

Ni matokeo ambayo yaliwashtua wadau wengi wa ndondi nchini mwaka huu baada ya Said Mbelwa bondia mzoefu kuchapwa kwa KO na Karim Mandonga.

“Nilicheza lile pambano nikiwa na fikra za kumuokoa zaidi Mandonga kwa kuwa uwezo wa Mbelwa naufahamu, lakini ilikuwa ni tofauti, Mbelwa alizidiwa kuanzia raundi ya kwanza,” alisema Anthony Rutha, refarii wa pambano hilo.

Bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka alisema alichokishuhudia ulingoni ni tofauti na alichokitarajia.

“Safari hii Mandonga inaonyesha amefanya mazoezi sana, alikuwa fiti muda wote kulinganisha na mpinzani wake,” alisema.


GEAY AVUNJA REKODI

Ukiachana na Sh450 milioni ambazo Gabriel Geay, Simbu na Failuna Abdi walitakiwa kulipwa baada ya kushinda kesi dhidi ya Multichoice ambayo ilitumia picha zao bila ridhaa yao, kwa Geay mwaka huu pia ulikuwa na rekodi mpya kwake.

Geay licha ya kutwaa medali ya fedha kwenye mbio za Valencia Marathoni, pia aliweka rekodi mpya ya taifa ya marathoni ya saa 2:03:00.

Awali yeye ndiye alikuwa akishikilia rekodi hiyo kwa saa 02:04, muda ambao ameuboresha zaidi kwenye Valencia marathoni.

Kabla ya rekodi hiyo, Geay aliingia kwenye nane bora ya dunia katika mbio za marathoni alipomaliza wa saba kwenye mashindano ya dunia mwaka huu huko Marekani.


RT WAFUKUZWA UKUMBINI

Lilikuwa tukio la kufungia mwaka kwenye riadha baada ya washiriki wa mkutano mkuu na uchaguzi mdogo wa RT kufukuzwa ukumbini, tukio lililotokea Novemba 27 kwenye ukumbi wa Magereza, Msalato jijini Dodoma baada ya kutolewa tangazo la wajumbe kuondoka ukumbini ndani ya dakika 10.

“Hii ni order ‘agizo’ kutoka kwa mkuu wa jeshi, tunawapa dakika 10 wote muwe nje ya geti,” lilitoka agizo hilo kabla ya RT kuamua kutafuta ukumbi mwingine na kuendelea na mkutano mkuu na uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya makamu mwenyekiti na mjumbe mwakilishi wa kanda ya Pwani.


PAMBANO LAVUNJIKA

Kwenye ngumi, mwaka huu pia umeacha kumbukumbu ya pambano la Samuel Muloko wa DR Congo na Meshack Mwankemwa kuvunjika kabla huku bondia wa Congo akizichapa kavukavu na mashabiki.

Ilikuwa kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, ambapo Kamisheni ya ngumi za Kulipwa Tanzania ilizuia pambano hilo kabla kwa kile ilichoeleza kuna masharti promota hakuyatimiza, hivyo wakati mabondia wakiwa ukumbini bila kujua hatma ya pambano, Mcongo akawakebehi wapinzani kuwa wasiogope wapande ulingoni kuzichapa, hapo ndipo zogo lilipoanzia kwa mmoja wa mashabiki wa Mwankemwa kumzonga na kumfanyia vurugu.